loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Tujitokeze wengi kuwapa  wanafunzi taulo za kike’  

ELIMU imekuwa ikitajwa kuwa ndio urithi muhumu zaidi kwa kizazi chochote kile na ndio maana imekuwa ikipewa kaulimbiu mbalimbali kama ‘elimu ni ufunguo wa maisha’, ‘elimu ni bahari’ elimu haina mwisho na kadhalika na kadhalika.

Ni kutokana na elimu, taifa linapata watalaamu mbalimbali na pia taifa linarithisha taaluma na tunu zake kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipata kusema kwamba ukitaka kumsaidia mtoto wa maskini, mpe elimu.

Baba wa Taifa alipotaja maadui watatu wanaolikabili taifa; umaskini, maradhi na ujinga imekuwa ikielezwa kwamba ukishapambana na ujinga (elimu) unakuwa umemsaidia mtu kupambana na maadui waliobaki; maradhi na umaskini.

Ni kwa kutambua umuhimu wa alimu, serikali ya awamu ya tano iliamua kutoa elimu bure, ili kuhakikisha ada na michango haziwi sababu za watoto wa kitanzania kukosa elimumsingi.

Wakati serikali ikihaha kuhakikisha watoto wa Tanzania wanapata elimu, watoto wengi wa kike waliopevuka wamekuwa wakabiliwa na changamoto ya kimaumbile pale wanapokuwa na ada za kila mwezi. 

Wakati mwingine hupata taabu kutokana na uhaba wa vyumba maalumu au vyoo kwa ajili ya usafi, kukosa waalimu wa kusimamia faragha zao lakini kubwa ambalo makala haya yanaliangalia ni kukosa taulo za kike ili kujisetiri wanapofikwa na hedhi.

Changamoto hiyo inaelezwa kuwakumba zaidi watoto wa kike wa maeneo ya vijijini kulinganisha na wenzao wa mijini ambapo inaelezwa kwamba wengine hulazimika kukaa nyumbani wanapoingia katika siku za hedhi kutokana na kukosa taulo za kujesitiri shuleni na hivyo kukosa masomo. 

Hali hiyo inaelezwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kushusha ufaulu wa watoto wa kike kwani mtoto ambaye kila mwezi anakosa masomo kwa siku nne au zaidi, hawezi kulingana na mwenzake wa kiume ambaye hana siku anayokosa shule.

Wakati mashule kwa kawaida huwa hayana taulo hizo za kike kwa ajili ya kuzigawa kwa wanafunzi, madukani huuzwa kati ya Sh 1,500 hadi  Sh 3,500 kwa pakiti moja, kiwango ambacho baadhi ya wazazi hawamudu kuwanunulia mabinti zao.

Kutokana na kukosekana au kutomudu kununua taulo hizo, baadhi ya wasichana inaelezwa kwamba wamekuwa wakitumia mbinu nyingine ambazo zinatajwa kwamba si salama sana kiafya abadani.

Kwa kutambua uwepo wa changamoto hiyo ambayo haiikumbi Tanzania pekee bali nchi nyingi za dunia ya tatu, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Agri Thamani, Neema Lugangira, hivi karibuni alitoa msaada wa taulo za kike kwa wanafunzi 1,800 kutoka Shule 16 za Sekondari za Manispaa ya Bukoba.

Neema ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu kuputia Chama Cha Mapimduzi (CCM) akitokea kwenye kundi la Asasi za Kiraia (NGOs) anasema kila mwanafunzi mw ahao 1,800 amepatiwa ‘neema’ ya taulo ambazo ataweza kuzitumia angalau kwa mwaka mmoja.

Ugawaji huo wa neema hizo kwa wanafunzi ulifanyika hivi karibuni kwenye uwanja wa Kaitaba Mjini Bukoba, ambapo pakiti 25,200 za taulo hizo za kike ziligawanywa kwa wanafunzi 1,800 kutoka shule hizo zilizopo katika kata zote 14 za Manispaa hiyo.

Shughuli hiyo ambayo imekuwa ahueni kubwa kwa watoto hao wa kike iliratibiwa na Idara ya Elimu ya Sekondari katika Manispaa ya Bukoba kwa kushirikiana na Afisa Elimu Taaluma Sekondari.

Neema anasema ameamua kutoa msaada huo ili kuwasaidia wanafunzi wa kike kujihifadhi na kuendelea na masomo yao wakati wa kipindi cha hedhi.

Neema anasema wanafunzi walionufaika na msaada huo ni wa kidato cha tatu na kidato cha nne, ambao wengi wao, kutokana na mazingira wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kushindwa kuhudhuria masomo wanapokuwa katika hedhi.

“Tunaamini msaada huu utakuwa na manufaa makubwa kwao na kuwawezesha kutumia muda mwingi kusoma hata wakiwa katika hedhi, tofauti na ilivyokuwa awali,” anasema.

Mbunge huyo anasema walianza kutoa taulo hizo za kike Mkoa wa Dodoma mwisho wa mwaka jana, kisha wakaenda mikoa ya Tabora na Tanga.

“Kwa upande wa Kagera, tumeanzia Bukoba sababu ndiyo makao makuu ya Agri Thamani tangu mwaka 2018 na ndio wilaya ambayo tumekuwa tukitoa elimu ya lishe bora shuleni,” anasema na kuongeza:

“Idara ya Elimu Sekondari Bukoba Manispaa ndio waliochagua shule na vidato vya kupata huu msaada. Changamoto ya ukosefu wa taulo za kike ni kubwa sana na tunaposema huchangia watoto wengine kushindwa kwenda shule ni kweli kabisa. Jambo hili linaathiri ufaulu kwa watoto wa kike.

“Nikiwa kama mdau wa maendeleo, natumia fursa hii kuwasihi wadau wengine wa elimu waungane nasi katika jitihada zetu kuu mbili ambazo ni lishe shuleni na kuhakikisha upatikanaji wa taulo za kike kwa wanafunzi,” anaongeza.

Anasema mradi huo wa taulo za kike utawanufaisha wanafunzi wa kike katika mikoa ya Dodoma, Tabora, Pwani, Tanga, Kigoma, Mtwara na Kagera na kwamba mikoa inayofuata ni Ruvuma na Lindi.

Kwa mujibu wa Neema, hadi Mei mwaka huu wanafunzi wa kike 5,500 watakuwa wamenufaika na mradi huo ambapo kila mmoja atapata pakiti za taulo hizo za kutumia kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Ofisa Elimu Sekondari Manispaa ya Bukoba, Emanuel Ebeneza anashukuru kwa msaada huo wa taulo za kike kwa wasichana ambao anaamini utakuwa chachu ya kupunguza utoro shuleni.

Anasema kupitia msaada huo, wanafunzi wamekuwa pia wakifundishwa juu ya hedhi salama, elimu anayosema itawasaidia kuelewa zaidi namna ya kujihifadhi na kupunguza utoro shuleni.

“Elimu juu ya hedhi salama itawasaidia wanafunzi wa kike kujiandaa kisaikolojia wakiwa katika hedhi na kuwaondolea hofu. Wamepewa elimu ya lishe bora inayowasaidia waepukane na changamoto ya upungufu wa damu (anemia),”anasema.

Mmoja wa wanafunzi hao kutoka Shule ya Sekondari Hamugembe, Avitha Faustine, anashukuru kwa msaada huo na kusema umekuwa faraja kubwa kwao kwani utasaidia kupunguza changamoto hiyo ambayo inawakabili wanafunzi wengi wa kike.

Avitha ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu, anasema taulo hizo zitawapa jeuri ya kutokosa masomo kwani anakiri kwamba kuna wakati wanashindwa kuhudhuria masomo wakiwa katika hedhi.
“Kwa sasa tumezidi kupata ujasiri wa kuendelea na masomo kwani kabla ya kupata taulo hizi wengine walikuwa wakilazimika kurudi nyumbani pindi hedhi inapowakuta wakiwa shule, hivyo kukosa masomo,” anasema.

Mwanafunzi mwingine, Catherine Mwijage anakiri kwamba baadhi yao hawajawahi kabisa kuona taulo za kike na kwamba wamekuwa wakitumia njia mbalimbali za asili kujihifadhi kipindi cha hedhi ambazo siyo salama kiafya.

Mwanafunzi mwingine, Amina Bakari naye anakiri kukosa masomo mara kwa mara wakati wa hedhi na hivyo anashukuru kwa msaada huo na kutamani kuona wadau wengine wanajitokeza kuwasaidia ili neema hiyo isikome baada ya mwaka mmoja.

Maneno ya mwanafunzi huo yanaonesha umuhimu wa wadau wote wa elimu ikiwemo serikali kuona umuhimu wa kushughulikia tatizo la taulo za usafi kwa watoto wa kike na kuhakikisha linabaki historia katika mashule yetu sambamba na kihakikisha uwepo wa vyumba vya kujisitiri watoto wa kike wanapopata hedhi wakiwa shuleni.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi