loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mkumbo atoa maagizo 17 kukuza uchumi

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo ametoa maelekezo 17 kuimarisha sekta ya viwanda na biashara ili zichangie ukuaji uchumi na kutekeleza Mpango wa Taifa wa Tatu wa Maendeleo.

Pia amewaekeleza wataalamu wa wizara hiyo watoe ushauri na kufanya uamuzi kwa kuzingatia utafiti na ushahidi wa kisayansi.

Profesa Mkumbo alitoa maelekezo hayo alipokutana na menejimenti ya wizara hiyo na wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, ambapo alisisitiza haja ya kuimarisha na kuoanisha sera, mikakati na sheria kwa lengo la kufanya mapinduzi ya kiuchumi.

Alisema Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025 inalenga kuona Tanzania inatoka kwenye kundi la nchi masikini na kufikia uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2025 na kusisitiza kuwa ili kufikia dira hiyo wizara hiyo ina nafasi na mchango mkubwa.

“Uchambuzi wa maudhui ya Dira ya Maendeleo unaonesha wazi nafasi ya sekta ya viwanda na biashara katika kila eneo la matokeo tarajiwa.

Ndiyo kusema tutakuwa sehemu ya washangiliaji kama utekelezaji wa dira utakwenda kama ilivyopangwa na tutakuwa sekta kiongozi katika kuvuna aibu ikitokea tumeshindwa kufikia lengo,” alisema Profesa Mkumbo.

Alisema pia katika Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Tatu, malengo sita kati ya malengo mahsusi 12 yanahusu sekta ya viwanda na biashara na kati ya vipaumbele vitano vya mpango huo vitatu vinahusu wizara hiyo.

Profesa Mkumbo alisema hakusudii kutumia muda mwingi kutunga sera, sheria na mikakati na kuwa yeye analenga katika utekelezaji na kuona matokeo ya utekelezaji huo kwa kuchochea ukuaji wa haraka wa sekta ya viwanda na biashara.

Aliwataka wataalamu wa idara ya sera na mipango na ile ya sheria kusimamia uhuishaji wa nyaraka za kisera ili ziende na wakati na kuakisi maudhui ya mpango wa maendeleo na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Kuhusu viwanda, Profesa Mkumbo alitaka wataaamu waeleze bayana aina ya viwanda vinavyotakiwa kuendelezwa nchini, kuwa na kanzidata ya kisasa ya viwanda, na kupima maendeleo ya viwanda kwa kuzingatia uzalishaji na kiwango cha ajira.

Pia aliwataka waweke mkazo kukuza na kuchochea viwanda vidogo vinavyotumia teknolojia rahisi na ya kisasa na vilivyojikita vijijini na mijini na kuwatambua, kuwawezesha na kuwahudumia wawekezaji katika viwanda vikubwa na vyenye tija katika uchumi na kuhuisha mkakati wa viwanda nchini, ikiwamo dhana ya EPZ na SEZ.

Alisema pia wanapaswa kusimamia kwa karibu miradi ya kielelezo iliyopo katika Mpango wa Maendeleo wa Tatu wa Taifa ambayo ni mradi wa chuma wa Mchuchuma na Liganga, magadi soda wa Engaruka, ujenzi wa kiwanda cha Sukari-Mkulazi na kanda maalum za uchumi na maeneo maalum ya uwekezaji Profesa Mkumbo alisema pia kunatakiwa kuwa na uimarishaji wa utafiti na matumizi yake katika maendeleo ya viwanda, ikiwamo kuwa na ushirikiano wa karibu na taasisi za utafiti na elimu ya juu na kupanua na kuboresha mahusiano na ushirikiano na taasisi za sekta binafsi.

Kuhusu sekta ya biashara, Profesa Mkumbo alisisitiza suala la kujenga imani kwa wafanyabiashara kupitia uwazi na kutabirika kwa mwelekeo wa kisera wa serikali na mawasiliano chanya ya mara kwa mara.

“Tunataka tunapokutana na wafanyabiashara tufanye mazungumzo yenye tija ya kubadilisha mikakati ya kukuza biashara na masoko badala ya mikutano hiyo kutumika tu kama jukwaa la kusikiliza malalamiko ya wafanyabiashara,” alisema

Alisema pia kazi nyingine iliyopo ni kuendelea kuzipitia kanuni za mamlaka za udhibiti zinazoonekana kukwamisha biashara, kuchochea na kuhamasisha tabia ya kujali wateja miongoni mwa watendaji wa serikali wanaohudumia sekta mbalimbali za biashara.

Profesa Mkumbo alisema pia kunahitajika kuipitia tena Blue Print kwa lengo la kuona maeneo ambayo bado hayajatekelezwa na kusimamia utekelezaji wake kikamilifu na kwa haraka, kushirikiana na Tamisemi, kuchambua na kuchakata kwa umakini maoni ya wabunge na wadau wengine kuhusu haja ya kuwa na mfuko mmoja wa mtaji kwa ajili ya wajasiriamali na wafanya biashara wadogo.

Alisema pia kuratibu na kusimamia uanzishwaji wa sera ya maendeleo ya sekta binafsi, ikiwamo biashara ndogo zinahitaji upendeleo maalumu ili kukua na kuweka msisitizo wa pekee katika kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania ndani na nje ya nchi na kuratibu na kusimamia uanzishwaji wa maeneo maalum ya kibiashara hususan kwa maeneo ya mipakani.

“Pia, kuona namna ya kuimarisha eneo maalumu la kibiashara la Kariakoo ambalo kihistoria limekuwa likifanya vizuri na kuona namna ya kuliboresha zaidi,” alisema Profesa Mkumbo

SERIKALI inakusudia kurejesha mfumo wa maendeleo ya sanaa ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi