loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

18,900 wakimbilia polisi ukatili wa kijinsia

JESHI la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam limesema zaidi ya wakazi 18,900 jijini humo wamefika katika huduma zinazotembea za mkono kwa mkono maarufu ‘One Stop Center Mobile’ kupata msaada kutokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo Lazaro Mambosasa, alisema wananchi hao wakiwemo wanaume wanatoka katika kata 16 katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala.

Aliyasema hayo wakati akifunga awamu ya pili ya huduma za mkono kwa mkono zinazotembea kwa waathirika wa unyanyasaji na ukatili wa kijinsia zilizotolewa katika kata tisa za Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Machi 15 hadi Aprili 1, mwaka huu.

“Katika awamu hii ya pili, tumewafikia watu 11,709  wanaume wakiwa 5,312 na wanawake 6,397 ukilinganisha na kipindi kilichopira (awamu ya kwanza Desemba 2020), tulipowafikia watu 7,200 wanaume wakiwa 3,251 na wanawake 3,949 waliojitokeza kwenye huduma na wengine tukawafuata mitaani kwao,” alisema Kamanda Mambosasa.

Takwimu zinaonesha katika awamu zote, wanaume 8,563 sawa na asilimia 45.28 walijitokeza katika vituo hivyo wengine wakidai kufanyiwa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na wake zao. Wanawake walikuwa 10,346 sawa na asilimia 54.72.

Mambosasa aliwataka hata wanaume wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika familia zao, wajitokeze na kudai haki zao mbele ya sheria, badala ya kuendelea kukaa kimya kwa kuona aibu huku wanazidi kuteseka.

Aliipongeza taasisi ya Fredrich Naumann Foundation for Freedom East Africa kwa kushirikiana na Polisi kufanikisha huduma za mkono kwa mkono zinazotembea.

Mkurugenzi wa Programu wa Naumann Foundation for Freedom East Africa (Tanzania na Kenya), Veni Swai, alilipongeza Jeshi la Polisi nchini kwa kuimarisha uhusiano na wananchi hali inayowafanya kujitokeza kueleza kero zao zikiwamo za vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia vinavyotokea katika familia na jamii.

Veni alisema hayo akilifafanulia HabariLEO kuhusu ushirikiano wa taasisi yake na Jeshi la Polisi unaowezesha wananchi kutoa taarifa mbalimbali kuhusu uhalifu na wahalifu pamoja na vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia vinavyofanywa dhidi ya watoto, wanawake na wanaume.

Kwa mujibu wa Mwanzilishi na Mratibu wa Huduma za Mkono kwa Mkono katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Dk Christina Onyango,

wanaume waliojitokeza kulalamika walisema wake zao wanawafanyia unyanyasaji na ukatili ukiwemo wa kupigwa, kutohudumiwa kwa mahitaji kama chakula na kunyimwa unyumba.

Dk Onyango alisema taarifa kutoka kwa baadhi ya wananchi zilibainisha hata wanaume wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kikatili eneo hilo, lakini wamekuwa na soni kujitokeza na kutoa taarifa kwa vyombo husika.

Kwa mujibu wa takwimu, katika awamu ya pili, miongoni mwa watu 11,709 waliofikiwa na huduma wakiwemo watoto 120, watu 3,487 walipatiwa huduma za kisheria.

Takwimu zinaonesha kuwa, watu 3,005 walipata huduma za kipolisi, watu 2,800 walipatiwa huduma za ustawi wa jamii na watu 2,417 walipatiwa huduma za afya zikiwano za upimaji wa macho, kisukari na shinikizo la damu maarufu BP.

Akizungumza katika uzinduzi wa awamu ya pili, maeneo ya Pugu Mnadani, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Janeth Magomi, alisema haki na usawa wa kijinsia unawahusu wabawake na wanaume.

“Ingawa ni maadhimisho ya kumtambua nafasi ya mwanamke katika maendeleo na ustawi wa jamii, hatuwaachi nyuma wala kuwabagua wanaume, bali tunahakikisha wote kuanzia watoto, wanawake na wanaume wana amani na hakuna anayefanyiwa unyanyasaji wala ukatili wa kijinsia.”

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi