loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Jafo ahimiza vijana kuenzi Muungano

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Selemani Jafo amewaasa vijana waendelee kuuenzi Muungano kwa kudumisha amani.

Jafo alitoa rai hiyo jana baada ya kuhudhuria dua  kumuombea aliyekuwa Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Abeid Aman Karume.

Alisema katika ofisi za CCM Kisiwandui kuwa, vijana wanapaswa kuona fahari ya Muungano na kuenzi yaliyoachwa na Karume kwa kuwa aliacha alama Zanzibar hasa katika ujenzi wa miundombinu na kuwajali wananchi.

Jafo alisema kiongozi huyo alikuwa na maono makubwa kwa wananchi wake na alikuwa mfano wa kuigwa kwa viongozi wengine nchini na Afrika kwa ujumla.

"Tukumbuke kwamba Hayati Karume na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere walifanya kazi kubwa ya kuasisi Muungano na leo hii tunajivunia kuwa Watanzania hivyo kwetu sisi ni faraja hatuna nchi nyingine isipokuwa ni Tanzania," alisema.

Jafo alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi kwa uongozi wake ambao umewafanya wananchi kuwa na imani  kwake.

Alitoa rai kwa Watanzania kumuunga mkono Dk Mwinyi kwa anayoendelea kuyatekeleza na kuwa ameonesha weledi katika utendaji wake ambao unaakisi aliyofanya Hayati Karume hasa katika ujenzi wa makazi bora kwa wananchi.

Aprili 7 ya kila mwaka ni kumbukumbu ya kifo cha Karume ambaye aliaga dunia kwa kupigwa risasi mwaka 1972 kwenye ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui.

Dua ya kumuombea ilifanyika katika ofisi hizo ambapo rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na viongozi mbalimbali walishiriki.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Zanzibar

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi