loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Walimu watakiwa kujiunga na benki yao

KATIBU MKuu wa Chama cha Walimu (CWT) Deus Seif amewataka walimu nchini kujiunga na Benki ya Walimu Tanzania (MCB) ambayo licha ya kupata mikopo, watakuwa wanahisa na hatimaye ikipata faida watapata gawio.

"Tusimame na benki yetu... turudi benki yetu huko mikopo ipo kwa riba nafuu," alisema Seifu wakati akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma.

Seif aliwataka pia walimu kuacha utamaduni wa kupitisha fedha zao katika benki nyingine kwani tayari wana benki yao ambayo itawasaidia kupata gawio tofauti na mahali pengine.

Seif alisema inashangaza kuona benki ya walimu ambao ni zaidi ya asilimia 56 ya watumishi, wameshindwa kutumia fursa ya uwepo wa benki yao kwa faida yao.

Alisema katika kuhakikisha walimu wanapoenda benki hawakosi mikopo au huduma nyingine za kifedha, CWT imetoa sh bilioni tano ili kuongeza mtaji na hivyo kupanua uwigo wa fursa kwa walimu kupata mikopo na huduma nyingine katika benki hiyo.

Aliwataka walimu watumie benki yao, kwani inashangaza kwa watu wote kwamba chombo hicho kimeanza kwa ajili yao, lakini ni asilimia ndogo tu ya walimu ndiyo wamejiunga au wana akaunti katika benki hiyo.

Seifu alisema mkakati wa CWT ni kuona mikopo ya walimu inashuka kutoka asilimia 16 ya sasa hadi kwenda tarakimu moja ili kuhakikisha walimu wanafaidi na huduma bora za benki yao na kupata mikopo yenye riba nafuu.

Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Richard Makungwa alisema benki hiyo ni kwa ajili ya walimu na wao wana hisa asilimia 35 ya umiliki wa benki hiyo.

Alisema katika idadi ya walimu 217, 000 ni walimu takribani 41,000 tu wamejiunga na benki hiyo ndio wanafaidi na huduma bora zinazotolewa na benki hiyo.

Makungwa alisema kwa sasa benki hiyo ina wakala 180, ina mashine za ATM pamoja na benki nyingine ili kuhakikisha kwamba mwalimu anaweza kutoa fedha mahali popote.

Makungwa alisema tangu Oktoba mwaka jana benki hiyo imeanza kutoa mikopo na mwalimu anaweza kupata mikopo pamoja na huduma kama mikopo ya viwanja na huduma ya jikimu mwalimu.

Alisema pia wameanzisha huduma ya walimu wataaafu kupokea malipo kwa haraka kupitia benki hiyo na pia inatoa huduma ya kutoa mikopo kwa wanastaafu nahata kuruhusu kupokea mafao yao kupitia benki hiyo.

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi