loader
ZAKIA MEGHJI Mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Fedha Tanzania

ZAKIA MEGHJI Mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Fedha Tanzania

WIZARA ya Maliasili na Utalii, ndio nilipokaa kwa muda mrefu maana nilikuwa huko kama waziri kwa miaka mitano ya Rais Benjamin Mkapa (Rais wa Awamu ya Tatu) na nilipogombea ubunge kwa mara nyingine, nikateuliwa tena katika nafasi hiyo, kwa hiyo nimekaa karibu miaka tisa na nusu katika Wizara ya maliasili na Utalii nikiwa Waziri na ninajivunia mpaka sasa mimi ndiye waziri niliyekaa muda mrefu kuliko waziri mwingine yeyote katyika wizara hii na rekodi yangu haijavunjwa.”

Ndivyo anavyosema mwanasiasa mkongwe na kiongozi mstaafu katika ngazi na wadhifa mbalimbali katika Chama cha Mapinduzi(CCM) na serikali nchini Tanzania, Zakia Hamdani Meghji.

Zakia anasema hata alipoingia madarakani, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alimteua na kuwa Waziri wa Fedha wa Kwanza Mwanamke nchini Tanzania na alipotoka Wizari ya Fedha, aliendelea na ubunge na kwa upande wa chama alikuja kuteuliwa kuwa Katibu wa Fedha na Uchumi Taifa.

Anasema anamshukuru Rais Mstaafu Kikwete kwa kumuamini na kumteua kushika nafasi hiyo nzito na kwamba, siku alipotangazwa kuwa waziri wa Fedha, alishtuka.

“Lakini Rais Kikwete alinitia moyo; akaniambia Meghji; utafanya na kazi hii utaifanya vizuri… kwa kweli nashukuru kwamba nilipata ushirikiano mzuri na wa kutosha hapo wizarani. Hakuna kitu kizuri sana kama ushirikiano na wakurugenzi, katibu mkuu pia, nilikuwa na manaibu waziri tulioshirikiana vizuri,” anasema.

Huyu ndiye Zakia, ambaye sasa ni mwanamke Mtanzania mstaafu aliyehudumu katika nafasi mbalimbali katika siasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikalini kwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwa ni pamoja na kuwa waziri wa fedha wa kwanza mwanamke nchini Tanzania.

Anasema amekuwa katika ulingo wa siasa tangu akiwa kijana na ameanza hatua za chini. Anabainisha kuwa, aliwahi kuwa mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa, na kisha akashika nafasi mbalimbali za uwaziri serikalini.

Ndani ya CCM, amehudumu katika Kamati Kuu kwa miaka 20 na Halmashauri Kuu, baadaye akawa Katibu wa Fedha na Uchumi wa chama hicho.

Kuhusu taaluma Zakia Meghji anasema: “Kitaaluma, mimi ni mwalimu na ualimu ndio niliosomea katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika digrii yangu ya kwanza, lakini katika digrii yangu ya pili, nilisomea masuala ya uchumi.

“Kwa hiyo baada ya kumaliza masomo ya chuo kikuu nilifanya kazi kama mwalimu katika Shule ya Sekondari Jangwani na kisha, tukaenda Moshi kwa sababu mume wangu alipata uhamisho kwenda Moshi katika Chuo cha Ushirika,” anasema.

Meghji anasema alilazimika kumfuata mumewe na kuanza kufundisha katika Shule ya Sekondari Weruweru na alikuwa akifundisha masomo zaidi ya Historia na Kiingereza.

“Hata hivyo huko sikufundisha kwa muda mrefu sana katika Sekondari ya Weruweru kwani baada ya hapo ilitokea nafasi katika Chuo cha Ushirika Moshi baada ya kufanyika mabadiliko kidogo ya muundo uliotaka kuanzishwa kwa Idara ya Wanawake na Ushirika.

Anasema wakati huo ushirika ulikuwa na nguvu sana Moshi, Kilimanjaro wakati huo (KNCU), lakini wanawake ndio walikuwa wazalishaji kama ni kahawa n.k, hata hivyo hawakuwa na nafasi katika vyama vya ushirika.

“Kutokana na hilo, walitaka kuanzisha idara ili kuwahamasisha wanawake, lakini wanaume pia wakubali pia kuwa wanawake wana nafasi yao katika vyama vya ushirika… Kwa hiyo, wakaanzisha idara na wakasema anayetaka aombe, nikaomba nafasi, Alihamdulillah! Nikapata nafasi na kuwa Mkuu wa Idara ya Ushirika wa Wanawake,” anasema.

Akiwa huko, anasema ilitokea nafasi katika Shirika la Kimataifa la Ushirika (International Corporate Alliance).

Alipoomba nafasi hiyo, alifanikiwa, hivyo akawa anahudumia elimu ya vijana na wanawake na kutokana na nafasi hiyo alitembelea nchi kadhaa katika mafunzo mbalimbali. Alikuwa akihudumia nchi 10 za Afrika.

Anasema wakati akifanya hivyo na alikuwa katika mafunzo, aliweza kusaidia sana watu wa nyumbani (Watanzania) wengi hasa upande wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) katika Mkoa wa Kilimanjaro.

“Nilikuwa nawapeleka mara nyingine Mauritius, kutoka Zanzibar labda wanakwenda S waziland n.k nikafanya hiyo kwa muda mrefu,” anasema.

ALIVYOKUWA MBUNGE WA VITI MAALUMU

Baadaye mwaka 1985, kulikuwa na mabadiliko ya serikali ya kikatiba, yanayosema kuna nafasi za ubunge viti maalum kwa ajili ya wanawake na wanawake mkoani Kilimanjaro walimfuata na kumuomba agombee ubunge, lakini alikuwa anasita akiamini hataweza.

“Hii ni kwa sababu ubunge mmh; nilikuwa nawaangalia akinamama Lucy Lameck wakati ule, Mama Getrude Mongela, nikasema mimi mwalimu, sifikiri kama nitaweza, lakini wakasema hapana, hapana, ugombee… wakanilazimisha kwelikweli; wakaniambia wewe kubali tu, sisi tutakujazia fomu, kweli wakaniletea fomu, nawashukuru sana.”

Anasema baada ya kujaza na kuzipeleka Dodoma, alipitishwa kugombea nafasi hiyo ya mbunge ili ashindane na akinamama wengine anaosema ‘walikuwa wazito.’

Anamshuku na kumpongeza marehemu mumewe, Ramadhani Meghji, aliyemtia moyo na kumwambia atamsindikiza huku akinamama wa Kilimanjaro wakisema watamfanyia kampeni.

Zakia anasema katika duru la kwanza tu la uchaguzi, ‘akapita,’ kisha duru la kapu. “Sasa nikawa mbunge mwaka 1985 na mwaka 1988, bado nikiwa bungeni, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, akaniteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi.”

Anasema alimshirikisha mumewe kuhusu uteuzi huo. “Akasema, kuna watu chungu mzima, lakini Rais amewaacha na kukuchukua wewe (Zakia) hata kama utapata fedha kidogo, inabidi ukubali, basi nikakubali na namshukuru Mungu ikawa kama mpenyo wangu pale.”

Zakia anasema alikuwa mkuu wa wilaya kwa miaka miwili na alifanya mambo mengi na kukabiliana na baadhi ya changamoto likiwemo tukio la mafuriko na alijitahidi kufanya kazi kubwa ya kujituma na baada ya miaka miwili Rais Mwinyi alikwenda na kuangalia.

Anatoa mfano akisema kuna mama mmoja alikuwa azame, akamuokoa na huyo mama aliamua kumwita mtoto wake Zakia “walikwenda kumbatiza mtoto wao, wakasema, tutamuita Zakia.”

Kwa mujibu wa Waziri huyo mstaafu, baada ya miaka miwili akateuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa 

wa Mbeya, kisha akarudishwa tena Kilimanjaro kama Mkuu wa Mkoa na Katibu wa Chama wa Mkoa wakati huo kofia mbili, lakini baada ya muda tena, akateuliwa kwenda Dodoma, kama Katibu wa Sekreterieti ya Uchumi na Huduma za Jamii.

Anasema nafasi hiyo ilikuwa nyeti, lakini alifanya na kukaa kwa muda mfupi na yalitokea tena mabadiliko ya muundo, mwaka 1993 Rais Mwinyi akamteua kuwa Naibu Waziri wa Afya. Waziri wa Afya wakati huo alikuwa Profesa Philemon Sarungi.

Kwa mujibu wa Meghji, wakati huo wizara ililkuwa imekaa bila naibu waziri kwa muda wa miaka nane na wa mwisho, alikuwa Mustafa Nyang’anyi na yeye alikaa kama naibu kwa muda wa miaka miwili, baadaye kukawa na mabadiliko ya baraza la mawaziri, akapandishwa akawa Waziri wa Afya.

Anasema ukaja uchaguzi tena akagombea na kuchaguliwa tena kwa nafasi ya viti maalumu. Zakia anabainisha kuwa, wakati huo alikuwa anaingia madarakani Rais wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa (marehemu) mwaka 1995; naye akamteua kuwa Waziri wa Afya, lakini baada ya mwaka mmoja kukawa na mabadiliko ya baraza la mawaziri; ndipo Zakia akapelekwa Wizara ya Maliasili na Utalii.

KATIKA WIZARA YA AFYA

Katika wizara hii, Meghji anasema changamoto kubwa ilikuwa bajeti na uchumi mdogo, lakini anapongeza awamu za baadaye kwa kuongeza bajeti.

Anasema walijitahidi kufanya programu mbalimbali ikiwamo ya kuelimisha wananchi kuhusu HIV kwani kulikuwa na unyanyapaa mkubwa, lakini kutokana na uelemishaji huo masuala ya Ukimwi yakaanza kuzungumzwa kwa uwazi zaidi.

Changamoto nyingine ilikuwa malipo yaliyosababisha migomo ya madaktari na wataalamu wa afya. Anasema walijaribu kuzungumza na madaktari, lakini hawakukubali walitaka malipo, wizara ya fedha haikuwa na fedha na Rais alikuwa safari Afrika Kusini.

“Niliamua kufanya maamuzi magumu ya kuwafukuza madaktari, nikaamua kuwafuata jeshini ili madaktari wakiondoka tuchukue wa jeshini. Nilifanya maamuzi hayo kwa sababu, watu walikuwa wanafika kupata matibabu, hawapati wanakufa, halafu madaktari wamegoma kutoa huduma…”

“Maprofesa wakubwa hawakugoma, vijana ndio waligoma. Madaktari wakaa kikao baada ya kuwaeleza nataka nyumba zangu leo, jioni wakaja wakasema basi tunarudi kufanya kazi. Mpaka leo kiongozi wa madaktari hao ni rafiki yangu anakaa Uingereza na akija Tanzania na mkewe, lazima aje kunisalimia,” anasema Meghji.

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

Anasema kielelezo chake katika wizara hiyo ni kuwa amekaa 

na watu wizarani hapo vizuri pamoja na kwamba ilikuwa wizara yenye changamoto kubwa ikiwa ni pamoja na kuhusishwa na rushwa na tyuhuma mbalimbali za ufisadi.

Anasema wizara hiyo inahitaji kujifunza na ilikuwa kawaida yake akiingia katika wizara yoyote, anajifunza kwanza badala ya kuanza kutembea tu.

“Mimi nikifika najifunza kwanza, nachukua mafaili, nayaangalia na kusoma, ama sivyo, ukifika tu na kuanza kutembea, unaweza kudanganywa vitu vingine, ukafikiria ni kweli… kwa hiyo wizara ya maliasili na utalii, nilifanya hivyo na tulishirikiana na Katibu Mkuu wakati huyo Philemoni Luhanjo ambaye baadaye pia alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi pamoja na viongozi wengine,” anasema.

WIZARA YA FEDHA

Katika wizara hii, Zakia anasema changamoto kubwa ilikuwa bajeti ndogo, lakini ziliendelea kuongezeka kwa mambo yaliyokuwa muhimu na mojawapo ni masuala ya ujenzi wa barabara.

Anasema barabara inachukua fedha nyingi, lakini ulifanyika utaratibu katika kodi ya mafuta ya petroli zitolewe sehemu ya fedha asilimia 30 zitumike kwa ajili ya barabara. Hapo ndipo ulipoanzishwa mfuko wa barabara kwa kushirikiana na wizara ya ujenzi.

Mfano mwingine anasema ni mafuta ya kupikia wafanyabiashara walikuwa wakiagiza mafuta ghafi, lakini hawalipii ushuru, wanaingiza na kuuza, hivyo serikali ikaamua kuweka utaratibu wakiingiza mafuta wanalipia asilimia 10, jambo hilo liliwasaidia wakulima. “Haya ni baadhi ya mambo niliyoyasimamia nikiwa waziri wa fedha,” anasema.

“Mimi nafikiri siri ya mafanikio ni kujituma, hilo ndio la kwanza, lakini pia kushirikisha watu… kwa mfano nilipokuwa mimi Wizara ya Maliasili na Utalii nilikaa kama miaka tisa na ninajivunia mpaka sasa hivi ni waziri niliyekaa muda mrefu kuliko waziri mwingine, kwa hiyo bado rekodi yangu haijavunjwa,” anasema.

Zakia anasema amefurahi sana, kwamba mwanamke amepata nafasi ya kuwa Rais, kwani walikuwa wakizungumza tu, mwanamke akipewa nafasi anaweza, lakini haiwi haiwi imekuwa na anaongeza kuwa Samia si mwanamke tu ila ni kiongozi na ana historia nzuri na watarajia makubwa kutoka kwa Rais huyo.

SIRI YA MAFANIKIO

Anasema, “siri ya mafanikio ni kujituma, hilo ndio la kwanza, lakini pia kushirikisha watu… kwa mfano nilipokuwa Wizara ya Maliasili na Utalii, nilikaa kama miaka tisa na ninajivunia mpaka sasa hivi ni waziri niliyekaa muda mrefu kuliko waziri mwingine, kwa hiyo bado rekodi yangu haijavunjwa.”

Zakia anaongeza, “la msingi ni kujituma, lakini pia kukaa pia vizuri na watu na kutambua kuwa wewe hujui kila kitu, lakini kuna watu wanajua, waulize ujifunze na kujua kwamba kujifunza kunaendelea, hakuna mwisho, pia kuwaheshimu watu; mdogo na mkubwa maana huwezi kujua utamkuta wapi tena…na pia kujituma, nidhamu ya kazi na uadilifu kazini jambo ambalo ni muhimu sana…”

MAISHA YA KUSTAAFU

Anasema, “Kustaafu ni raha, namshukuru Mungu nimestaafu na ninaendelea vizuri; sasa hivi sina presha…nafanya mazoezi yangu, nashughulika ujirani mwema hapa, nasoma na nilikuwa sipati muda hata wa kusoma, lakini sasa hivi napata muda wa kusoma, nimesoma vitabu vya Nyerere, nimesoma cha Mkapa na sasa nataka kusoma cha Rais Mwinyi… basi namshukuru Mungu na watoto wangu na wajukuu zangu…”

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/82f9f25e798c506c171718e81a701c72.jpeg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Angela Semaya

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi