loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

11,280 wafundishwa ufugaji wa samaki

KITUO cha ukuzaji viumbe maji cha Kingolwira kilichopo Morogoro kimetoa mafunzo kwa wananchi 11,280 kutoka mikoa mbalimbali kuhusu ufugaji samaki kwa njia ya kisasa.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Imani Kapinga, alisema hayo kituoni hapo wakati akieleza  utekelezaji majukumu ya kituo tangu kilipoanzishwa.

Dk Kapinga alisema katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2020 ambacho wananchi hao walipata mafunzo,kituo hicho pia kilizalisha vifaranga (mbegu) vya sato 6,026,832 vilivyosambazwa katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Pwani, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya, Ruvuma, Rukwa, Dodoma , Singida , Tabora, Unguja, Mwanza na Arusha.

"Sehemu ya vifaranga (mbegu za samaki) vilivyozalishwa vilitumika kupandikiza kwenye malambo na mabwawa ya asili katika mikoa ya Morogoro, Pwani, Singida na Iringa," alisema.

Kapinga alisema wanavyuo 1,450 kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo cha Uvuvi Mbegani na Chuo cha Uvuvi Kunduchi kwa nyakati tofauti walipatiwa elimu kwa vitendo katika kituo hicho.

Alisema kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti ya Uvuvi (TAFIRI), SUA na UDSM, kituo hicho kimefanya tafiti zinazohusu ufugaji samaki.

Dk Kapinga alisema katika kutatua changamoto zinazokikabili kituo hicho, katika mwaka wa fedha 2020/2021, serikali ilitenga Sh milioni 262.3 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa jengo la ofisi, kitoleshi na kibanda cha walinzi.

Alisema ukarabati huo unatarajiwa kuboresha mazingira ya kazi, kuiongezea uzalishaji wa vifaranga (mbegu za samaki), na kuimarisha ulinzi wa kituo hicho.

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi