loader
Dstv Habarileo  Mobile
DARASA LA RAMADHANI:  Kuswali usiku kumi la mwisho  na umuhimu wa Zakatulfitr

DARASA LA RAMADHANI: Kuswali usiku kumi la mwisho na umuhimu wa Zakatulfitr

WAISLAMU sasa wako katika kumi la mwisho ambalo mashehe wanasema ni kumi nyeti ambalo watu wanapaswa kufanya ibada kwa wingi, hususan swala za usiku.

Ingawa usiku wenye cheo uitwao Lailatulqadir umefichwa ili kuwafanya watu kujipinda kwa kufanya ibada usiku kuutafuta, riwaya nyingi zinaonesha kwamba unapatikana katika kumi hili la mwisho.

Mashehe wanasema endapo wanadamu wangeijua kwa uhakika siku hiyo basi hata wasingeshughulika kufanya ibada kwa wingi katika zile siku nyingine za Ramadhani.

Lailatulkadir ni nini? Kurani inasema: "Hakika tumeiteremsha (Kurani) katika usiku wa Lailatuqadri (Usiku wenye heshima kubwa na unaopatikana katika mwezi wa Ramadhani pekee).

Kurani inazidi kusema: Ni nini kitakujulisha usiku huo wa Lailatulqadir? Usiku huo (mmoja tu) wa Lailatulqadri ni bora kuliko miezi elfu.  (97:1-3).

Usiku huu kama Mwenyezi Mungu anavyotudokeza katika Kurani, ameupa heshima kubwa sana hadi ukafikia kuipita miezi elfu  ambayo ni sawa na miaka 83 na miezi 4.

Hii maana yake ni kwamba anayefanya mema katika usiku huu mmoja tu, huwa sawa na aliyefanya mema kwa muda wa miezi 1,000, na afanyaye maovu usiku huu, pia naye huwa amejidhulumu nafsi yake kwa kujichumia adhabu kubwa.

Inawezekanaje usiku mmoja tu kuishinda miezi elfu? Hili ni swali wanalojiuliza baadhi ya watu.

Jibu linaweza kuwa kwamba sote tunaamini ukweli wa Mwenyezi Mungu. Hangeweza kutujuza habari zisizo na ukweli. Pia kulingana na fahamu zetu, hatuwezi kufikia ujuzi wa hali ya juu wa Mwenyezi Mungu ambaye ni mwenye uwezo mkubwa.

Mfano ambao ni karibu zaidi katika kulifafanua swali hili ni huu kwamba pale mtu anapopanda mbegu moja ya papai, ambayo kwa kawaida huwa ndogo sana, atastaajabu kuona imetoa tunda ambalo ni kubwa kinyume na mbegu ya embe ambayo ni kubwa na lakini wakati wa kuzaa hutoa tunda dogo.

Hivyo kwa Mwenyezi Mungu si ajabu kuona usiku mmoja tu ukishinda miezi elfu kwa thawabu na utukufu.

Kama usiku huo umefichwa kwa nini kumi la mwisho? Kumi la mwisho linatajwa na mashehe wengi kwamba huenda ndimo ilimo Lailatulqadir.

Katika jitihada zao wanataja siku kama vile Ramadhani 21, 23, na 27 kuwa huenda ndio Lailatulkadir. Ramadhani 19, 25 na 29 pia zinatajwa ingawa wengi wanaitaja zaidi Ramadhani 27.

Inaelezwa kwamba kumi la mwisho ndilo ambalo Mtume Muhammad (S.A.W) alikuwa akiwaamsha wake zake pamoja na wanawe kwa ajili ya kukithirisha kufanya ibada za usiku na kumuomba Mwenyezi Mungu.

Shehe Abdulkadir al-Ahdal, Rais wa Al-Hikima Foundation na mmoja wa mashehe wakubwa nchini anasema, muumini akishaswali swala hiyo haimzuii kuendelea na swa la zingine za usiku.

Hata hivyo, anasema kwamba mtu akishaswali swala ya Witri yenye rakaa tatu wakati wa tarawehe, hatakiwi kusali tena sala hiyo endapo ataamka na kuswali swala za usiku wa manane.

Shekhe anaweka angalizo kwamba Witri haiswaliwi mara mbili na kwamba ipo hadithi inayoonesha kwamba Mtume Muhammad (S.A.W) aliswali witr ya jamaa na kisha akasimama usiku na kuswali jumla ya raka nne bila kuswali tena witri.

Kadhalika Shekhe anasema kwa watu walioko kwenye ajira, ambao wanahofu kwamba wakiamka usiku watashindwa kufanya kazi zao za maofisini sawasawa, basi tarawehe pamoja na witri vinawatosha na watahesabiwa kwamba wamesimama usiku kuswali kama wengine wenye nafasi.

Hata hivyo, Shekhe anasisitiza kwamba kumi hilo la mwisho si la kulala. Ni la kujipinda kwa kufanya ibada usiku kadri mtu anavyoweza. 

ZAKAT ALFIRT

Lakini pamoja na kukumbushana kufanya ibada zaidi katika kumi hili ikiwemo kusimama swala za usiku, Waislamu wanapaswa kuanza kujiandaa na zaka inayotolewa mwisho wa funga (Zakat al-Fitr.

Zaka hii ni lazima kutolewa na kila Muislamu mwenye uwezo wa kutoa ambapo anajitolea yeye mwenyewe na wale wanaomtegemea. 

Wanazuoni wameeleza kuwa asie muislamu ambae anaishi na waislam na mahitaji ya waislam wale yote pamoja na mambo yao yote wanamtegemea yeye anaweza kuwatolea wahusika Zakatulfitr. Mfano, kama asie Muislam anawalea watoto wa kiislam au ana wafanyakazi waislam, hawa anaweza kuwatolea Zakatulfitr.

MUDA WA KUTOA

Muda wa kutoa zaka hii umegawika katika sehemu mbili; kuna wakati unaofaa na kuna wakati ambao ni lazima kutoa.

Wakati unaofaa ni kuanzia mwanzo wa mwezi wa Ramadhani ambapo Muislam anaweza kutoa zaka yake na wakati wa lazima kutoa unaanzia tokea kuzama kwa jua katika siku ya mwisho wa mwezi wa Ramadhani na unaishia kabla ya kuswali swala ya Idd.

Zaka hii hii inapendeza zaidi kutolewa siku tatu au mbili kabla ya siku inayotazamiwa kuwa Idd.

Ama mtu akitoa baada ya swala ya Idd hiyo haiwi Zakatul fitr bali itakuwa ni sadaka miongoni mwa sadaka na kama alikuwa na uwezo wa kutoa lakini akachelewesha kutoa mpaka baada ya swala ya Idd atakuwa amefanya makosa na hivyo atakosa fadhila za kutoa zaka hiyo.


KIWANGO CHA ZAKA
Kiwango ni pishi moja ambayo ni sawa na kilo mbili na nusu ya chakula kinachopendelewa na wakazi wa eneo husika wakati wa sherehe. Kwa Tanzania ni mchele.

Lakini pia kwa kuwa kipimo cha pishi na kilo vina tofauti, wapo waliosema kuwa pishi moja ni sawa na kilo mbili na nusu na wengine kilo tatu. Kwa hiyo kama unaweza kutoa kilo tatu ni bora zaidi.


Wanazuoni pia wanaona kwamba kinachotakiwa kutolewa hasa ni chakula na si pesa lakini pia wapo wanaoona ni vyema kutolewa kwa pesa kutegemea na mazingira na hasa inashauriwa kutoa pesa kwa taasisi husika ndizo zinunue chakula na kuwapa maskini.

Mashehe pia wanaona kwamba kumpa mtu maskini mchele, bila mafuta, mkaa na mboga pia unaweza kuwa hujamsaidia. Na hivyo, wapo wanaoshauri kama una uwezo wa ziada basi si vibaya ukamsaidia fukara vitu hivyo pia.

WANAOTOLEWA ZAKATUL-FITR
Kwanza kabisa anatakiwa ajitolee yeye mwenyewe kiongozi wa familia na kisha atawatolea wale wote walio chini ya himaya yake kulingana na uwezo wake. Hii ni pamoja na wazazi kama wanamtegemea.

Hata mtoto aliyezaliwa siku ile au kipindi kile cha kuzama jua katika siku ya kuandama mwezi anatolewa pia. Kwa mtoto aliyeko tumboni hakuna zakatulfitr inayotolewa kwa ajili yake kwa mujibu wa wanazuoni, lakini kama utaamua kumtolea hakuna kosa. 

Pia inaruhusiwa kutuma zakatulfitr kutoka sehemu moja hadi nyingine, kwa mfano kutoka Dar es Salaam na kuwapelekea fukara sehemu yoyote, lakini inapendeza zaidi mtu kuwapa maskini wanaomzunguka.

HUKUMU YA MADENI
Ikitokea mwenye deni la kulipa au muda wa kulipa deni umekwishafika na yeye ikawa kile kiasi anachodaiwa amekwishakiweka pembeni na siku ile ya kuandama mwezi ikawa hana ziada nyingine zaidi ya kile alichokitenga kwa ajili ya kulipa deni, hapo hatowajibika kutoa Zakatulfitr.

Lakini kama tarehe au muda wa kulipa haujafika au umefika lakini kile kiasi anachotakiwa kulipa deni ikawa bado hajakitoa hapo atalazimika kutoa Zakatul- fitr kwani bado itakuwa inahesabika kuwa hii ni sehemu ya mali yake.

WANAOSTAHIKI KUPEWA
Zakatulfitr inachukuliwa kutoka kwa Waislamu wenye uwezo wa ziada ya mahitaji yao ya chakula siku ya Idd, na hivyo inatakiwa wapewe Waislamu ambao hawana uwezo wa mahitaji yao ya chakula siku ya Idd, yaani mafakiri na maskini. 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/45368b4ec247c820abdf55f287853cf7.jpg

MISITU ni mkusanyiko wa uoto unaojumuisha ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi