loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Waziri Ndaki, afurahia Brela kupunguza urasimu

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, amefurahishwa na hatua iliyofikiwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) katika kupunguza urasimu.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya Biashara, Uwekezaji na Utalii katika viwanja vya Rock City Mall jijini hapa.

Alielezea kufurahishwa na hatua hiyo baada ya kupewa ufafanuzi na Ofisa Usajili kutoka Brela, Gabriel Girangay kuhusu jitihada zilizofanyika kumaliza tatizo hilo alipotembelea Banda la Maonesho la Brela.

Girangay alisema Brela imeboresha huduma inazotoa kwa wadau wake ikiwa ni pamoja na kupunguza muda wa kukamilisha usajili kwa kadri inavyowezekana, pia kuwahudumia wateja wote kwa ukaribu kupitia kituo cha miito.

“Kwa sasa muda wa usajili wa jina la biashara ni siku moja na si zaidi ya siku tatu za kazi, usajili wa kampuni ni siku tatu na si zaidi ya siku tano za kazi. Usajili wa alama za biashara na huduma ni kipindi cha siku 90 kutokana na takwa la kisheria,” alisema.

Akaongeza: “Maombi ya kupata ni siku 120 kutokana na takwa la kisheria, kupata leseni ya kiwanda au leseni ya biashara kundi A ni siku moja na si zaidi ya siku tatu za kazi.”

Girangay alisema Brela inashiriki maonesho haya ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kuwafikia wadau wake katika maeneo yao ili kuwapa elimu juu ya umuhimu wa kurasimisha biashara.

Katika ufunguzi wa maonesho hayo, Waziri Ndaki aliwataka wafanyabiashara na wajasiriamali wa Mkoa wa Mwaza kutumia fursa ya uwepo wa Brela katika maonesho haya kutatua changamoto zao na kupata elimu.

“Changamoto zinazosemekana zipo katika urasimishaji biashara sasa ndio muda wake kuzimaliza na bahati nzuri Brela wapo katika maonesho haya, fikeni katika banda lao la maonesho, pateni elimu, wasilisheni changamoto zenu hapo na rasimisheni biashara papo kwa hapo,” alisema.

Alisema wanaelimisha kuhusu taratibu za urasimishaji biashara na gharama zake, kutatua changamoto na kufanya usajili wa papo kwa hapo.

Maonesho hayo ya Biashara na Uwekezaji yaliyondaliwa na Rock City Mall na kufanyika kwa siku tatu, yalianza Aprili 30 na yalimalizika jana.

 

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amesema serikali imeweza ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Mwanza

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi