loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Samia na uteuzi wa kimkakati

WASOMI na wachambuzi wa masuala ya uchumi na siasa wameuelezea uteuzi na mabadiliko ya nafasi za makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na wakuu wa taasisi za serikali yaliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa yana matumaini makubwa kwa mustakabali wa nchi.

Wakizungumza na HabariLEO kwa nyakati tofauti jana, wasomi na wachambuzi hao walisema Rais Samia hajafanya mabadiliko makubwa ya watu waliokuwa kwenye nafasi hizo, lakini kuwaweka watu katika nafasi kulingana na maeneo ya ubobezi ya kitaaluma anatarajia kupata matokeo chanya zaidi.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Profesa Raphael Chigunda alisema: “Ni kitu chema, Mheshimiwa Rais anajaribu kuunda timu kama alivyosema wakati anamtambulisha Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kwamba ataendana naye. Anajaribu kumpeleka mtu mahali alipo na uzoefu kitaaluma kwa nia njema zaidi.”

Alitoa mfano wa Katibu Mkuu, Profesa Riziki Shemdoe aliyehamishiwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutoka Katibu Mkuu Viwanda na Biashara, kuwa ni mzoefu katika Tamisemi kwa kuwa alishawahi kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma (RAS).

“Tuna matumaini makubwa na serikali anayoipanga itaendeleza yalioachwa na hayati Dk John Magufuli na kuibua mapya ili kusukuma uchumi wa nchi. Ni mabadiliko yenye afya, ninavyoyaona mimi yamejaa matumaini yenye tija kwa nchi. Si mabadiliko makubwa ya wapya bali ni hao hao lakini anajaribu kuwaweka katika maeneo ya ubobezi ya kitaaluma, sisi wasomi tunayapokea kwa matumaini makubwa,” alisema Profesa Chigunda.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Idara ya Uchumi, Dk John Mtui alisema mabadiliko hayo yamewarejesha wachache waliokuwa na nafasi kipindi cha nyuma pengine kwa kuwa ana imani nao na kuwaweka katika maeneo ya ubobezi kama njia ya kuleta ufanisi zaidi.

“Rais amejaribu kuwaweka katika maeneo ya ubobezi zaidi, ukifanya hivi kwa kuweka katika nafasi zao za kitaaluma kuna kuwa na mafanikio zaidi, ni matumaini kwamba mambo yatakuwa mazuri, kuna vitu vingi Rais aliyepita amefanya vizuri kwa mabadiliko haya vitaendelea,” alisema Dk Mtui. 

Alisema pamoja na kwamba si lazima mtu akiwekwa kwenye nafasi aliyosomea afanikiwe, lakini kwake yeye taaluma ya mtu, uelewa wa mtu ni kitu cha msingi zaidi kwani kutegemea watu wengine kutatua tatizo usilokuwa na taaluma nalo, kunachelewesha matokeo chanya hivyo hatua hiyo itawaongezea walioteuliwa kujiamini kwa kuwa ni maeneo yao ya kitaaluma.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (Tudarco), Danford Kitwana alisema mabadiliko hayo yapo nusu kwa nusu kwa kuwa inawezekana mtu akapewa nafasi kulingana na taaluma yake bado akashindwa kufikia malengo kwa kuwa uongozi ni zaidi ya taaluma.

“Uongozi wa kisiasa ni zaidi ya taaluma ulinayo, unaweza kuwa na taaluma usiweze kuwa kiongozi mzuri. Upande wa pili wa shilingi inaweza kusaidia kama wanataaluma watatumia taaluma zao vizuri kusaidia sekta husika kama sheria, uchumi na nyinginezo, inategemea zaidi utashi wa kisiasa wa kiongozi husika,” alisema Kitwana.

Wakati Kitwana akisema hayo, Mhadhiri wa UDSM, Dk Richard Mbunda alisema: “Ninachoona ni kwamba mabadiliko ni machache, lakini ni uteuzi wa mwendelezo wa sera kutoka awamu moja kwenda nyingine.”

“Wananchi wana maswali mengi kama kweli kutakuwa na muendelezo wa sera zilizokuwepo au la. Mabadiliko haya machache yana muelekeo huo wa muendelezo wa kisera zaidi, inawezekana falsafa ikabadilika lakini angalau hizi zinaonesha muendelezo wa mtangulizi,” alisema Dk Mbunda.

Alisema ili malengo fulani yatimizwe, ni lazima atafutwe mtu mwenye uwezo aliyebobea katika eneo hilo anayeweza kusaidia kuyafikia na mwenye kuelewa anachopaswa kukifanya. 

“Mabadiliko haya ni kitu chema na sisi wachambuzi tutakuwa na maswali zaidi pale asiyeendana na taaluma anapelekwa katika nafasi fulani inayohitaji taluma zaidi, lakini hii ya mtu kubadilishwa na kuwekwa eneo la ubobezi inaleta matumaini zaidi,” alisema Dk Mbunda. 

Uteuzi mpya

Juzi Jumapili, Rais Samia aliteua makatibu wakuu wa wizara, naibu makatibu wakuu na wakuu wa taasisi.

Katika uteuzi huo baadhi walihamishwa, wengine waliachwa na wachache wapya wamechukua nafasi. Wateuliwa hao wanaapishwa leo, Ikulu, Dar es Salaam.

Waliohamishwa

Katika uteuzi huo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James amehamishiwa Wizara ya Viwanda na Biashara kuendelea na nafasi hiyo.

Aidha, Joseph Malongo aliyekuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Wizara hiyo ina makatibu wakuu wawili.

Profesa Riziki Shemdoe aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tamisemi, huku Joseph Malongo akiteuliwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi) kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Ludovick Nduhiye katika uteuzi huo amehamishwa na kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii.

Waliopanda 

Katika uteuzi huo wapo naibu makatibu wakuu waliopanda na kuwa makatibu wakuu akiwemo Mary Maganga aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango ambaye sasa ameteuliwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Mwingine ni Dk Allan Kijazi aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii. Awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu katika wizara hiyo.

Rais Samia pia alimteua Gabriel Migire kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi) ambaye awali alikuwa Kaimu Katibu Mkuu sekta ya Uchukuzi.

Makatibu wakuu wapya

Rais Samia katika uteuzi huo, amewateua makatibu wakuu wapya, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba. 

Kabla ya uteuzi huo, Tutuba amewahi kuwa Katibu Tawala (RAS) Mkoa wa Mwanza na amefanya kazi pia kwenye kitengo cha bajeti katika  wizara hiyo.

Mwingine ni Profesa Godius Kahyarara aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji. Kahyarara aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Rais pia alimteua aliyewahi kuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Abel Makubi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Afya).

Pia alimetua Dk Hashil Twaibu Abdallah kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara.

Uteuzi huo pia umemuibua Dk Carolyne Nombo aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Elimu ya Msingi, Elimu ya Sekondari na Ufundi Stadi).

Makatibu wakuu walioachwa

Katika mabadiliko hayo baadhi ya makatibu wakuu wameachwa akiwamo Dorothy Mwaluko, aliyekuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera na Uratibu), Joseph Nyamhanga (Tamisemi), Elius Mwakalinga aliyekuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya Ujenzi).

Wengine ni Dk Aloyce Nzuki, aliyekuwa Wizara ya Maliasili na Utalii na aliyekuwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Afya), Profesa Mabula Mchembe.

Wanaoendelea na nafasi zao

Dk Hassan Abbas amebaki kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, huku nafasi yake ya Msemaji Mkuu wa Serikali akiteuliwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa. Aidha, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ni Dk Ali Possi.

Dk Moses Kusiluka ameendelea kuwa Katibu Mkuu Ikulu, huku naibu makatibu wakuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) wakibaki Jerald Mweli (Elimu) na Grace Maghembe (Afya). 

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ni Dk Laurian Ndumbaro na Naibu wake ni Dk Francis Michael. Katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Katibu Mkuu anayeendelea ni Mohammed Abdallah Khamis.

Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Katibu Mkuu ni Tixon Tuyangine Nzunda, Naibu Katibu Mkuu ni Profesa Jamal Katundu na Caspary Muya.

Wizara ya Fedha na Mipango, naibu makatibu wakuu watatu wameendelea na nafasi zao ambao ni Adolf Ndunguru, Amina Khamis Shaaban na Dk Khatibu Kazungu. 

Wizara ya Katiba na Sheria, Katibu Mkuu amebaki Sifuni Mchome na Naibu Katibu Mkuu ni Amon Mpanju. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Katibu Mkuu ni Dk Faraj Mnyepe. 

Aidha, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wilbert Ibuge ameendelea kushika nafasi hiyo na Naibu Katibu Mkuu ni Balozi Fatma Rajab. 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni Christopher Kadio na Naibu Katibu Mkuu ni Ramadhan Kombwey. 

Katika Wizara ya Madini, Katibu Mkuu amebaki Simon Msanjila. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Katibu Mkuu ni Mary Makondo na Naibu Katibu Mkuu ni Nicholas Mkapa. Wizara ya Maji, Katibu Mkuu ni Anthony Sanga na Naibu wake ni Nadhifa Kemikamba.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Katibu Mkuu ni Dk Leonard Akwilapo na Naibu Katibu Mkuu ni Profesa James Mdoe (Elimu, Sanyansi na Teknolojia).

Kwa upande wa Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) amebaki Dk John Jingu. 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ni Profesa Siza Tumbo. Aidha, Wizara ya Mifugo na Uvuvi makatibu wakuu ni Dk Rashid Tamatamah (Uvuvi) na Profesa Elisante Gabriel (Mifugo). 

Wizara ya Nishati Katibu Mkuu ni Leonard Masanja na Naibu Katibu Mkuu ni Kheri Mahimbali, huku Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Katibu Mkuu ni Dk Zainabu Chaula na Naibu Katibu Mkuu amebaki kuwa Dk Jim Yonazi.

Mabadiliko wakuu wa taasisi

Katika mabadiliko hayo, Rais Samia amewaondoa waliokuwa wakuu wa taasisi mbalimbali za serikali akiwemo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko ambaye amesimamishwa kupisha uchunguzi, sasa nafasi yake ameteuliwa Erick Hamis.

Mabadiliko hayo pia yalimuhamisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya baada ya kumteua kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya akichukua nafasi ya James Kaji.

Rais Samia pia amefanya mabadiliko katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kumteua Alhayo Kidata kuwa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo kuchukua nafasi ya Edwin Mhede, huku Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) akiteuliwa Dk Jabir Kuwe anayechukua nafasi ya James Kilaba.

Dk Kuwe kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA)

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) aliyeteuliwa ni Kaimu Mkeyenge aliyechukua nafasi ya Emmanuel Ndomba.

Uteuzi mwingine ni wa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichwale na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba.

Ateua na kutengua uteuzi

Aidha, ndani ya saa 11, Samia aliteua na kutengua uteuzi wa Thobias Richard kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kumrejesha James Mataragio kuendelea na nafasi hiyo.

Viongozi wa taasisi waliotemwa

Mbali na Kakoko wa TPA, Ndomba wa TASAC na Kilaba wa TCRA, wakurugenzi wengine wa taasisi ambao hawakuteuliwa tena ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), William Erio.

SERIKALI inakusudia kurejesha mfumo wa maendeleo ya sanaa ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi