loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Simba yala bilioni 2/-, kuivaa Kagera leo

KLABU ya soka ya Simba imeingia mkataba wa miaka miwili na kampuni ya Vunjabei kwa ajili ya utengenezaji na usambazaji wa jezi na vifaa vingine vya michezo vyenye nembo ya timu hiyo ambao unathamani ya Sh bilioni 2.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbra Gonzaez alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kampuni hiyo ya Kitanzania kushinda tenda hiyo na kuridhishwa na utendaji wake na kiwango cha fedha ilichoweka mezani.

“Nachukua nafasi hii kuitangaza kampuni ya Vinjabei kuwa ndio mshindi wa tenda ya kununua na kusambaza jezi za Simba kwa mkataba wa miaka miwili, mbali ya jezi pia watakuwa na uwezo wa kwenda mbali zaidi wakutengeneza skafu, kofia na vitu vingine vingi vyenye nembo ya klabu yetu kwa kipindi chote hicho kuanzia msimu ujao,” alisema Barbra.

Kwa upande wake, mmiliki wa kampuni hiyo, Fred Ngajiro aliushuruku uongozi wa Simba kwa imani kubwa waliyoionesha kwao na kuwapa tenda hiyo ambayo ni ya kwanza kwa ukubwa tangu kuanza kufanya kazi hiyo na kuahidi kuifanya kwa weledi mkubwa katika kipindi chote cha mkataba walioingia.

“Naupongeza uongozi wa Simba kwa imani yao kubwa kwetu Vunjabei, wakati tunaomba hii tenda hatukuwa na imani kama tungeweza kushinda sababu kulikuwa na kampuni kubwa zaidi yetu lakini uongozi wa Simba chini ya CEO Barbra wakatupa hii nafasi, niwaahidi hatutawaangusha tutahakikisha Simba inavaa jezi zenye ubora kuliko timu nyingine yeyote hapa nchini,” alisema Ngajiro.

Mtendaji huyo wa Vunjabei alisema biashara ya kuivalisha Simba ina maslahi kwa pande zote mbili endapo itasimamiwa vizuri timu hiyo inaweza kujiendesha bila kutegemea fedha za viingilio.

Alisema wamejipanga kuhakikisha jezi mpya za Simba zinapatikana kuanzia siku ya tamasha la Simba (Simba Day) na tayari wameandaa maduka makubwa katika mikoa 13 ambayo yatakuwa yakiuza jezi za timu hiyo lengo ni kutaka kila shabiki wa timu hiyo kuiunga timu yake mkono kwa kuvaa jezi mpya katika kila msimu mpya.

Vunjabei ndio waliokuwa wakiivalisha Lipuli iliyoshuka daraja msimu uliopita.

Mkataba huo ni mkubwa wa kwanza wa Simba kwenye jezi. Mkataba uliopita ulikuwa wa Sh milioni 100 na kampuni ya Romario.

Katika hatua nyingine, Simba leo itakuwa ugenini kwenye uwanja wa Kaiba Bukoba kucheza na Kagera Sugar mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mabingwa hao watetezi wako Kanda ya Ziwa ambapo mwishoni mwa wiki iliyopita walicheza na Mwadui ya Shinyanga na kushinda bao 1-0.

 Mechi ya leo inatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kwa vile Simba inahitaji ushindi ili kukwea kileleni mwa msimamo wa ligi na Kagera inahitaji ushindi ili kujiondoa kwenye hatari ya kushuka daraja.

Kagera Sugar iko chini ya kocha mpya, Francis Baraza aliyetoka Biashara United akichukua nafasi ya Mecky Maxime aliyefutwa kazi kutokana na kushindwa kufanya vizuri. Baraza atakutana na Simba kwa mara ya pili, mara ya kwanza alikutana nayo akiwa Biashara ambapo mzunguko kwa kwanza walifungwa bao 1-0.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeiagiza ...

foto
Mwandishi: Mohamed Akida

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi