loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mkutano wa wakandarasi na bodi yao ulivyoibua changamoto

HIVI karibuni Bodi ya Makandarasi Nchini (CRB), ilifanya mkutano na wakandarasi wazalendo jijini Mbeya ikiwa ni mwendelezo wa mikutano yake kwa ajili ya kusikiliza kero zao na kuziwasilisha serikalini kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi.

CRB imekuwa ikiendesha mikutano ya aina hiyo kama sehemu ya kuwajengea uwezo wakandarasi ili waweze kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi na hivyo kuokoa fedha nyingi kama ingefanywa na wageni.

Kwenye mkutano huo wa siku mbili uliowashirikisha zaidi ya wakandarasi wazalendo 300 wa Nyanda za Juu Kusini, mambo mbalimbali yaliibuliwa ambayo serikali iliahidi kuyachukua na kuyafanyia kazi.

Miongoni mwa masuala yaliyolalamikiwa sana na wakandarasi wengi ni uamuzi wa serikali kufanya miradi ya ujenzi yenyewe kwa kutumia utaratibu wa force account. Huu ni utaratibu ambao miradi kama ya ujenzi inafanyika bila kutumia mfumo wa zabuni na wahandisi wa taasisi za serikali ndio husimamia ujenzi kwa kutumia mafundi wa kawaida wa eneo husika.

Wakandarasi hao wanasema utaratibu huo unawadhoofisha kiuchumi na kitaalamu kwani wamekuwa wakikaa muda mrefu bila kuwa na shughuli za kufanya, huku wakiwa na madeni na wafanyakazi wanaowalipa kila mwezi.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabondi Electrical Contractors, Anania Mwakibete anasema utaratibu wa serikali kufanya miradi ya ujenzi yenyewe kwa kutumia mfumo wa force account umedidimiza uchumi wa kampuni za wakandarasi wazalendo.

Anasema miaka ya hivi karibuni kulijengeka utaratibu wa miradi mingi ya serikali kufanywa na taasisi zake kama Suma JKT kwa maelezo kuwa wakandarasi binafsi wamekuwa wakichelewesha kukamilika kwake au kutoza fedha nyingi.

Anasema hata taasisi za umma zinazopewa zabuni na serikali nazo zimekuwa zikitekeleza miradi kwa fedha zinazolingana au kukaribiana na zile za wakandarasi binafsi kutokana na gharama za manunuzi ya malighafi za ujenzi.

“Tunaomba serikali hii ifikirie kuturudishia kazi zetu, isiue ujuzi wetu. Ukiangalia wakandarasi wengi tuna hali mbaya kiuchumi sisi na familia zetu na wengine wamekopa benki, wameshindwa kurejesha mikopo kutokana na uhaba wa kazi,” anasema.

Mkurugenzi wa Videfca Construction ya Iringa, Vitusi Mushi, anasema wakandarasi hawakatai baadhi ya miradi kutekelezwa kwa mfumo wa force account lakini isichukuliwe kuwa wakandarasi wazawa hawawezi.

Anasema mara kadhaaa wakandarasi wazalendo wamekuwa wakilalamikiwa kwamba wanachelewesha miradi hata 

“Sisi tunakaguliwa mara kwa mara na kutoa vyeti vya kazi mahali tulipofikia kitu ambacho hatudhani kwamba kinafanyika kwenye utaratibu wa force account, halafu wao wanaletewa malighafi zote eneo la kazi kama nondo, mchanga, kokoto, saruji wakati sisi tunatafuta wenyewe wakati mwingine mbali na malipo yanachelewa,” anasema.

Anasema wakandarasi wengi walikuwa wakilaumiwa kuchelewesha miradi ya maji lakini ukweli ni kwamba watoa kazi wengi ndio walikuwa wakichelewa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi husika.

“Unakuta kiongozi anakuja anahoji mbona mradi haujakamilika na bila kujali sababu zilizochelewesha mradi anaamuru utaratibu wa force account utumike, mradi unaweza kufanywa haraka lakini usiwe na kiwango, ukiichunguza miradi mingi ya force account inajengwa harakaharaka je, tujiulize ina ubora kama miradi yetu,” anahoji.

Edna Kajiba ambaye ni Mkurugeni wa Kampuni ya Shahazuru anasema ni matarajio yake kuwa serikali mpya itasikiliza kilio cha wakandarasi wazalendo ili kuwapa kazi nyingi zitakazosaidia kuimarisha mitaji yao.

“Sisi wakandarasi wazalendo tunaamini kwamba Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, atasikiliza kilio chetu tupewe kazi na tuwe tunalipwa kwa wakati ili tukamilishe miradi husika kwa wakati kwa sababu usipolipwa kwa wakati huwezi kukamilisha kazi kwa wakati,” anasema.

Kilio cha wakandarasi hao kuhusu Force account kinaungwa mkono na Mwenyekiti wa Bodi ya CRB, Consolatha Ngimbwa ambaye anasema kweli utaratibu huo umewadhoofisha wakandarasi wengi na kubaki maskini.

Anasema baada ya wakandarasi kulalamikiwa kwamba zabuni zao ziko juu na hawajui kujaza zabuni hizo, CRB iliamua kufanya mafunzo nchi nzima kwa wakandarasi hao na sasa wameshaiva na wako mahiri kwenye ujazaji wa zabuni hizo.

“Kwa sasa tulipofikia kunatia matumaini na tunaomba mtupe kazi yoyote tutaifanya kwa ufanisi na kwa wakati kwa sababu wakandarasi hawa tuliwapa mafunzo na wameiva,” anasisitiza Ngimbwa.

Anawataka wakandarasi kuungana ili waweze kuwa na mitaji mikubwa na zana za kazi, hali ambayo itawawezesha kumudu kutekeleza miradi mikubwa na kuacha ubinafsi wa kila mtu kufanya kazi kivyake.

Anasema kuna baadhi ya wakandarasi ambao walijaribu kufanya miradi ya ujenzi pamoja lakini wengi wamekuwa wakianza vizuri na kumaliza vibaya kutokana na ubinafsi wa baadhi yao.

Anasema wakandarasi hao kwenye maazimio yao wanataka kuanzisha benki itakayowasaidia kuwakopesha wanapokwama kwenye kutekeleza miradi lakini hawawezi kufanikiwa bila kuungana na kuwa na sauti moja ya kuwasemea.

“Tuna vyama vingi vya wakandarasi lakini nashauri ikiwezekana tuviunganishe tuwe na chama kimoja chenye nguvu ili kupata sauti ya kuzungumza na serikali kuhusu changamoto zetu... Hata hii benki tunayosema hatuwezi kuianzisha bila kuwa kitu kimoja maana tutashindwa kuiendesha,” anasema.

Akifunga mafunzo hayo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Leonard Chamuriho, anasema serikali inatamani kuona miradi mikubwa ya ujenzi kama ule wa Reli ya Kisasa (SGR) Mradi wa Umeme Rufiji (JNHPP) inafanywa na kampuni ya wazalendo.

Chamuriho anasema si kwamba serikali inafurahia kuona kazi hizo zikifanywa na kampuni za kigeni ndiyo maana itaendelea kuwajengea uwezo wakandarasi wa ndani ili waje kuzifanya.

Anasema ndiyo sababu serikali itaendelea na utaratibu wake wa kutenga baadhi ya miradi kama sehemu ya kuwajengea uwezo wakandarasi wa ndani kiuchumi, rasilimali watu na zana bora za kufanyia kazi.

Anasema iwapo kampuni za wazalendo zitaimarika kutakuwa na ushindani kwenye zabuni za ujenzi, hali ambayo itasababisha kushuka kwa gharama za ujenzi, hivyo serikali kuokoa fedha nyingi.

Anasema katika mkakati huo wa kuwainua wazalendo, serikali itasimamia sheria ya manunuzi kuhakikisha miradi yote isiyozidi Sh milioni 10 wanapewa wakandarasi wa ndani kwani fursa hiyo iko kisheria na inahitaji utekelezaji pekee.

Waziri anawataka wakandarasi hao wanapopewa kazi za ujenzi kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na miradi ikamilike kwa wakati na kwa kuzingatia makubaliano ya kwenye mikataba yao.

Akizungumza namna CRB inavyowalea wakandarasi wazalendo, Msajili wa Bodi hiyo, Rhoben Nkori anasema wamekuwa wakiandaa mikutano ya mashauriano ya aina hiyo mara kwa mara ili kuwajengea uwezo wa kuongeza madaraja yao.

Anasema kwa mwaka huu pekee mbali na mkutano wa Mbeya watakuwa na mkutano mkoani Arusha, Dar es Salaam na Mwanza, lengo ikiwa ni kusikiliza kero zao na kuziwasilisha serikalini kwa ajili ya ufumbuzi.

Nkori anasema CRB imeendelea kuimarisha mfuko wa kusaidia wakandarasi (CAF) kwa kuwadhamini wakandarasi wazalendo Benki ya CRDB ili wapewe dhamana kwa ajili ya zabuni na malipo ya awali.

Anasema mwaka 2020 bodi ilifanikiwa kufanya majadiliano na Benki ya CRDB na kufikia makubaliano ya kudhamini wakandarasi wa ndani wa madaraja yote, badala ya wakandarasi wadogo na wa kati.

Nkori anasema bodi ilihakikisha kiwango cha dhamana kinaongezeka kutoka Sh milioni 50 hadi milioni 100 ingawa anasema kiasi hicho bado ni kidogo kulinganisha na mahitaji halisi ya wakandarasi .

Nkori anasema mikutano hiyo ya mashauriano imekuwa muhimu kwani bodi imekuwa ikikutana na waajiri wakuu na wasimamizi wa sera na kujadiliana na kufanya maboresho kwenye upungufu.

Anasema mikutano hiyo ambayo hufanyika kila mwaka imekuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya wakandarasi nchini kwani wengi wameboresha kazi zao.

Nkori anataja baadhi ya maazimio ya wakandarasi hao kuwa ni kuitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iweke utaratibu mzuri wa kuwaelimisha wakandarasi kuhusu masuala ya kodi na kutoza kodi halisi kulingana na biashara ya ukandarasi.

Anasema wakandarasi wameomba malipo yao yafanyike kwa wakati, pale yanapocheleweshwa yalipwe kwa riba kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Anasema CRB itafanya mikutano ya mashauriano kama hiyo kwa kanda katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza, lengo ikiwa ni kuwajengea uwezo wakandarasi hao wazalendo.

LINUS Robert wa kijiji cha Mabamba, wilayani Kibondo, ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi