loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tiba ya TB imeboreshwa, ukisikia dalili katibiwe

UGONJWA wa Kifua Kikuu (TB) unatibika na ni vyema mgonjwa akiona tu dalili awahi hospitalini ili asiendelee kuambukiza watu anaokutana nao.

Lakini pia TB hutibika endapo mgonjwa atagundulika kuwa anao na kufuata maelekezo yote ya daktari anayopewa.

Maria John (siyo jina halisi) mkazi wa Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam, ni miongoni mwa waliougua ugonjwa huo lakini baada ya kufuata ushauri wa daktari amepona kabisa.

Anasema mwaka jana akiwa na miaka 25 aliugua TB na kwamba alianza kwa kukohoa huku akitokwa na jasho jingi wakati wa usiku. Baadaye uzito wake ukawa unapungua na ndipo akaamua kwenda kupima, akakutwa nao.

“Baada ya kukutwa na TB nilipewa elimu kuhusu ugonjwa huo kisha nilianzishiwa matibabu katika Hospitali ya Amana, ndani ya miezi miwili nikajisikia ninapona. Lakini nilitumia dozi miezi sita kama inavyotakiwa,” anasema.

Anasema anagundua kuwa wagonjwa wa TB baadhi yao wanakwepa dawa kutokana na kunyanyapaliwa na ndugu zao hivyo anakuwa kwenye msongo wa mawazo, mwisho wa siku hakumbuki kunywa dawa.

Naye Joseph Martini, Mkazi wa Kiwalani jijini Dar es Salaam anasema Novemba mwaka jana alikuwa akibanwa pumzi na kifua na ndipo akashauriwa kufanya vipimo na kukutwa na TB.

Anasema Desemba mwaka jana alianza dozi ambayo anaendelea nayo na mpaka sasa ana miezi mine, bado miwili na kama matokeo yatakuwa mazuri atakuwa amemaliza dozi hiyo.

Anashauri watu kufika na kupima afya zao pale miili yao itakapokuwa haijakaa sawa ili wapatiwe tiba stahiki.

Kwa upande wake, Mratibu Kifua Kikuu na Ukoma Wilaya ya Ki-TB Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Dk Linda Mutasa anasema ugonjwa huo umekuwepo muda mrefu na sasa watafiti wanaendelea kuboresha huduma hususan kwenye matibabu.

Dk Mutasa anasema mwanzoni wakati wa tiba ya ugonjwa huo wagonjwa walikuwa wakitumia vidonge vingi kwa wakati mmoja lakini sasa tiba imeboreshwa ambapo vidonge vinne vimechanganywa na kuwa kidonge kimoja.

Anasema kuboreshwa kwa tiba ya dawa kumesababisha wagonjwa wengi kujitokeza na kumeza dawa tofauti na zamani.

“Lakini pia muda wa kumeza dawa ulikuwa ni mrefu miezi nane lakini sasa ni miezi sita tu.

“Unakuta mgonjwa anapata pills chache za kumeza kwa mfano kidonge kimoja kwa sasa kina dawa nne ambazo hizo dawa nne zilikuwa zimegawanywa gawanywa hivyo umezaji wa dawa umekuwa mzuri.

“Tunawashukuru wana sayansi kwa kuendelea kuboresha hii hali na ikiwezekana labda huko mbele zinaweza zikapungua zaidi hasa kwenye kupungua kwa miezi ya matibabu kwa sababu kuna tafiti  zinaendelea, inaweza ikafikia hata matumizi ya dawa yakawa miezi minne badala ya miezi sita ya sasa,” anasema.

Anasema hata kifua kikuu sugu kinapona na kwamba kinachoangaliwa ni usugu wa dawa za kifua kikuu endapo hazifanyi kazi mgonjwa hubadilishiwa dawa.

Anasema wanashauri mtu atibiwe haraka kwani mgonjwa mmoja wa kifua kikuu ambaye hajaanza tiba ana uwezo wa kuambukiza watu 15 mpaka 20.

Maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu duniani hufanyika kila mwaka Machi 24 lakini mwaka huu kwa Tanzania yalipita kimya kimya kwani ni kipindi ambacho Tanzania ilikuwa ikiomboleza kifo cha Rais John Magufuli.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 duniani zenye idadi kubwa ya maambukizo ya Kifua Kikuu.

Lakini kidunia nchi ya India ndio inayoongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa ambayo ni takribani milioni mbili kwa mwaka kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2019.

 Mratibu wa Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Allan Tarimo anasema hapa nchini kwa mwaka 2019 ilikadiria kuwepo kwa wagonjwa wa kifua kikuu takribani 137,000, kati ya hao waliogundulika na kuwekwa kwenye matibabu ni 82,000.

“Hii ikiwa ni sawa na asilimia 53 tu. Hii ina maana hatukuweza kuwapata wagonjwa 55,000 ambao wameendelea kueneza ugonjwa huu katika jamii yetu,” anasema.

 Dk Tarimo anasema Mkoa wa Dar es Salaam umekuwa ukiongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa, takribani asilimia 20 ya wagonjwa wote nchini walipatikana Dar es Salaam.

 Lakini mikoa ya Kigoma, Songwe, Katavi na Zanzibar kwa ujumla imekuwa na idadi ndogo ya wagonjwa.

 Anasema serikali imeweka mikakati madhubuti ya kupambana na ugonjwa huo nchini ikiwa ni pamoja na kuboresha na kuongeza wigo wa huduma za ugunduzi wa TB kwa kutumia teknolojia mpya ya vinasaba ya Gene-Xpert.

Pia wizara imeongeza mashine za GeneXpert zinazopima TB kutoka mashine 65 mwaka 2015 hadi kufikia 259 mwaka 2020.

 “Mikakati mingine ni kuhakikisha dawa na vitendanishi vyote kwa ajili ya huduma za kifua kikuu nchini vinapatikana kwa wakati pasipo kukosekana,” anasema.

Vilevile anasema wizara itaendeleza mkakati wa kushirikisha sekta binafsi vikiwemo vituo binafsi vya afya na maduka ya dawa katika kuibua wagonjwa wa TB kutoka vituo 560 vya sasa hadi kufikia 1400 ifikapo 2025.

Anasema mkakati mwingine ni ushirikishwaji wa jamii katika kudhibiti Kifua Kikuu na kwamba wizara pia imeendelea kutekeleza  kampeni za uhamasishaji na upimaji wa TB na VVU kwa wananchi katika makazi duni yenye msongamano au sehemu za kazi zenye mazingira hatarishi kama vile maeneo ya migodi, magerezani  na makazi duni, miji mikubwa na shule za bweni.

Hatua nyingine inayofanyika anasema ni pamoja na kuwajengea uwezo waganga wa jadi ili watambue mapema na kuwapa rufaa wahisiwa wote wa TB wanaofika kwenye  maeneo yao.

Kwa mujibu wa Dk Tarimo ugonjwa wa Kifua Kikuu huathiri zaidi makundi ambayo kinga za mwili ni dhaifu kwa sababu mbalimbali.

Ni kwa muktadha huo anasema makundi yaliyo katika hatari ya kuugua TB ni watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi, watoto walio na umri chini ya miaka mitano, wenye utapiamlo pamoja na wachimbaji madini wadogo wadogo.

Wengine ni wajidungaji wa dawa za kulevya, wazee wenye umri zaidi ya miaka 60, wagonjwa wa kisukari na wenye magonjwa ya saratani.

 Kundi lingine anasema ni wafungwa na mahabusu na wale wanaoishi katika mabweni pamoja na watoa huduma za afya.

Halikadhalika, Dk Tarimo anasema TB ni ugonjwa sugu wa kuambukiza unaosababishwa na vimelea aina ya bakteria, ambavyo kitaalamu hujulikana kama “Mycobacterium tuberculosis”. Anasema mara nyingi huathiri sehemu zote za mwili na hasa mapafu.

 Anasema TB ni ugonjwa unaoenezwa kwa njia ya hewa na vimelea husambaa kwenye jamii kwa haraka sana kutokanana idadi kubwa ya watu wanaougua TB kutogunduliwa na kuwekwa kwenye matibabu mapema.

 Dalili za TB ni pamoja na kukoa kwa zaidi ya wiki mbili, homa za mara kwa mara, kupungua uzito, kutokwa na jasho jingi hasa wakati wa usiku na makohozi kuchanganyika na damu.

 Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Muda wa kufikia malengo ya kutokomeza TB ni 2022. Tuongeze kasi! Muda umekaribia”.

 Kaulimbiu hii inataka wananchi waongeze kasi na juhudi katika kufikia malengo kutokomeza ugonjwa huu nchini sanjari na malengo yaliyowekwa na Shirika la Afya Duniani na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

LINUS Robert wa kijiji cha Mabamba, wilayani Kibondo, ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi