loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

TaSUBa inavyodhihirisha sanaa ni maisha toshelevu

SANAA ni neno ambalo asili yake ni Kiarabu lenye maana ya ufundi anaotumia mwanadamu kuwasilisha fikra au mawazo yaliyo ndani ya akili yake kwa kutumia sauti, vitu vyenye maumbo au michoro.

Aidha, kamusi mbalimbali zinaeleza kuwa, sanaa ni uzuri unaojiibua katika umbo lililosanifiwa kufikisha ujumbe kwa hadhira iliyokusudiwa.

Kwa kutambua umuhimu wa sanaa, hapa nchini imekuwa ni sekta ya muhimu inayochangia pato la taifa kwa kutoa ajira hasa kwa vijana katika muziki, maigizo, michoro na filamu na kuburidisha jamii.

Miaka mingi sanaa imekuwa kama kiburudisho pekee lakini jicho la sasa kwa sekta hiyo linaiona kama urithi wa utajiri kwa vizazi na vizazi ikiwa itachukuliwa kama sekta muhimu na endelevu.

Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) imedhamiria kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu sanaa kwa kuweka sekta hiyo kama tegemeo la ajira hasa kwa kundi la vijana.

TaSUBa imeanza hatua za kuifanya sanaa kuwa urithi wa uchumi kwa kuwajengea uwezo wa kimafunzo na ujuzi wanaopita katika chuo hicho ili kuongeza thamani ya mazao yanayotokana na sekta hiyo kuwezesha kuuzwa ndani na nje ya nchi na kukuza uchumi wa mtu na Pato la Taifa (GDP).

Hatua ya taasisi hiyo inayotoa elimu ya kati kwa usimamizi wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) kama zilivyo hatua za baadhi ya vyuo vikuu nchini kikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), inaanza kubadili taswira ya sekta hiyo.

Mkuu wa TaSUBa, Dk Herbert Makoye, akizungumza na HabariLeo hivi karibuni, alisema taasisi hiyo imeanza utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025 na maagizo ya viongozi yakiwamo ya Rais John Magufuli aliyoyatoa Novemba 13 mwaka jana, alipozindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma.

Dk Makoye anasema mtazamo wa sanaa na utamaduni uliwekwa mbali na urithi wa kiuchumi lakini sasa taasisi hiyo imedhamiria kutengeneza ajira kupitia tasnia hiyo ili kukuza uchumi kwa vijana na wadau husika na kuongeza Pato la Taifa.

 

Anasema utekelezaji wake umewekwa katika utoaji wa mafunzo kama jukumu kuu la taasisi hiyo kupitia maelekezo ya Ilani ya CCM na maagizo ya viongozi akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan kufundisha kozi fupi kwa njia ya kuwafuata wahitaji walipo.

 

Juzi katika hotuba yake, Rais Samia aliitaka Wizara ya elimu kuangalia upya mfumo wetu wa elimu utakaomwezesha mwanafunzi kujiajiri na kutosahau mazingira yake.

Dk Makoye anasema mafunzo hayo ni ya mguu kwa mguu, kikundi kwa kikundi, yaliyolengwa kuwafuata watu walipo badala ya kusubiri waje katika taasisi hiyo kutafuta ujuzi.

Dk Makoye anasema sanaa na utamaduni ni maisha yaliobeba watu wengi hasa vijana katika kujipatia kipato, hivyo kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao yake ni kuvikwamua vizazi na vizazi katika wimbi la umasikini na hiyo ndio dhamira ya serikali kwa watu wake.

Anasema tayari wanashirikiana na wadau wengine ikiwamo Bodi ya Filamu Idara ya Ubunifu ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam ( UDSM), Idara ya Sanaa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na wadau wengine katika kutoa mafunzo kuwawezesha wahusika kuingia kikamilifu katika soko la ajira na kuongeza thamani ya bidhaa za sanaa.

Kwa mujibu wa Dk Makoye, mafunzo ya kwanza waliyatoa kwa vijana zaidi ya 100 katika Halmashauri ya Mji wa Geita kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 6 mwaka jana na mpango ni kuziendea halmashauri zote nchini kulingana na mahitaji yao.

“Sisi tunapokea mahitaji yao maeneo wanayoona wanahitaji mafunzo kwa hiyo kupitia vikundi vyao vinavyosimamiwa na halnashauri, tunawaendea kwa kushirikiana na wadau wengine na kuwapa mafunzo hayo,” anasema Dk Makoye.

Katika eneo la kozi zinazitolewa katika chuo hicho kilicho kituo cha umahiri wa taaluma ya sanaa na utamaduni Afrika Mashariki kwa vyuo vya kati, kinatarajia kuanza kutoa kozi mpya kulingana na mahitaji ya soko la ajira.

Kozi hizo ambazo bado zipo kwenye mchakato wa kupewa ithibati na Nacte ni tatu ambazo ni Muziki; Urithi wa Utamaduni na Utalii; na Uongozi wa Sanaa na Masoko. Anasema matamanio yao ni kozi hizo kuanza katika mwaka ujao wa masomo ikiwa Nacte itazipitisha.

“Tunazo kozi nyingine ambazo bado hatujazipeleka, tunasubiri kwanza hizi zilizo katika mchakato zikamilike kwanza. Kuna kozi kama ya Kiswahili, ya Ngoma za Kitanzania, Sanaa za Ufundi lakini bado hazijakamilika, zikikamilika tutazipeleka Nacte,” anasema Dk Makoye.

TaSUBa mbali na kozi hizo mpya na zinazotarajiwa baadae kuanza kufundishwa chuoni hapo, hivi sasa inatoa kozi za muda mfupi na mrefu kwa ngazi ya cheti na diploma katika sanaa na utamaduni.

Mapinduzi ya urithi wa uchumi kupitia sanaa yanayofanywa na taasisi hiyo ya serikali, yanajitokeza katika idadi ya uhadili katika mwaka huu wa masomo 2021/2022 ambapo wanafunzi 397 (karibu 400) wamejiunga idadi ambayo ni kubwa kuwahi kutokea tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1981.

“Kwanza kabisa napenda niishukuru Tamisemi kwa mara ya kwanza katika mwaka huu wa masomo tumepata wanafunzi moja kwa moja kutoka Tamisemi kutoka kidato cha nne. Hii imeongeza udahili kwa watu 651 kuomba kujiunga na walioweza kujiunga ni kama 400 hivi. Wengine wanaenda labda vyuo vingine au kukosa karo na mambo kama hayo,” anasema Dk Makoye.

Idadi hiyo kubwa ya wanafunzi bado wanataka iongezeke na inatimiza dhamira ya taasisi hiyo kuirithisha jamii sanaa inayolipa. Hitaji la kukarabati miundombinu nalo likajitokeza kwa kazi na sasa ukarabati wa majengo mbalimbali yakiwamo madarasa, unaendelea kupitia serikali na wafadhili wengine marafiki wa taasisi hiyo.

Wafadhili hao ni taasisi mbili za Ujerumani zisizo za kiserikali ambazo ni Bagamoyo Friendship Society na Music for Life ambazo kila moja ilikubali kuboresha jengo moja moja kuanzia Juni mpaka Septemba mwaka jana (2020) lakini kutokana na Covid-19 hawakufanya.

“Hawa Music for Life wametumia tawi lao lililopo hapa Arusha kuanza ukarabati huo hivi sasa hapa chuoni. Ukarabati unaendelea na hilo wanalokarabati ni darasa la muziki na wamesema wakikamilisha ukarabati wataleta na vyombo vya muziki. Tunaamini na wale wengine watakuja pia wakiona hawa wenzao wanafanya,” anaeleza Mkuu huyo wa TaSUBa.

Kwa mujibu wa Dk Makoye, ukarabati huo unahusisha pia stoo ya kutunza vifaa na ofisi ya walimu.

Hii ndio TaSUBa iliyozalisha zaidi ya asilimia 80 ya maofisa utamaduni nchini na wasanii na watalaamu wengine hii ikiwa ni sehemu ya mazao ya wahitimu zaidi ya 900 waliomaliza chuoni hapo tangu kianzishwe kikiwa na wanafunzi wasiozidi 24.

Hili ni kimbilio la vijana wengi zaidi ya kada nyingine. Ukimuona msanii akitumbuiza jukwaani, kuna wataalamu wa taa, wajenzi wa jukwaa, waliotengeneza muziki, wasimamizi, mameneja, madansa na wataalamu wa sauti ambao miongoni mwa hawa, wapo uzao wa TaSUBa.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa alipofanya ziara mwishoni mwa mwaka jana chuoni hapo, alisema sanaa ni maisha hivyo nia ya Serikali ni kuifanya taasisi hiyo kuzalisha watu wenye ujuzi na utaalamu mkubwa katika sekta hiyo na kuleta mapinduzi ndani na nje ya nchi.

Bashungwa alisema sanaa ni urithi wa kiuchumi unaoweza kutumiwa kizazi kimoja baada ya kingine hivyo ni wakati sasa wa kuongeza ujuzi kwa kupata mafunzo katika taasisi kama TaSUBa ili kuuza sekta hiyo nje ya nchi.  

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi