loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Zitto ashauri Bodi ya Bandari kuvunjwa

KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameishauri Serikali kufanya ukaguzi maalumu katika miradi mikubwa inayotekelezwa na Mamlaka ya Bandari (TPA) ili kupata uhalisia wa ubadhilifu katika mamlaka hiyo.

Zitto ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akichambua ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Alisema wakati ukaguzi huo maalum unafanyika ACT Wazalendo wanapendekeza kuwa Mamlaka za Uteuzi zivunje Bodi ya Bandari na kuiunda upya ili kuweza kuweka misingi ya uwajibikaji katika Shirika.

Kauli ya Zitto imekuja siku tatu tangu Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kuwasilisha ripoti kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.

Awali ripoti hiyo ya CAG iliwasilishwa kwa Rais Samia Suluhu, ambapo baada ya kupitia ripoti hiyo alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini TPA Mhandisi Deusdedit Kakoko ili kupisha uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha bandarini hapo.

Uamuzi huo wa Rais Samia ulifikiwa Jumapili ya  Machi 28, 2021 na Rais Samia mara baada ya kupokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Rais Samia alisema ripoti hiyo ameiyona na kuipitia na kubaini kuwa kuna ubadhirifu mkubwa uliofanywa bandarini, hivyo amewaomba Takukuru kwa kushirikiana na watu wengine kushirikiana katika kufanya uchunguzi wa kina. Tayari Mhandisi Kakoko  yupo mikononi mwa Takukuru kwa mahojiano.

Katika ripoti ya CAG aliyoiwasilisha Alhamis Aprili 8, mjini Dodoma ilibaini vitendo vya ubadhirifu katika Bandari ya Mwanza na Bandari ya Kigoma ambako katika Bandari ya Mwanza, Shilingi  bilioni 3.27 zilitolewa katika akaunti ya benki ya TPA iliyopo CRDB kupitia miamala 737. Vitabu vya fedha havikuonesha hati za malipo na pia matumizi ya fedha hizo hayakuoneshwa.

CAG alisema katika Bandari ya Kigoma, Shilingi milioni 655.90 zilitolewa kutoka benki kwa kutumia hundi 30 bila kuwa na hati za malipo kuthibitisha malipo yaliyofanywa, na hundi hazikusajiliwa kwenye daftari la udhibiti wa hundi, na vipande vitano vya hundi havijaonekana katika daftari la udhibiti wala katika taarifa za benki.

“Nyaraka kama vitabu vya hundi, hati za uhamishaji fedha na taarifa za bodi ya zabuni hazikutolewa kwa uchunguzi zaidi,” alieleza na kuongeza kuwa katika Bandari ya Kigoma, alibaini ukosefu wa ripoti za mapato za kila siku ili kuhakiki ripoti za mapato ya kila mwezi kwa kipindi cha miezi saba.

SERIKALI inakusudia kurejesha mfumo wa maendeleo ya sanaa ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi