loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Trafiki wageuza daladala vikoba

BAADHI ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Dar es Salaam wamegeuza daladala mtaja uliobatizwa jina la ‘vikoba vya trafiki’ kwa kuwatoza na kupokea rushwa ya kati ya Sh 2,000 na 5,000 jambo ambalo limetajwa kusababisha kero katika usafirishaji wa abiria.

Uchunguzi wa HabariLeo umebaini  jumla ya kati ya Sh 17,000 na Sh 30,000 hukusanywa kutoka kila daladala kwa siku kupitia ‘vizuizi’ vyenye wastani wa askari watatu kwa kila kimoja katika maeneo tofauti barabarani ambavyo kila mmoja husimamisha magari kwa zamu na kukabidhiwa fedha hizo.

Kutokana na vitendo hivyo vinavyotia doa jeshi, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Wilbrod Mutafungwa amesema anaunda timu ya uchunguzi itakayofuatilia nyendo za askari husika na wote watakaobainika watawajibishwa kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.

Trafiki wanavyopokea

Timu ya waandishi wa gazeti hili katika maeneo mbalimbali mkoani Dar es Salaam pamoja na baadhi ya maeneo ya Pwani, imebaini vitendo hivyo   vimekuwa vikifanyika bila kificho kati ya wafanyakazi hao wa daladala na askari kiasi cha abiria wanaokuwamo kwenye magari kufahamu kinachoendelea.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, madereva na makondakta wameomba serikali kuingilia kati kuwanusuru na rushwa hiyo waliyoibatiza ‘vikoba ya trafiki’ wakisema  hawawezi kuigomea kwa kuhofu kubambikiwa  makosa na kukomolewa kwa kuandikiwa faini ya Sh 30,000.

Katika Barabara ya Morogoro, gazeti hili limefuatilia  kuanzia kituo cha mabasi cha Kibaha mkoani Pwani hadi Mbezi ambako madereva na makondakta wamethibitisha  kutoa kati ya Sh 17,000 na 28,000 kulingana na vituo vya ‘makusanyo’ vilivyobatizwa ‘vijiwe vya elfu mbili mbili’.  

Kutoka Stendi ya Kibaha hadi Mbezi, vipo vituo vipatavyo vitano ambavyo kila daladala hutozwa  ama Sh 2,000 au Sh 3,000.  Askari wengine maarufu kama wa ‘Oysterbay’ wanatajwa kupokea Sh 5,000.

 “Katika stendi mpya ya Kibaha tunatoa Sh 5,000 na kwenye vituo vingine, tunatoa ama shilingi elfu mbili au elfu tatu,” alisema dereva wa daladala inayofanya safari kati ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo na Mbezi, wilayani Ubungo.

Vituo vingine   ambavyo  kila daladala hutozwa kati ya Sh 2000 na Sh 3000, ni Bwawani, Gogoni, Kwa Mangi, Luguruni na Kwa Yusufu vyote vya wilayani Ubungo, Dar es Salaam.  

Kwa daladala zinazofanya safari kati ya Mbezi Luis na Temeke kupitia Barabara ya Morogoro na Mandela, vituo vinavyosifika kukusanya fedha hizo ni Kibanda cha Zamani, Suka,Kimara Bucha, Ubungo Darajani na Mwananchi.

Katika barabara itokayo Tangibovu kwenda Goba, kituo cha kwanza ambacho  polisi kukaa ni Kayuni ikifuatia na Ulomi na kingine kikiwa kabla ya kilima cha kutokea kituo cha Uwanjani. Kingine ni Njiapanda Nne eneo la Lilian Kibo na Kwa Zulu mbele ya kituo cha Kanisa na kwenye mzunguko wa Mbezi.

Katika kituo cha Goba Mwembe Madole (senta), polisi wamekuwa wakiangalia usalama wa wanaovuka barabara na kuongoza magari kunapotokea msongamano wa magari kati ya Barabara ya Goba na inayotoka Makongo.

Barabara nyingine yenye vijiwe vya mavuno ya askari ya Sh Sh 2,000 au Sh 3,000 kwa kila daladala ni Kigamboni wilayani Temeke. Vituo husika ni Pius, Kwa Kipara, Nyumba ya Njano, Chuo, Kibada kwa Hamisi, Shangwe, Mji Mwema, Kijaruba, Big Ston, Gari Bovu na Malaika Beach.

Utozaji huo wa fedha unafanyika pia kwa daladala zinazotoka Toangoma kwenda Temeke katika vituo vya daladala vya Njia Panda ya Jeshi, Bakwata, Mbagala Rangi Tatu(3), Misheni Njiapanda ya kwenda Mtoni Kijichi, Mtoni Mtongani, Mtoni kwa Azizi Ali, Temeke Mwisho na kituo cha Big Bonn.

Kwa upande wa Barabara ya Temeke kwenda Tazara (Mandela), vituo maarufu kwa utozaji wa fedha kwa makondakta hufanyika  kwenye vituo vya Sokota hadi Magorofa ya Tazara.

Kwa Barabara ya Kivule-Kitunda, maeneo ambayo askari hao husimamisha daladala na kupokea fedha hizo ni Makaburini jirani na Daraja la Sirari.

Abiria katika maeneo mbalimbali walilalamikia rushwa hiyo wakisema inasababisha baadhi ya daladala kukatisha njia kwa kutofika katika baadhi ya maeneo wakilenga kupunguza idadi ya vituo vya kutoa fedha hizo.

“Daladala wanasema wamechoshwa na Vikoba ya trafiki ndiyo maana siku hizi magari ya Makumbusho hayaji Kibamba hususani wakati wa asubuhi. Mengi yanageuzia Mbezi” alisema mmoja wa abiria katika kituo cha daladala cha Kibamba Shule.

Askari wapeana zamu

HabariLeo leo limebaini kila kituo huwa na wastani wa askari watatu ambao hupeana zamu ya kusimamisha daladala na kupokea fedha hizo. “Anayekusimamisha ndiye unayempelekea mgao,” alisema kondakta wa daladala inayofanya kazi kati ya Kibamba na Mbezi.

 “Sasa fikiria, ukikuta wa elfu tatu mara tatu, wa elfu mbili mara nne na wa elfu tano mara mbili, ni kiasi gani cha pesa tunatoa? Mapato yote tunawafanyia askari,” alisema.

Suala lingine ambalo gazeti hili limebaini ni kwamba, vitendo hivyo vya kupokea fedha vinafanyika bila kificho kiasi cha kondakta au dereva kushirikisha abiria pale anaposimamishwa, akiwaambia kwamba anashuka kwenda kutoa mgawo na wakati mwingine kuomba chenji ya kwenda kuwapa askari.

Imekuwa kawaida kwenye barabara zote za Dar es Salaam kuona askari wa usalama barabarani wakisimamisha daladala kisha kondakta hushuka akiwa na risiti ya kieletroniki na Sh 2,000 na kumpatia.

Muda ambao matukio haya hushuhudiwa zaidi ni asubuhi kati ya saa moja na saa nne. Askari katika vituo hivyo,  mara nyingi husimamisha zaidi daladala kuliko magari binafsi.

Makondakta wabariki rushwa

Ingawa madereva na makondakta wanalia juu ya rushwa hiyo, baadhi yao wanaibariki kwa kile kinachodaiwa kuwa huwapunguzia kadhia ya kukamatwa na kulipishwa faini ya Sh 30,000 zinazoingia serikalini.

Kondakta aliyezungumza na gazeti hili katika Kituo cha Daladala cha Tabata Relini (Mwananchi) , alisema ni kawaida kutoa fedha kwa askari kila siku hususani asubuhi ili kupunguza kadhia ya kukamatwa na kulipishwa faini.

Wakati makondakta na madereva wakithibitisha kuwa ni nadra daladala kukwepa kutozwa  fedha hizo, kulingana na idadi ya daladala zinazotoa huduma mkoani Dar es Salaam, inakadiriwa mamilioni ya shilingi  hukusanywa kwa mwezi na kuingia mfukoni mwa askari.  

Kulingana na taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), mkoa wa Dar es Salaam una takribani daladala 600 zilizosajiliwa kutoa huduma katika njia mbalimbali. 

Taarifa ya Latra inaonesha njia ya Gongo la Mboto-Makumbusho ina  mabasi ya daladala 42, Mbagala-Kawe daladala 134, Mbagala-Mbezi Luis (21), Mbagala-Gongo la Mboto (17), Makumbusho-Mbezi Luis (114), Mbezi Luis-Temeke (208) na Kawe-Mbezi Luis daladala 89.

Wamiliki washangaa

Kwa upande wa wamiliki, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (DARCOBOA), Sabri Mabrouk alisema hawana taarifa juu ya makondakta wao kutoa Sh 2,000 kwa  baadhi ya askari.

"Hayo madai tunayasikia kwako na utaratibu ulivyo ni wajibu wa mmiliki kuhakikisha daladala lake ni zima na lina vibali vyote ili pindi polisi anapolisimamisha kukagua asikute kosa na anapokuta kosa ama anakuamuru kurekebisha au akupe notisi ya kulipa faini," alisema.

 

Kamanda aonya askari

Akizungumzia tuhuma hizo, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mutafungwa alisema zinalichafua jesho hilo. Alisema anaunda timu ya uchunguzi mkoani Dar es Salaam itakayofuatilia nyendo hizo na wote watakaobainika watawajibishwa kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.

 “Siwezi kukataa vitendo hivyo vinaweza kufanywa na baadhi ya askari wetu ambao si waaminifu, ambao wanafanya hayo kwa tamaa zao, ni jambo baya na linatia doa jeshi letu,tunachunguza na tutachukua hatua kali dhidi yao,”alisema Kamanda Mutafungwa.

Kamanda Mutafungwa alisema wanaotoa rushwa na wanaopokea, wote wana makosa. Alisisitiza kuwa ni ujinga na si sahihi kwa  kondakta na dereva kutoa fedha kwa askari .

 “Ni vitu vya ajabu, hao makondakta na dereva kukubali kutoa hizo fedha ni ujinga, wasikubali kwa sababu wanapowapa wanaendelea kulea tatizo. Wakatae na kama wataandikiwa makosa kwa sababu ya kukataa kutoa rushwa watoe taarifa kwangu,” alisema Kamanda Mutafungwa.

Kamanda Mutafungwa ameonya askari wanaofanya vitendo hivyo akiataka  kuacha mara moja . Amewataka viongozi wa mikoa ya kipolisi kukomesha vitendo hivyo na kuacha daladala zifanye kazi zao bila kubugudhiwa.

Alisema kama zina makosa ya barabarani, ziwajibishwe kwa mujibu wa sheria na si kuomba rushwa. “Naomba hili nalibeba, nitazungumza na watu wangu, ni tabia mbaya inachafua taswira ya jeshi letu, hao askari wenye njaa zao hizo tutawawajibisha na kama kuna wakubwa wao wanashirikiana nao tunawashughulikia,”alisema Kamanda Mutafungwa.

SERIKALI inakusudia kurejesha mfumo wa maendeleo ya sanaa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi