loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Madhehebu yamwombea Samia aiongoze vema Watanzania

UMOJA wa Madhehebu ya Kikristo Mkoani Tabora umefanya ibada ya pamoja kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ili Mungu amwepushie mabaya yoyote na kumwongoza kuwaletea maendeleo Watanzania.

Akizungumza katika ibada hiyo iliyofanyikia juzi katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Magharibi Kati, mjini Tabora, Askofu Elias Mbagata alisema wamekutana ili kumwomba Mungu ampe mafanikio makubwa Samia katika utawala wake.

Alisema Mungu alijua kuwa Samia atakuwa Rais, hivyo kama Kanisa wanapaswa kumwombea ili mapenzi ya Mungu kwa Watanzania yatimie.

Askofu Mbagata ambaye pia ni Katibu wa Umoja huo, alisema kupitia maombi hayo, Mungu atalinusuru taifa dhidi ya roho zozote za uharibifu, machafuko na rushwa.

Mwenyekiti wa Umoja huo, Askofu Isaack Laizer, alisema wamemwomba Rais Samia na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ili wawasaidie kuyasimamia na kuyaenzi kwa vitendo mema yote yaliyoanzishwa na hayati Dk John Magufuli.

Laizer ambaye ni Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Magharibi Kati, alisisitiza kuwa, vilio na simanzi vilivyooneshwa na wananchi wakati wa msiba huo vilidhihirisha jinsi jamii ilivyompenda kiongozi huyo kutokana na mambo mazuri aliyolifanyia taifa ikiwemo kutetea wanyonge.

Naye Askofu Mstaafu wa Kanisa la TAG-Kitete, Paul Meivukie, alisema Watanzania wanahitaji umoja wa kweli utakaoliwezesha taifa kuendelea kudumisha amani na mshikamano huku ili kuchochea maendeleo ya wananchi.

“Taifa linahitaji amani na mshikamano wa kweli, ndio maana tumeungana ili kumwombea rais na taifa kwa jumla ili Mungu atuepushe na migawanyiko ya aina yoyote,” alisema Askofu Meivukie.

Mwakilishi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Tabora, Padri Faustine Rwechungura alisema maombi hayo ni faraja kubwa kwa hayati Rais Magufuli kule aliko kwa sababu alimtanguliza Mungu katika kila jambo katika maisha yake.

Akizungumza katika ibada hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Philemon Sengati, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Abel Busalama, aliwapongeza viongozi wa dini kwa kuungana na kumwombea Rais Samia na wasaidizi wake wote.

Busalama alisisitiza kuwa, serikali inathamini mchango wa madhehebu ya dini katika kudumisha amani, upendo na mshikamano na akawataka kuendelea na utaratibu huo ili kuharakisha maendeleo ya nchi.

foto
Mwandishi: Lucas Raphael, Tabora

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi