loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mapori tengefu 12 yarejeshwa kwa wananchi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema katika mwaka huu wa fedha mapori tengefu 12 yenye ukubwa wa ekari 707,659.94 na misitu ya hifadhi saba yenye ukubwa wa ekari 46,715 imefutwa ili kuruhusu wananchi waendelee na shughuli zao za kiuchumi na kijamii.

Hatua hiyo ni katika juhudi za serikali kuondoa migogoro ya ardhi nchini ikienda sambamba na kutatuliwa kwa migogoro ya ardhi 23,783 kupitia Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya.

Majaliwa alisema hayo wakati akiwasilisha bungeni hotuba yake ya makadirio ya bajeti ya ofisi ya waziri mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka ujao wa fedha 2020/2021.

Alibainisha kuwa katika mwaka 2020/2021 serikali imesimamia mikakati mbalimbali yenye lengo la kuondoa migogoro ya ardhi na kuhakikisha uwepo wa mipango na matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya shughuli za uwekezaji, kiuchumi na kijamii.

“Kwa kuzingatia hatua ambazo serikali imezichukua, naelekeza viongozi wote wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya serikali na kuhakikisha kuwa hakuna migogoro mipya ya ardhi inayojitokeza katika maeneo yao,” aliagiza

Waziri Mkuu alisema kuimarika kwa uchumi na maendeleo ya watu kumechangia kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii ambazo zimeibua migogoro ya matumizi ya ardhi. Alisema Julai 10, 2020 serikali iliridhia vijiji 920 kati ya 975 vyenye migogoro kubaki katika maeneo ya mikoa na kuendelea na shughuli za kiuchumi na kijamii.

Vilevile, serikali imeridhia vijiji 19 kati ya 55 vilivyokuwa na migogoro na vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea na shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo yao.

Waziri Mkuu alieleza kuwa hadi kufikia Januari 2021 viwanja 95,329 vilitambuliwa, kupimwa na kumilikishwa kwa kutumia dhana shirikishi katika upangaji na upimaji wa ardhi na kuongeza kuwa hatua hiyo, ni utekelezaji wa programu ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini. Vilevile, ardhi yenye ukubwa wa ekari 224,885.40 imetengwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya uwekezaji ikiwemo ujenzi wa viwanda.

Alisema katika mwaka 2021/2022, serikali itatekeleza mipango na programu za upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi katika maeneo ya wananchi pamoja na miradi ya kimkakati ya kitaifa, uimarishaji wa muindombinu ya upimaji na ramani na uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ambayo kwa pamoja itapunguza migogoro ya ardhi nchini.

SERIKALI inakusudia kurejesha mfumo wa maendeleo ya sanaa ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi