loader
Binti wa kiafrika aliyetembea nchi zote duniani

Binti wa kiafrika aliyetembea nchi zote duniani

JESSICA Nabongo, binti wa Kiafrika mwenye umri wa miaka 36 amekuwa mwanamke wa kwanza mweusi kurekodiwa kusafiri nchi zote duniani.

Binti huyu raia wa Marekani mwenye asili ya Uganda, bloga wa masuala ya usafiri na mwenye ushawishi, ambaye alizaliwa mjini Detroit, Michigan kwa wazazi raia wa Uganda anasema jambo moja analojivunia ni kutambua ukweli katika maisha ‘Dunia ni jirani yetu’.

Ukweli huo aliueleza wazi katika mahojiano na Jarida la Travel+Leisure ambapo alisisitiza: “kwangu, nyumbani ni watu. Unaweza kupata nyumbani katika maeneo mbalimbali, hata kama unatembelea kwa mara ya kwanza.”

Nabongo anaamini kuwa kila kwenye watu ni nyumbani, kila mtu ni jirani, haijalishi yupo wapi duniani. Vile vile anaamini kuwa watu wengi ni wazuri na wako sawa kuliko tofauti zao.

“Kusafiri kumenifanya ni tambua haijalishi wewe ni Muislamu au Myahudi, Mwafrika au mzungu, mwanaume au mwanamke, wote ni binadamu… na katika kusafiri na kuzungumza na watu katika maeneo ya vijijini, katika zinazoendelea na uchumi mdogo, ndio unapata kutambua, ‘oh kumbe wewe kama mimi. Kweli, hatuzungumzi lugha moja, lakini hali zetu sawa,” anasema Nabongo.

Miongoni mwa maeneo ambayo binti huyu wa Kiganda alitembelea ni Kambi ya Ng’ombe Sudan Kusini, kupanda puto la hewa ya joto Myanmar, kutembelea duka la kinyozi linalomilikiwa na mkimbizi raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC) nchini Malawi na hata Korea Kaskazini.

Nabongo katika orodha yake ya matukio ameshatembelea nchi 195, ameishi Benin, Italia, Japan, Uingereza, Marekani (Washington, New York, Detroit), ameshabadilisha kazi mara sita, kuzindua biashara mbili zilizofanikiwa na kutengeneza maisha anayoyataka. Mwaka 2019 pekee, alitembelea nchi 66 kati ya hizo 46 zikiwa mara ya kwanza. Ameshafanya safari 170 za ndege, ameshatumia saa 601 katika ndege na kuruka maili 244,547. Nchi ya mwisho kuitembelea ni Kisiwa cha Shelisheli. Aliwasili nchini humo Oktoba 6, 2019 ikiwa ni nchi ya 195.

Kila kitu kina sababu zake lakini la msingi kwa binti huyu, udadisi juu ya ulimwengu na watu waliomo ulimsukuma mwaka 2017, kuanza safari yake ya miaka miwili na nusu duniani. Anasema kuna chimbuko ambalo limemfanya awe hivi alivyo: “Kusafiri kimsingi ni sehemu ya mimi,” anasema Jessica ambaye alianza kusafiri kimataifa akiwa na umri wa miaka minne na wazazi wake katika maeneo mbalimbali duniani kama Jamaica, Mexico, Uganda, London na Canada.

Hadi anamaliza kidato cha sita, Jessica alishatembelea nchi nane na ndio kwanza alikuwa anaanza.

Ukimfuatilia Nabongo unagundua kwamba ametumia miaka mingi kukatiza katika ramani ya dunia, kwanza aliacha kazi kwenye kampuni moja kwa ajili ya kwenda kufundisha lugha ya kiingereza nchini Japan, kisha alikwenda kujiunga na Shule ya Uchumi London, halafu alikwenda kuishi Benin, Afrika Magharibi na Rome, Italia wakati akifanya kazi na Umoja wa Mataifa.

Kwa ujumla aliishi katika nchi tano ndani ya mabara manne na hadi muda wake wa kusafiri kuizunguka dunia ulipokuwa umepamba moto, tayari alishatembelea nchi 60. Kutokana na mzunguko wake huo ndio maana amekuja na kauli mbiu yake inayosema Catch Me If You Can.

Mbali ya Nabongo kusafiri na marafiki na familia, lakini amefanya safari zake akiwa mwenyewe. “Faida ya kusafiri binafsi, inakuruhusa fursa ya kuhusiana na watu wa ndani vizuri,” anasema.

Anaongeza kuwa, “ tunaposafiri na wengine, tupo na watu hao, mara nyingi, hatuwafahamu watu wa ndani. Lakini ukisafiri mwenyewe inakupa fursa mara nyingi, kwa njia nyingi, kuchunguza kwa undani kwa maana ya kutengeneza uhusiano na kutumia muda mwingi wa kujichanganya na wenyeji.”

“Inapokuja katika nchi za watu wenye rangi nyeusi na kahawia, mara nyingi mtazamo ni chanya na huo haukuwa uzoefu wangu,” anasema na kuzitaja nchi za Sudan, Somalia, Afghanistan na Saudi kama sehemu ambazo alikuwa na uzoefu nazo vizuri.

“Nakumbuka kabla, nilipokwenda Urusi, Saudi na Libya, watu walikuwa wakiniambia, ‘ unatakiwa kuwa makini. Urusi hawapendi Waafrika, Saudi wanachukia Waafrika., lakini tayari nilikuwa na uzoefu mzuri katika nchi zote hizi,” anasema.

Pamoja na mambo kuonekana shwari kwake Nabongo amekutana pia na changamoto katika safari zake hizo.

“Nimekuwa nikihojiwa sana na uhamiaji katika nchi mbalimbali, kwa sababu hawaamini, mmiliki wa Hati ya Kusafiria Mganda, anaweza kufanya utalii,” anasema Nabongo ambaye hutumia Hati ya Kusafiria ya Marekani na Uganda, kulingana na nchi anayokwenda.

Nabongo anasema kumbukumbu yake nyingine ni katika eneo la kijiji kimoja nchini Kyrgyzstan, alipogundua watu kwenye magari barabarani walikuwa wakisimama kumshangaa alipokuwa akivuka kwenda kutafuta laini ya simu ya eneo hilo.

“Nilijiseme, ‘Oh yeah, duh, mimi Mwafrika, huenda hawajawahi kuona mtu mweusi hapa…sio kwamba nilisahau mimi ni mweusi, la hasha, lakini sio kitu ambacho nimekuwa nikifikiria mara kwa mara,” anasimulia.

Pamoja na hayo Nabongo anasema kwamba amekuwa na ujasiri mkubwa pamoja na maelezo ya watu kuhusu masuala ya usalama. Vikwazo mbalimbali havijawahi kumrudisha nyuma. “Nawafahamu Waafrika wengi , ambao wamekuwa wakiniuliza nchi gani waafrika wako salama? Lakini mimi linapokuja suala la kusafiri sizingatii jambo hilo. Wala sitafuti katika mtandao ‘eti waafrika kwenye nchi X wanachukuliwaje, kwangu mimi, nastahili mahali popote nitakapokuwepo.”

Anakiri kuwa watu wana uzoefu tofauti tofauti wa maisha ambao unaweza kuchochea vitendo vyao na wasiwasi.

Nabongo anatoa wito kwa kila mtu kutokuwa na woga. “Nataka kila mtu, ajisikie dunia iko kwa ajili yake kuitafiti. Nataka tuondokane na hofu, iwe ni mwanamke au mwanaume, mzungu au mwafrika. Ninataka watu watambue kuwa ulimwengu ni wa sisi wote kuchunguza.”

Huu ndio mtazamo wa Jessica Nabongo, mtazamo ambao amekuwa akiubeba anapokwenda nchi moja hadi nyingine.

Katika nchi 195 alizotembelea, msafiri huyo asiyekuwa na woga, anabainisha katika uzoefu wake,amefurahiza zaidi katika nchi zisizotembelewa, wala kupewa kipaumbele, kwa sababu, “ watu wenyewe wanashauku kupata watalii, na pia wanataka kuonesha watu wageni uzuri wa nchi yao na kuondoa mtazamo hasi unaoelezwa katika taarifa za habari.

Kati ya maeneo ambayo hayathaminishwi lakini yanajulikana, Nabongo anayataja kuwa ni Sudan, Namibia, Norway Kaskazini, Madagascar na Tonga. Anasema :“ Sudan kwa sababu ina piramidi nyingi na ya zamani zaidi kuliko Misri. Kuna Bahari Nyekundu, unaweza kuzamia na masuala ya kitamaduni. Inavutia.”

Nabongo anasema, “ Namibia ni nchi nzuri sana kama unataka kufanya utalii kwa njia ya barabara. Kuna Jangwa la Sossusvlei, Skeleton Coast, na mengine mengi mazuri.”

Kwa upande wa Norway Kaskazini anasema kuna maeneo mengi ya kutembelea kama fukwe, misitu ya mvua na miti ya mibuyu, hii ni baadhi ya mifano ya maeneo aliyokwisha tembelea.

Kutokana na shughuli zake za masuala ya kusafiri, thamani halisi ya Nabongo ya kipato imekuwa ikiongezeka kutoka 2019-2020 . Chanzo kikubwa cha kipato chake ni bloga na huyu hasa ndiye bloga aliyefanikiwa. Kipato chake kimetoka dola za Marekani milioni moja hadi Dola za Marekani milioni tano.

Nabongo anajulikana kwa kuanzisha kampuni inayoitwa Jet Black, ambayo hufanya kazi ya kuandaa safari kwa ajili ya makundi madogo kufanya safari Afrika, pamoja na kuuza mavazi ya safari kwenda nchi na maeneo mbalimbali duniani, kama fulana zenye brandi na majalada ya hati za kusafiria.

Pia amekuwa akifanya kazi za kutangaza hoteli na maeneo mbalimbali ya kitalii duniani.

Mbali na mapenzi yake makubwa katika masuala ya usafiri na utalii, Jessica Nabongo pia ni msomi. Mwanadada huyu ana Shahada ya Pili ya Maendeleo ya Kimataifa kutoka Shule ya Uchumi London na Shahada ya Kwanza ya Sanaa katika lugha ya Kiingereza kutoka Chuo Kikuu cha St John, mjini NewYork.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/6a89e3dd0e987ee8bfe9c4cb16d5e2a3.jpeg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi