loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Samia ajadili uchumi na Obasanjo, bosi IMF

RAIS Samia Suluhu Hassan jana kwa nyakati tofauti amezungumza na Rais Mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Kristalina Georgieva.

Wamezungumzia kuhusu masuala ya maendeleo ya kiuchumi Afrika na ushirikiano kati Tanzania na IMF katika masuala ya kiuchumi.

Katika mazungumzo yake na Obasanjo, pia wamesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuongeza ushirikiano na kuondoa vikwazo vya biashara na uwekezaji.

Obasanjo ametumia mazungumzo hayo kutoa salamu za rambirambi kwa Rais Samia na Watanzania kutokana na kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli na Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilieleza kuwa mazungumzo hayo yalifanyika jana Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Ilieleza kuwa viongozi hao wamezungumzia masuala ya maendeleo hasa katika nyanja ya uchumi na kusisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuongeza ushirikiano na kuondoa vikwazo vya biashara na uwekezaji.

Kwa mujibu wa Ikulu, viongozi hao pia wamezungumzia hali ya usalama Afrika na umuhimu wa wakuu wa nchi kujadiliana na kutafuta suluhisho la migogoro hiyo inayosababisha vifo vya watu wasio na hatia hasa wanawake na watoto.

Obasanjo amempa pole Rais Samia kwa kifo cha Dk Magufuli aliyefariki Machi 17, mwaka hu una kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Mkapa kilichotokea Julai 23, 2020.

Rais huyo mstaafu wa Nigeria amempngeza Rais Samia kwa kupokea kijiti cha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumtakia heri katika majukumu yake.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa IMF, Rais Samia amefanya mazungumzo kwa njia ya mtandao akiwa ofisini kwake Ikulu ya Chamwino, na amemshukuru Kristalina aliyekuwa nchini Marekani kwa ushirikiano na ufadhili mkubwa ambao IMF umeutoa nchini Tanzania.

Amemhakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano huo kwa lengo la kuendelea kujenga uchumi imara wa Tanzania.

Alimueleza juu ya hali ya uchumi wa Tanzania kwa sasa ambao ukuaji wake umeshuka kutoka wastani wa asilimia 6.9 mwaka jana hadi asilimia 4.7 hivi sasa kutokana na changamoto za janga la Korona (Covid-19) ambalo limeathiri sekta za uzalishaji na huduma za kijamii zikiwemo utalii, afya na kilimo.

Rais Samia alisema japo kuwa hali ya uchumi wa Tanzania bado ni nzuri, serikali inahitaji kushirikiana zaidi na IMF kunusuru sekta zilizoathirika na janga la Korona na kuendeleza miradi ya kimkakati ambayo utekelezaji wake unaendelea ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere katika mto Rufiji utakaozalisha megawati 2,115, ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na ujenzi wa barabara na madaraja.

Alisema pamoja na kukabiliwa na changamoto hizo, serikali inaendelea kuchukua hatua mbali mbali za kuimarisha uchumi ikiwemo kujenga mazingira mazuri ya kufanya biashara kama vile kuondoa dosari za kikodi na ardhi, kuimarisha utawala bora na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Naye Kristalina amempa pole Rais Samia kufuatia kifo cha Dk Magufuli, amempongeza kwa kupokea kijiti cha Urais na amemhakikishia IMF ipo tayari kukuza zaidi ushirikiano wake na Tanzania kwa lengo la kuimarisha uchumi.

Alisema IMF ipo tayari kutoa ufadhili wa haraka kwa Tanzania kwa ajili ya kusaidia maeneo yaliyopata madhara makubwa ya kiuchumi kutokana na janga la Korona zikiwemo sekta za utalii, afya, uzalishaji na huduma za kijamii na amebainisha kuwa shirika hilo litafanyia kazi mara moja maombi ya mkopo nafuu kutoka Tanzania.

Aliongeza kuwa katika awamu ya pili, IMF imepanga kutumia Dola za Marekani bilioni 650 kwa ajili ya kusaidia kwa dharura uchumi wa nchi mbalimbali zikiwemo nchi zinazoendelea zilizopatwa na madhara ya Korona.

Kutokana na ahadi hiyo, Rais Samia amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula waliohudhuria mazungumzo hayo, kukamilisha haraka mchakato wa maandiko ya kuomba mkopo nafuu kutoka IMF ili fedha hizo zisaidie kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za kijamii.

Wakati huo huo, Rais Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Kenya kwa mwaliko wa Rais Uhuru Kenyatta ambako anatarajiwa kuhutubia Bunge la Kenya na kuhudhuria mkutano wa Jukwaa la Wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania jijini Nairobi.

SERIKALI inakusudia kurejesha mfumo wa maendeleo ya sanaa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi