loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tumuache JPM apumzike, Samia afanye kazi

MACHI 17, mwaka huu, Tanzania ilimpoteza Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Magufuli aliyefariki dunia katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena, Dar es Salaam kutokana na maradhi ya moyo.

Kutokana na kifo chake na kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliapishwa Machi 19, mwaka huu kushika wadhifa wa urais wa Tanzania kumalizia kipindi kilichobaki cha serikali iliyoingia madarakani Novemba mwaka jana.

Dk Magufuli aliyeingia madarakani Novemba 5, 2015 na kisha kushinda tena kiti cha Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, amefanya mambo mengi makubwa katika uongozi wake wa miaka mitano na miezi mitano, ambayo siyo tu ni ya kupigiwa mfano nchini, bali Afrika na duniani kwa ujumla.

Hakuna ubishi kuwa Dk Magufuli na serikali yake walitenda hayo baada ya kuaminiwa na Watanzania kupitia ilani za uchaguzi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) za mwaka 2015-2020 na 2020-2025, zilizowapa ushindi kutokana na mambo mengi waliyowaahidi ambayo waliyatekeleza kwa mafanikio makubwa katika ilani ya 2015-2020 na ushahidi upo, na walikuwa wameanza kutekeleza miaka mingine mitano ya Ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025.

Hivyo, kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anatokana na CCM, yeye na wenzake ndani ya serikali na hata wale wa chama hicho tawala, wataendeleza yote yaliyoasisiwa chini ya uongozi wa Dk Magufuli kama walivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 ambayo waliinadi kwa pamoja mwaka jana walipokuwa wanaomba tena ridhaa kuiongoza Tanzania.

Kwa msingi huo, hatuoni sababu za kuwapo kwa malumbano, tena mengine yakiwa ndani ya Bunge kuhusu kubeza yale yaliyofanywa na Dk Magufuli. Tunaona malumbano haya hayana tija na ingefaa kwa sasa wabunge na watu wengine, wakamuacha Dk Magufuli akapumzika kwa amani baada ya kazi alizowafanyia Watanzania.

Kwetu sisi huu ni wakati wa kuungana na Rais Samia katika kumsaidia kuchapa kazi ili yote yaliyoahidiwa katika ilani yatekelezwe kikamilifu na kuwaletea maendeleo Watanzania. Dk Magufuli amemaliza kazi yake, na sasa nchi iko chini ta Rais Samia, hivyo tumsaidie awaletee Watanzania maendeleo kupitia ilani ya CCM ya 2020-20225.

Tulitarajia wabunge ambao wengi ni wa CCM wajikite katika kuishauri serikali wakati huu wa Bunge la Bajeti ambalo linapitia bajeti mbalimbali za kisekta na hivyo mchango wao unahitajika sana wakati huo ili serikali iweka mipango mizuri ya kuhakikisha Watanzania wanaendelea kupiga hatua katika maisha yao.

Kama alivyosema wakati wa uhai wake, Dk Magufuli kuwa tutamkumbuka kwa mazuri, hakuna ubishi wa hilo. Tumuache apumzike tukikumbuka mazuri aliyowafanyia Watanzania, na sasa tumsaidie Rais Samia kutenda kazi zake kwa kumuunga mkono ili afanikishe yote yaliyomo katika ilani na yale atakayoyaanzisha wakati huu akiwa Ikulu.

 

 

LINUS Robert wa kijiji cha Mabamba, wilayani Kibondo, ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi