loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mikunde ilivyo na faida  kuanzia kilimo hadi lishe

MAZAO jamii ya mikunde yana faida kubwa mwilini na hustawi karibia kila eneo hapa nchini, hivyo kuna haja ya kuyatilia maanani zaidi kwa kuyalima na kuyala.

Mazao jamii ya mikunde hujumuisha maharage, mbaazi, kunde, choroko, dengu, njugumawe, soya, fiwi, ngwara na njengere.

Mratibu wa kitaifa wa Utafiti wa Mazao Jamii ya Mikunde ambaye pia ni Mtafiti Mgunduzi wa mbegu hizo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Ilonga wilayani Kilosa, Morogoro, Meshack Makenge anaeleza faida za mazao hayo kuwa ni pamoja na kuboresha usalama wa chakula.

Faida nyingine anasema ni kuongeza kipato cha kaya na taifa kwa kuwa soko la mazao hayo ni kubwa ndani na nje ya nchi.

“Zao la soya, kwa mfano, mbali na matumizi mengine, hutumika kukamua mafuta ya kula na vilevile hutumika kutengenezea maziwa. Mazao ya mikunde kwa miongo mingi yamekuwa yakitumika kama mali ghafi viwandani kwa kutengeneza vyakula vya mifugo na bidhaa nyingine,” anasema.

Mazao hayo pia anasema yana uwezo wa kipekee wa kurutubisha udongo kwa kupitia vijidudu vilivyopo kwenye mizizi ambavyo huchukua hewa ya nitrojeni iliyopo angani na kuibadilisha kupitia mchakato maalumu na kuwa mbolea ardhini.

“Mazao haya hutumika kupunguza mmomonyoko wa udongo, hutumika kama mazao funika kwa ajili ya kuhifadhi unyevunyevu ardhini na kuzuia uotaji na ukuaji wa magugu.

“Kwenye suala zima la mabadiliko ya tabianchi mikunde hutumika kama mazao yanayokabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwani mazao haya yana sifa ya kustahimili ukame.

“Kwenye mifumo ya kilimo hulimwa kwa kuchanganywa na mazao mengine, yaani kilimo mseto kama vile mbaazi na mahindi, mbaazi na mtama, kunde na mahindi, ufuta na choroko, mihogo na kunde, minazi na fiwi, migomba na kunde, mkonge na choroko, korosho na maharagwe,” anasema.

Kwa maelezo ya Mratibu huyo, Tanzania inashikilia nafasi ya 12 duniani kwa uzalishaji wa mazao jamii ya mikunde.

Pamoja na kushika nafasi hiyo ya 12 duniani, uzalishaji wake bado upo chini ambao ni chini ya tani 0.9 kwa hekta.

Hivyo anasema juhudi kubwa zinatakiwa kuchukuliwa kwa ajili ya kuongeza matumizi ya teknolojia mbalimbali zilizozalishwa na watafiti wa TARI hususani teknolojia ya mbegu kwa kuzihaulisha kwa kushirikiana na wataalamu wa ugani kwenye Halmashauri nchini, kuzisimamia na kuzitolea maelekezo stahiki.

“Ushirikiano wa wadau wote kwenye sekta ya kilimo, waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao jamii ya mikunde kama vile wazalishaji, wasindikaji, wafanya biashara, wasafirishaji nje ya nchi na walaji wote unatakiwa ili kuleta tija kwa wakulima wadogo wadogo nchini kwa lengo la kuwakomboa kiuchumi na kimaisha,” anasema.

Akizungumzia mbegu asilia na chavua huru, anasema kuwa teknolojia ya mbegu nchini kwa miaka mitano iliyopita imeendelea kukua na matumizi ya mbegu za ndani kwa mujibu wa takwimu za Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) hadi kufika mwaka 2018/19 zimefikia asilimia 81 na hivyo kupunguza uagizaji wa mbegu kutoka nje ya nchi. 

Makenge anasema TARI imeendelea na utafiti wa kugundua mbegu bora zikiwemo, chavua huru (OPV) na chotara.

“Kwa miongo mingi sasa mbegu zinazotumika kwenye mazao jamii ya mikunde ni mbegu asilia na chavua huru. Matumizi ya mbegu bora zilizofanyiwa utafiti zinasisitizwa zitumike kwa wingi kwa ajili ya kuleta tija na hivyo wadau wanatakiwa watoe kipaumbele na uzito mkubwa kwani ndipo uzalishaji wenye tija unapo anzia,” anasema.

Anasema taasisi hiyo ya kilimo kupitia kituo chake cha Ilonga kina jukumu la msingi la kitaifa kwa ajili ya kufanya utafiti na kuratibu ugunduzi wa teknolojia za mbegu bora za mikunde na mazao mengine, na kuboresha kanuni za kilimo bora cha mazao jamii ya mikunde nchini kote.

Makenge anasema TARI imepata mafanikio makubwa kwa kugundua aina mbalimbali za mbegu bora za mikunde ambazo ni OPV zenye uwezo mkubwa wa uzaaji hadi kufikia tani 3.5 kwa hekta, kustahimili visumbufu vya mazao na zinazokubalika katika soko la ndani na nje ya nchi.

Anaeleza hadi sasa mazao ya mikunde yaliyofanyiwa utafiti ni Mbaazi aina saba ambazo zinastawi vizuri ukanda wa Kaskazini, ushorobo wa kati na ushorobo wa Kusini mwa nchi ya Tanzania na ukanda wa chini.

Upande wa kunde, Makenge anasema zipo aina nane zenye sifa ya uzaaji mkubwa, kustahimili magugu chawi aina ya Alectra vogelii, kukomaa kwa muda mfupi (siku 55-75), na kwamba kuna kunde wima na zinazotambaa.

Anasema choroko zipo aina mbili zenye sifa ya mbegu nene, zinazozaa sana na zinakomaa kwa siku 60 tu na kwamba dengu zipo aina nne zinazozaa sana, zinastahimili ukame, hupandwa baada ya mvua kukatika na baada ya kuvuna mazao ya nafaka shambani.

Kuhusu soya, mratibu huyo anasema zipo aina nne na kwamba zina sifa ya kustawi kwenye maeneo ya ukanda wa juu wa mwinuko kutoka usawa wa bahari mita 1,200 hadi mita 2,000, pia zipo aina ambazo hustawi kwenye maeneo ya ukanda wa chini na wa kati, zinazaa sana na zinatoa mafuta mengi.

Njugu mawe anasema zipo aina sita na kwamba zina sifa ya kuzaa sana na kustahimili visumbufu vya mazao. Kwenye aina hizi sita za mikunde zilizofanyiwa utafiti Makenge anasema zina tija kubwa sana kwa kaya na taifa letu kwa ujumla.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk Geoffrey Mkamilo amekuwa akisema kwamba katika kufikia uchumi wa kati wa juu na Tanzania ya viwanda, tunapaswa kutumia teknolojia mbalimbali zinazotoa majibu chanya kwa ajili ya kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

Hivyo anahimiza Watanzania kuitegemea taasisi hiyo  inayojihusisha na usambazaji wa mbegu bora zilizofanyiwa kazi kisayansi katika kuwafikia wakulima na wadau wengine wa kilimo.

Tari ilianzishwa  kwa sheria ya bunge namba 10 ya mwaka 2016 ikiwa na jukumu la kutafiti, kusimamia pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia mbalimbali kwa wakulima na wadau wengine ikiwa ni pamoja na kuratibu shughuli zote za utafiti wa kilimo Tanzania Bara.

Dk. Mkamilo anasema taasisi hiyo ina Idara kuu tatu ambazo ni utafiti na ubunifu, usambazaji wa teknolojia na mahusiano pamoja na utawala na rasilimali watu, ambapo  Shughuli zote za utafiti zinafanywa na idara ya utafiti na ubunifu.

Kuna vituo 17 vya utafiti, kila kimoja kikiwa na jukumu la kitaifa la kufanya utafiti na maendeleo ya zao moja au zaidi ya zao moja. Kituo cha Ilonga kinafanya  utafiti wa mahindi, mazao jamii ya mikunde, mtama, uwele, ulezi na alizeti.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TARI, Dk. Yohana Budeba anaipongeza serikali kupitia wizara ya kilimo kwa kuanzisha taasisi hiyo ya kilimo, ili kutafuta majawabu na changamoto za wakulima nchini.

“TARI imefanya vizuri, imeandaa mbegu bora na teknolojia mbalimbali za kusaidia wakulima wafanye kilimo chenye tija,” anasema.

Mkurugenzi wa TARI, Kituo cha Ilonga Dk. Joel Meliyo anasema kituo hicho kina majukumu ya uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya mtama, uwele na ulezi kwa nchi nzima ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa mbegu bora za mikunde ambazo ni mbaazi, kunde, choroko, soya na den

Anasema taasisi hiyo imekuwa ikigundua na kuhimiza matumizi ya teknolojia mbali mbali za kilimo ili kuongeza tija, uhakika wa chakula na lishe.

Kwa maelezo yake , uhaulishaji wa teknolojia katika kituo hicho unafanywa kupitia mashamba darasa, maonyesho ya kilimo biashara, siku za wakulima, ziara za mafunzo kwa wadau pamoja na maonyesho ya nane nane.

Naye Mtaalamu wa Lishe ya Binadamu kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe, Dk. Esther Nkuba anasema vyakula  vinavyotokana na mikunde vinasaidia sana kujenga miili kutokana na virutubisho vya protini vinavyopatikana kwa wingi katika mimea ya mikunde.

“Vyakula hivi viliwe pamoja na makundi mengine ya vyakula kama vile nafaka, mizizi, ndizi, mboga n.k,” anasema.

Anasema mikunde ni chanzo cha protini kinachopatikana kwa urahisi zaidi ukilinganisha na nyama.

“Pia mikunde ni chanzo cha virutubishi vingi ikiwemo vitamini, madini, antioxidant na nyuzi lishe. Sio tu kwamba mikunde ina wanga lakini pia ina tindikali ya folic, kopa, madini chuma, na magnesiamu.

“Mimea jamii ya mikunde kama soya ni chanzo kizuri cha manganese, fosforasi, na pia chanzo kizuri cha madini chuma, tindikali ya mafuta ya omega-3, nyuzi lishe, vitamini B2, magnesiamu, vitamini K, kalsiamu na potasiamu,” anasema.

Kwa maelezo yake virutubishi hivyo ni muhimu sana kwa afya hivyo anashauri Watanzania kula mikunde zaidi kwani ni mbadala wa nyama kwa watu wasiokula nyama.

Katika kipindi hiki cha tishio la maradhi ya corona, mtaalamu huyo wa lishe anashauri Watanzania kula  mikunde ili kupata protini, vitamini na madini  ambayo ni muhimu sana katika kuongeza kinga mwilini.

Tafiti zinaonyesha kuwa watu wanaokula mikunde kwa wingi  wanapunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, kisukari, saratani ya utumbo mpana. Pia anasema wanapunguza uwezekano wa kuwa na kiriba tumbo.

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi