loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

  Mrusi na mwanzo wa safari za binadamu angani

KAMA mtu wa kwanza kabisa kwenda anga za mbali, mwanaanga wa Urusi Yuri Gagarin kutoka Muungano wa Sovieti ya zamani (USSR) aliizunguka dunia miaka 60 iliyopita.

Yuri Gagarin alikwenda anga za mbali kwa chombo maalumu cha kusafiria angani kilichoitwa Vostok mnamo Aprili 12, 1961. Safari yake iliashiria mwanzo wa mashindano ya kuwania kwenda kufanya uchunguzi katika anga kati ya nchi za Mashariki na Magharibi.

Hilo ni tukio la kihistoria lililoibua fursa za kuuchunguza mfumo wa anga kwa manufaa ya wanadamu wote na kutoa mchango mkubwa wa sayansi ya anga na teknolojia katika kufikia malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs).

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliifanya Aprili 12 kuwa Siku ya Kimataifa ya Binadamu Kwenda Angani mwaka 2011 ili kuadhimisha mwanzo wa binadamu kwenda angani na kusisitiza umuhimu wa mchango wa sayansi ya anga na teknolojia katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Katika ujumbe wa mwaka huu, Mkurugenzi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Anga, Simonetta Di Pippo anasema: “Miaka 60 iliyopita ukurasa mpya ulifunguliwa na kudhihirisha kwamba angani si mwisho wa kila kitu tena.”

Anasema kuwa wanaanga ni wajumbe wa ubinadamu katika anga za mbali, wamejawa na talanta, ujuzi na ushujaa na sasa wanavuka hata mipaka ya yale tunayoweza kufanikisha katika maendeleo ya ustaarabu.  

Siku ya kimataifa ya binadamu kwenda angani ilioadhimishwa Jumatatu hii imekuwa fursa muhimu ya kusherehekea mafanikio yetu kwa elimu ya anga, tukiikumbuka siku ambayo Yuri Gagarin alizunguka dunia na kuwa binadamu wa kwanza angani.

Tangu hapo mwanaanga huyo akawa amefungua ukurasa wa utafiti wa masuala ya anga kwa wanadamu wote. 

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipoitangaza Aprili 12 kama Siku ya Kimataifa ya safari ya binadamu angani lilikuwa na sababu ya kuuenzi mwanzo wa enzi ya wanadamu kwenda angani, ikithibitisha mchango muhimu wa sayansi ya anga na teknolojia katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu na kuongeza ustawi ya mataifa na watu.

Vilevile kuhakikisha utimizaji wa matamanio yao ya kudumisha matumizi ya anga za mbali kwa madhumuni ya amani.

Iwe ni moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, matumizi ya anga za mbali huchangia malengo kadhaa ya maendeleo endelevu (SDGs).  

Kwa mfano, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Mambo ya Anga za Nje (UNOOSA) inasema teknolojia za masuala ya anga zinaweza kusaidia kuongeza uzalishaji wa mazao na kufanya matumizi ya ardhi, maji, mbegu, mbolea na rasilimali zingine kuwa bora zaidi, na kusongesha utimizaji wa Lengo namba 2 la maendeleo la kutokomeza njaa. 

Ubunifu kama huo ndani ya ofisi hiyo inasema ni makadirio muhimu zaidi ambayo janga la virusi vya corona linaweza kuwasukuma watu milioni 132 zaidi kutumbukia katika njaa, na kuwaongeza katika idadi ya watu milioni 690 ulimwenguni ambao tayari hawana chakula cha kutosha. 

Ili kuonesha umuhimu wa mifumo ya chakula na kilimo duniani, na kuifanya kuwa yenye nguvu zaidi, iliyo jumuishi, inayofaa na endelevu, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) lilimemteua mwanaanga wa Shirika la Anga za Ulaya (ESA) Thomas Pesquet kuwa balozi wake mwema. 

Pesquet ambaye ni mchagizaji wa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi, alipigia debe athari za mabadiliko ya tabianchi na kutoa wito wa kutaka heshima zaidi kwa mazingira wakati wa siku zake 196 mfululizo kwenye bodi ya Kituo cha Anga cha Kimataifa (ISS) katika mwaka 2016 na 2017. 

Kituo hiki cha ISS ni setelaiti inayozunguka dunia katika umbali wa takriban kilomita 400 juu ya uso wa ardhi. Kilianzishwa kutokana na mapatano baina ya mamlaka za usafiri wa angani za NASA (Marekani), Roskomos (Urusi), ESA (Umoja wa Ulaya), Japani na Canada.

Bila setelaiti, teknolojia nyingi za kisasa tunazofurahia leo kutuletea taarifa mbalimbali za kitafiti zisingewezekana, ila kwa setelaiti ya kwanza bandia, Sputnik, iliyozinduliwa mnamo 1957.

Leo, kuna satelaiti bandia zipatazo 2,666 zinazozunguka dunia zikifanya majaribio mbalimbali ya kisayansi na kuleta taarifa kama ilivyo kwa kituo cha ISS, ambacho ni maabara kubwa ya anga na wanaanga wanaishi na kufanya kazi kwa mwaka mzima. 

Ni rahisi kuona setelaiti angani nyakati za usiku, na hauhitaji darubini au hadubini kufanya hivyo. Kiza kinapoingia baada tu ya jua kutua, nenda nje na uzime taa zote za nje kisha angalia angani.

Mbali na kuona nyota na mwezi huenda pia utaona “nyota” bandia, chombo kinachong’aa sana kama sayari. Na kama umewahi kuona nyota yoyote inayoangaza ikienda polepole angani nyakati za usiku basi hiyo si nyota bali setelaiti!

Setelaiti ni kitu cha asili au cha kibinadamu ambacho kinazunguka sayari. Kwa mujibu wa machapisho mengi, chombo hiki kikubwa kilichotengenezwa na watu kina ukubwa wa takriban sawa na viwanja viwili vya mpira, na sehemu kubwa ya kufanyia kazi na kuishi iliyo sawa na vyumba vya ndege mbili aina ya Boeing 747. Na kina uzito wa tani 520.

Kusudi kuu la kituo hiki cha ISS ni kuwa na maabara katika anga za mbali. Katika mazingira yasiyo na nguvu ya uvutano (gravity) ambayo yanatoa nafasi ya kufanya majaribio mengi katika fani za biolojia, fizikia, kemia, tiba na astronomia (elimu ya anga).

Maabara hii ya kudumu ya utafiti wa angani inabeba vifaa vinavyopima mnururisho wa mialimwengu (cosmic rays) au mabadiliko ya nuru ya jua.

Mwezi ndiyo satelaite pekee ya asili ya Dunia. Setelaiti bandia huzinduliwa katika mfumo wa obiti kutusaidia katika mambo mbalimbali ya kisayansi duniani, iwe kutambua majira na utabiri wa hali ya hewa, mawasiliano ya simu za umbali mrefu, au kusaidia mifumo yetu ya urambazaji. 

Tangu kukamilika kwa kituo cha ISS wanaanga wamekuwa wanaishi katika kituo hicho kikubwa kwa wakati wote. Baadhi yao wanaishi humo kwa muda wa miezi kadhaa.

Ndani ya kituo hiki kinachotumika kama mahali pa kuutazama ulimwengu wote, wafanyakazi wa kituo hicho cha ISS wanafanya majaribio mbalimbali ya kisayansi yaliyovumbuliwa na wanasayansi kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Kwa mfano, nguvu za uvutano zinapokuwa hafifu sana, mizizi ya mimea haipenyi chini na matawi hayakui kuelekea juu. Kwa hiyo wanasayansi wanafanya majaribio yatakayoonesha jinsi mimea inavyokua pasipo nguvu za uvutano.

Kwa kuongezea, fuwele za protini huzidi kuwa kubwa na huwa na ulinganifu sawa zaidi angani. Kwa hiyo, fuwele safi zaidi zaweza kutokezwa chini ya hali hizo. Habari hii inawasaidia watafiti kutafuta dawa za kukabiliana na protini mahususi zinazosababisha maradhi.

Katika mazingira yaliyo na nguvu za uvutano zilizo hafifu sana, huwenda ikawezekana kufanya vitu ambavyo haviwezi kufanywa duniani.

Katika mfumo wa sayari, tunaamini kuwa endapo uchunguzi wa anga za mbali utafanywa kwa kuzingatia mustakabali bora wa jamii zetu unaweza kusaidia kuunda dunia bora zaidi.

Binadamu kufika angani kumebadili mtazamo wetu kuhusu dunia, sayari yetu na sisi wenyewe.

Safari ya Gagarin kwenye anga za mbali inachukuliwa kama mafanikio ya dunia nzima na mafanikio ya wanadamu (badala ya mafanikio ya Soviet pekee), setelaiti zinazozunguka sayari ya dunia zinaleta faida katika kila kona ya dunia katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu, njia kamili ya kuunda uendelevu kwa wote.

Maendeleo ya sayansi ya anga tangu ziara ya kwanza ya Gagarin kwenye anga za mbali, dunia imepiga hatua kubwa kutoka kwenye ufuatiliaji wa ukataji miti na ramani ya miamba ya matumbawe hadi ufuatiliaji wa maeneo ya mabadiliko ya haki za binadamu, orodha ndefu ya mashirika ambayo yanaendelea kusaka suluhisho na maoni yanayoweza kusaidia kusawazisha ukuaji wa uchumi, ustawi wa jamii na usimamizi wa mazingira.

Dhamira ya kwanza ilikuwa kuzindua setelaiti ambazo zingepiga picha ya dunia nzima kila siku na kuongeza upatikanaji wa habari na zana za kuona mabadiliko ili kuchukua hatua.

0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

LINUS Robert wa kijiji cha Mabamba, wilayani Kibondo, ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi