loader
Dstv Habarileo Mobile
Picha

Methali hizi za Kiswahili hazijapitwa na wakati

WIKI iliyopita tulianza kujadili baadhi ya methali ambazo baadhi ya watumiaji wa Kiswahili wanadai zimepitwa na wakati katika mkala iliyokuwa na kuchwa cha habari “Mjadala kuhusu baadhi ya methali za Kiswahili kupitwa na wakati,” tukaeleza sababu wanazotoa ikiwemo maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Methali hizo kwa wasomaji ambao hawakufuatilia makala iliyopita ni Mwenzako akinyolewa, wewe tia maji, Barua ni nusu ya kuonana, Mchagua jembe si mkulima na Alalaye usimwamshe ukimwamsha utalala wewe.

Methali zingine tulizozitaja ni  Polepole ndio mwendo, haraka haraka haina baraka, Simba mwenda pole ndiye mla nyama, Subira huvyaa (huzaa) mwana mwema na Kawia ufike.

Methali zingine zinazonyooshewa kidole ni Ajali haina kinga au Ajali haikingiki,  Mvumilivu hula mbivu, Aliye juu mngoje chini, na Mpanda ngazi hushuka

Je, ni kweli methali hizo zimepitwa na wakati na hatuna sababu ya kuendelea nazo? Hili ndilo swali tunalojaribu kujibu leo.

Baada ya kujadili baadhi ya methali hizo makala haya yatajadili maana ya methali na umuhimu wake katika jamii. Kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili, Toleo la 2 iliyoandikwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), ukurasa wa 652-653,  maana ya methali ni ”usemi wa kimapokeo wenye kutoa kauli kimafumbo na kimuhtasari kama njia ya kusisitiza, kuelimisha au kuonya na kupongeza kwa njia ya busara”.

Methali zinabeba dhana ambazo zimeelezwa kwa kifupi; kwa kutumia maneno machache.

Methali kwa kawaida huwa na uteuzi wa maneno na hubeba maana mbili: maana ambayo inaweza kuonekana au kupatikana waziwazi kwa ama  kuisoma au kuisikia methali fulani katika hali yake ya kawaida bila ya kuhusisha tafakuri (maana ya nje) na maana ya pili ni ile ya ndani ambayo inampasa mtu kuzama kifikra ili aweze kupata maana iliyokusudiwa. 

Kwa sababu hii basi, ufafanuzi wa methali ambao mtu anautoa uhusishe mawanda mapana ya kifikra na utalii mpana wa mazingira ya jamii, kwa kufanya hivi baadhi ya upotoshaji uliojadiliwa hautakuwepo. 

Kwa mfano, methali Ajali haina kinga kupingwa kuwa ajali nyingi zinazotokea katika jamii yetu zinaweza kudhibitika! Kwa mujibu wa kamusi ya BAKITA iliyotajwa awali, ‘ajali’ ni ”tukio la ghafla lenye madhara, pia ajali ni tukio la kifo”. 

Ni ukweli usiopingika kuwa mwanadamu hana uwezo wa kuzuia kifo. Methali hii aghalabu inatumika wakati wa msiba ili kumfariji mfiwa kwa maneno haya kwamba, ‘binadamu hana uwezo wa kuzuia ajali (kifo) kwani ni mapenzi ya Mungu.’ Hivyo, ufafanuzi wa methali unatakiwa usiwe wa kijuujuu.

Methali nyingine ambazo maana yake inahitaji tafakuri ni Mwenzako akinyolewa, wewe tia maji. Lengo la methali hii ni kutoa wosia au tahadhari kwa mtu ambaye jamaa yake amekumbwa na madhila kuwa naye pia anapaswa kujitayarisha au kuchukua tahadhari ili asije kukumbwa na madhila hayo, na wala si unyoaji wa nywele hasa kama wengi wanavyotafsiri.

Methali ya Mchagua jembe si mkulima, maana yake halisi ya ndani ni kusisitiza juu ya kuwa tayari kutekeleza jukumu lako bila ya kuleta visingizio. Aidha, maana ya ndani ya methali Alalaye usimwamshe ukimwamsha utalala wewe, ni kutoa tahadhari kwa wanadamu kuepeuka kujiingiza katika ujinga fulani wa mtu au mambo ya mtu mwingine.

Methali Mvumilivu hula mbivu, Aliye juu mngoje chini au Mpanda ngazi hushuka, zinatufundisha kuwa na subira katika maisha na pia kutowadharau watu wengine kwa sababu ya mali na vyeo vyetu kwani iko siku hatutakuwa na mali na vyeo hivyo.

Muundo wa methali ni wa pande mbili: Tukio na Matokeo. Hii inamaanisha kuwa lazima kuwe na tukio ili ukamilifu wa methali uweze kutokea, yaani, kwa kuonyesha matokeo ya tukio linalohusika. Tazama mifano hii:

Tukio -      Matokeo

Mwenda tezi na omo       -        Marejeo ngamani

Mchovya asali           -        Hachovyi mara moja

Ganda la mua la jana       -         Chungu kaona kivuno

Bahari iliko                      -        Ndiko mito iendako

Ivumayo                           -        Haidumu 

Dudu liumalo                   -        Silipe kidole              

Tofauti na vipengele vingine vya fasihi simulizi, kama vile vitendawili, hadithi, ushairi n.k., methali zinatumika katika mazungumzo ya kawaida ya kila siku pale mzungumzaji anapotaka kusisitiza jambo fulani kwa mtu anayezungumza naye. Jambo hilo linaweza kuwa zuri na lenye nia njema au baya. Kutokana na sifa hii methali huteuliwa kulingana na mazingira ya wazungumzaji na ujumbe uliokusudiwa.

Kwa sababu methali hutegemea mazingira maalumu ndio maana baadhi ya methali huwa na maana zinazokinzana. Tazama methali za Fungu A na zile za Fungu B:

Fungu A

 • Haraka haraka haina baraka
 • Polepole ndio mwendo
 • Mwenda kasi mngojee achoke
 • Mwenye pupa hadiriki kula tamu
 • Daraja livuke ulifikiapo.

Fungu B

 • Ngojangoja huumiza matumbo
 • Chelewa chelewa utamkuta mwana si wako
 • Awali ni awali, hakuna awali mbovu
 • Hatua ndefu hufupisha mwendo
 • La leo litendwe leo.

Mifano ya namna hii iko mingi. Hapa tunasisitiza kwamba kuna umuhimu mkubwa wa kutumia methali kulingana na matukio, ndio maana kuna ukinzani katika baadhi ya methali. 

Katika methali zilizo katika mafungu hayo  hapo juu, kila mtumiaji atatumia methali za fungu mojawapo kulingana na tukio na jambo analotaka kulisisitiza. 

Pamoja na ukweli kuwa ili kufanikiwa katika baadhi ya mambo mtu anapaswa kuharakisha lakini wakati mwingine haraka ya mtu inaweza kusababisha ajali na maafa. Takwimu za chanzo cha ajali nyingi za barabarani hapa nchini zinaweza kuthibitisha jambo hili.

Methali hutalii mazingira ya jamii na kuelezea shughuli za wanajamii, jambo ambalo huwafanya watu kujua utamaduni wa jamii fulani, hali ya kimaumbile ya eneo linalohusika, shughuli za kiuchumi, mavazi, vyakula, itikadi na kiwango cha maendeleo ya jamii inayohusika. 

Hivyo, hata kama baadhi ya dhana na zana hazitumiki leo hii; japo hatuna uhakika sana na hili, ujumbe uliobebwa katika methali utabaki kuwa kumbukumbu ya maisha ya jamii na kuakisi maisha yao kwa ujumla. 

Historia ya jamii inapatikana kupitia katika methali. Leo hii wakulima wakiacha kabisa matumizi ya jembe la mkono au Watanzania wakiacha kabisa kuandikiana barua bado methali: Mchagua jembe si mkulima na Barua ni nusu ya kuonana zitaendelea kuhifadhi historia muhimu ya maisha ya Watanzania, historia ambayo itarithishwa kwa vizazi vijavyo. 

Kuhitimisha, tunasema kwamba methali ni kipengele muhimu sana katika maisha ya mwanadamu kutokana na dhima mbalimbali ambazo zinabebwa na methali. Aidha, madai kwamba baadhi ya methali zimepitwa na wakati hayana mashiko kwani hayana ithibati. 

Ushauri tunaotoa ni kuwa ufafanuzi wa methali uhusishe tafakuri ya maana ya nje na maana ya ndani. Vilevile, tunafafanua kuwa methali huteuliwa kulingana na mazingira na tukio ambalo mtu anakabiliana nalo, ndio maana baadhi ya methali zina maana inayokinzana. Pia, tunamalizia kwa kusema kuwa methali zimehifadhi historia ya jamii zinamotumika.

 

Tujivunie Kiswahili!

R. P. Mtambi, Mhariri Mkuu, BAKITA simu 0765 - 616 421 

LINUS Robert wa kijiji cha Mabamba, wilayani Kibondo, ...

foto
Mwandishi: R. P. Mtambi, Mhariri Mkuu, BAKITA

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi