loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kamati Maalumu kuundwa tatizo la Covid-19

RAIS Samia Suluhu Hassan anakusudia kuunda kamati ya watalaamu ili waangalie kwa upana na kitaalamu tatizo la covid 19 na kuishauri serikali juu ya hatua sahihi za kuchukua kupambana na ugonjwa huo.

Akizungumza baada ya kuwaapisha makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu Ikulu, Dar es Salaam jana, Rais Samia alisema suala hilo halifai kunyamaziwa na kwamba kamwe Tanzania haiwezi kujitenga kama kisiwa.

“Suala la Covid-19, nakusudia niunde kamati ya wataalamu waliangalie kwa upana wake kitaalamu halafu watushauri serikali, haifai kulinyamazia watalaamu watatuambia upeo wa hili likoje hatuwezi kujitenga kama kisiwa bila kufanya tafiti za kweli,” alieleza Rais Samia.

Alisema wataalamu hao wataangalia tiba zinazotumika na kuja na suluhisho kwa upana wake kitalaamu na kuishauri serikali.

“Halifai kulinyamazia, aidha kulikubali au kulikataa bila utafiti wa kitaalamu, tutafanya tafiti za kitaalamu kupitia watalaamu wetu watuambie upeo wa suala hili lilivyo na hayo yanayopendekezwa na ulimwengu je yakoje kitaalamu tena kupitia watalaamu wetu wa ndani,” alisisitiza.

Alisema kutokana na hayo anakusudia kuunda kamati hiyo kwa kuwa Tanzania haiwezi kujitenga na haiwezi tu kupokea yanayoletwa bila kufanya utafiti wake.

“Rais Kikwete alituambia akili za kuambiwa changanya na zako kwa hiyo na sisi tuweke na akili zetu tuwe na msimamo unaoeleweka. Sio tunasoma mambo ya Covid-19 ulimwenguni, lakini Tanzania deshi deshi deshi haieleweki, tueleweke kama tunakubali au tunakataa tunafanyaje tueleweke,” alisema Rais Samia.

Alisema katika eneo la utalii, atawatumia wataalamu katika kamati hiyo atakayoiunda pia kutafiti namna ambavyo watalii kipindi ambacho mataifa yote yanapambana na corona walivyokuja nchini na namna ya kuwarejeshea tena kuiamini Tanzania.

“Tanzania tulibahatika kuwa nchi ya kwanza kutembelewa na watalii kipindi kile cha corona. sasa tutaomba kamati hii iangalie namna ya kuwarejeshea imani ili waje kwa wingi katika shughuli za utalii,” alisema Rais Samia.

Tangu mgonjwa wa kwanza wa corona agundulike nchini Machi 16, 2020, Tanzania ilichukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo kwa kufuata taratibu za kisayansi pamoja na kutumia njia za asili kutibu ugonjwa huo ambao hivi karibuni imelipuka tena dunia kwa kiwango cha kutisha.

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi