loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali yashusha rungu kampuni 163 za urasimishaji

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesitisha kampuni 163 binafsi kupatiwa kandarasi mpya za urasimishaji wa makazi nchini baada ya kutoridhishwa na kampuni hizo katika utekezelezaji wa kazi za urasimishaji.

Aidha, baadhi ya kampuni zimechukuliwa hatua kwa kupelekwa kwenye vyombo vya uchunguzi na nyingine kuchukuliwa hatua kupitia bodi za kitaaluma kutokana na kukusanya fedha nyingi za wananchi lakini zisizo na uwiano na kazi zilizotekelezwa.

Kutokana na uamuzi huo, halmashauri zote nchini zimeelekezwa kutokutoa kandarasi mpya kwa kampuni na badala yake kazi mpya zifanywe na halmashuri husika kwa kusaidiwa na Ofisi za Ardhi za Mkoa.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi wa wizara hiyo, Deogratias Kalimenze alisema sitisho hilo linahusisha kampuni zote zinazofanya kazi za urasimishaji katika halmashauri 134 kwa kuhusisha jumla ya mitaa 1,457 nchini kote.

Kalimenze alisema mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Morogoro na Pwani ndiyo inaongoza kwa kampuni nyingi kuathirika na hatua ya sitisho la kupatiwa kandarasi za urasimishaji kwa kuwa kampuni nyingi zinazofanya urasimishaji zimo kwenye mikoa hii.

Katika mahojiano hayo ambayo gazeti hili lilitaka kufahamu kuhusu utekelezaji wa agizo la Naibu Waziri Dk Angeline Mabula alilolitoa Januari 10, mwaka huu kuhusu kampuni husika, Kalimenze alisema usitishaji huo umefanyika kutoa fursa kwa changamoto zilizojitokeza kushughulikiwa ipasavyo na kazi zilizopo kukamilishwa.

Januari 10, mwaka huu, Dk Mabula aliagiza kampuni zote za urasimishaji ardhi ambazo zimeshindwa kazi na kushindwa kuhuisha mikataba yao zinyang’anywe kazi hiyo na kurejesha fedha za wananchi. 

Hatua zachukuliwa

Akizungumzia kampuni zilizowasilishwa kwenye vyombo vya uchunguzi, Kalimenze alizitaja kuwa ni Mosaic Co. Ltd, Independent Planners (T) Ltd, Makazi Consult Ltd, HUSEA Co. Ltd, Spatial Planning Vision (SPV) na GEOID Geomatics Enterprises ambazo zilikusanya kiasi kikubwa cha fedha kisichoendana na uwiano wa kazi iliyofanyika.

Kampuni zilizozuiwa kuingia mikataba mipya na Bodi ya Usajili wataalamu wa mipango miji ni Husea Co. Ltd, Erepo Development Estates Co. Ltd, Makazi Consult Ltd na Vissible Planners Co. Ltd.

“Hakuna kiasi cha fedha kilichorejeshwa kwa wananchi, bali ufuatiliaji uliofanyika na wizara umebaini kuwa kiwango kikubwa fedha zilizokusanywa na kamati za wananchi katika mitaa ya urasimishaji kimekwishalipwa kwa kampuni husika na kwa mujibu wa kampuni hizo kimetumika katika kazi za urasimishaji ambazo hata hivyo bado hazijakamilika,” alisema kaimu mkurugenzi huyo.

Alisema wameendelea kutoa msukumo mkubwa kwa kampuni zote za urasimishaji zikamilishe kazi zao kwa kuzingatia mikataba husika.

Idadi ya viwanja vinavyotambuliwa na kuidhinishwa vimeendelea kuongezeka, hadi sasa 1,638,062 vimerasimishwa nchini na upimaji umekamilika kwa viwanja 643,685.

Wizara imesema pia imeimarisha usimamizi na ufuatiliaji kwa kuchukua hatua za kiutawala kwa wote walioshindwa kuwajibika kikamilifu katika kusimamia kazi za urasimishaji katika maeneo yao.

Kila ofisi ya Ardhi ya Mkoa na Mamlaka ya Upangaji imeteua Mratibu wa Urasimishaji Makazi. Vile vile wizara imehuisha mwongozo uliopo kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji, usimamizi, tathimini na utoaji taarifa za utekelezaji wa kazi za urasimishaji nchini kama sehemu ya mkakati wa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.

Akizungumzia athari za baadhi ya kampuni kutokamilisha urasimishaji kwa wakati katika mitaa mbalimbali, Kalimenze alisema kumeathiri upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi na serikali ikiwamo wananchi kuchelewa kumilikishwa ardhi zao hivyo serikali kupoteza mapato hususani kodi ya pango la ardhi.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa makazi, makisio ya mapato ya viwanja 643,685 vilivyokamilika upimaji wake, kama kila kiwanja kingeweza kumilikishwa kwa gharama ya Sh 120,000, serikali ingekusanya Sh bilioni 77.24. 

Kalimenze alisema wanaendelea kutafuta namna bora ya kushirikisha sekta binafsi katika shughuli za urasimishaji kuendeleza juhudi za urasimishaji makazi yasiyopangwa nchini.

SERIKALI inakusudia kurejesha mfumo wa maendeleo ya sanaa ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi