loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Rais Samia amiminiwa pongezi Mwanza

WANANCHI jijini Mwanza wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa dhamira ya kuondoa kero zilizokuwa zimeibuka na hivyo kusababisha usumbufu katika nyanja za kibiashara na kijamii.

Wameeleza kuvutiwa na azma ya serikali kujenga uhusiano mzuri na wafanyabishara na wawekezaji kutoka nje ya nchi ili kuimarisha uchumi.

Walisema jana jijini Mwanza kuwa, uchumi wowote katika nchi hujengwa kupitia  katika sekta ya biashara ambayo inapata ushirikiano mzuri kutoka serikalini kutokana na kuwepo kwa mazingira rafiki baina ya pande mbili.

Mwalimu Fikiri Said aliyegombea ubunge katika kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Nyamagana, alielezea matumaini yake kwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan akisema ina dhamira imara ya kujenga uchumi imara wa viwanda na watu wake.

Alisema kujadiliana na wafanyabiashara na kusikiliza changamoto zao kutasaidia kuongeza makusanyo ya kodi kwani kupitia majadiliano ni chachu muhimu katika kuwezesha uvumbuzi wa vitu vipya vinavyoweza kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi.

Saidi alisema hatua ya Rais Samia kuvifungulia baadhi ya vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa, ni mwanzo mzuri wa ujenzi wa nchi kwa kuwa itasaidia watunga sera na serikali kufahamu zaidi wanachokitaka kuvifungulia baadhi ya vyombo vya habari kupitia vyombo vya habari.

"Wanahabari ni kiungo muhimu sana kati ya wananchi na serikali yao hivyo kufunguliwa kwa vyombo vya habari vilivyofungiwa kunaongeza wigo wa uhuru wa habari na hivyo, kutawezesha watawala na watawaliwa kuwa na wepesi wa ufanyaji kazi ulioridhiwa na pande zote," alisema Said.

Mwendesha bodaboda jijini Mwanza, Stanley Maliseli, alisema wamepokea kwa furaha tamko la Rais Samioa kuzitaka mamlaka zilizofungia baadhi ya vyombo vya habari kuvifungulia kuwa hatua hiyo itawawezesha wananchi kuwa na fursa kubwa ya kusikilizwa maoni yao.

Mkurugenzi wa Rasu Company ya jijini Mwanza, Sweed Omari, alisema walifurahishwa na tamko la Rais Samia kuzitaka mamlaka zinazotoa kazi kwa wakandarasi kuwalipa fedha kwa wakati.

Alisema hatua hiyo itawafanya kumaliza kazi wanazopata kwa wakati na hivyo kuepuka changamoto walizokuwa wakizipata na kusababisha kazi kutomalizika kwa wakati.

Mfanyabiashara wa vyuma chakavu ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alisema wanamshukuru Rais kwa kuona umuhimu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoza wananchi kodi kwa uhalisia na kufanya nao mazungumzo kuwezesha makubaliano yenye tija kwa pande zote.

 

foto
Mwandishi: Suleiman Shagata, Mwanza

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi