loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mahakama yataka mawakili watekeleze wajibu

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu mkoani Dar es Salaam, imewataka mawakili na wadau wa Mahakama kutekeleza wajibu wao kwa kusimamia kanuni zilizowekwa kisheria katika usikilizwaji wa mashauri.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Godfrey Isaya, aliyasema hayo wakati akisikiliza kesi ya uhujumu uchumi Namba 8 ya Mwaka 2020 inayomhusu Mkurugenzi wa Jaruma General Supplies Ltd, Lucas Mallya na wenzake watano.

Aliyasema hayo pia aliposikiliza kesi Namba 87 ya Mwaka 2020 inayomhusu Meneja wa Fedha wa Kampuni ya Bevico Ltd, Joseph Rwegasira, zilizopelekwa mahakamani kwa ajili ya kutajwa.

Mahakama ilielezwa kuwa, kesi hizo ziko katika mchakato wa kufanya majadiliano ya kuzimaliza na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa baadhi ya washitakiwa.

Ilidaiwa kuwa baadhi ya washitakiwa wamekubaliana na DPP na kulipa, lakini taratibu hazijakamilika kutokana sababu mbalimbali ingawa pande zote mbili katika kesi hizo zilipewa siku 30 kukamilisha majadiliano hayo.

"Haya mambo yako kikanuni na lazima kanuni zifuatwe na kutekelezwa, tukiendekeza haya masuala ya kuongeza muda tutakuwa hatufiki mwisho, tuwe ‘serious’ (makini), tuzitendekee haki kanuni, ikiwezekana wadau wote wanaopaswa kushiriki mchakato huu wapewe elimu na waelewe kwamba kuna ukomo wa muda katika kanuni hizi," alisema Hakimu Isaya.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai shauri hilo lilipelekwa mahakamani kwa ajili ya kutajwa na alitaka kupata maelezo kutoka upande wa utetezi kuhusu hatua iliyofikiwa katika machakato wa majadiliano na DPP. 

Ukijibu hoja hizo, upande wa utetezi katika kesi hizo kupitia mawakili wa utetezi Daniel Mugabe na Denis Mwesiga, ulidai bado mchakato wa majadiliano haujakamilika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kushindwa kumpata DPP ofisini na mwingiliano wa ratiba za sikukuu, hivyo wakaomba muda zaidi.

Wakili Mugabe alidai mahakamani kuwa, alifanya juhudi za kukutana na DPP lakini aliambiwa anapaswa kukutana na Kamishana wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kukamilisha mchakato wa makubaliano.

"Kwa upande wetu, kesi yetu ina pande mbili ambao ni wa DPP na TRA, kwa upande wa DPP tulishaongea naye akasema tuonane na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato tukiwa kwenye mchakato, tunaona kuna mabadiliko yamefanyika hivyo tunaomba muda tuweze kukamilisha," alisema Mugabe. 

Katika kesi Namba 8, ilielezwa kuwa washitakiwa wawili walikuwa wamekubaliana na DPP na walishalipa, lakini kutokana na ratiba za kikazi za DPP, ílishindikana kufikisha taarifa kwa Mahakama ili iendelee na hatua nyingine.

Awali kwa nyakati tofauti, Hakimu Isaya alitoa siku 30 kwa pande zote katika kesi hizo kukamilisha taratibu za majadiliano na DPP na watakaporejea mahakama iweze kuendelea na hatua nyingine za mashauri hayo. 

Katika kesi Namba 8, Mallya na wenzake Happy Mwamugunda, Prochesi Shayo, Geofrey Urio, mhasibu Tunsubilege Mateni na mkaguzi wa hesabu, Nelson Kahangwa wanakabiliwana mashitaka 23 likiwemo la kukwepa kodi, kuisababishia serikali hasara zaidi ya Sh bilioni 31.48 na kutakatisha fedha hizo.

Kwa upande wa Rwegasira na wenzake, Mtemi Masanja na raia wa Ufaransa Thierry Lefeuvre na Malanie Phillippe wanakabiliwa na mashitaka 46 likiwemo la kuongoza genge la uhalifu, kushindwa kulipa kodi, kukwepa kodi, kughushi nyaraka na kutakatisha fedha na kusababisha hasara Sh bilioni 1.6 kwa TRA.

 

foto
Mwandishi: Anna Mwikola

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi