loader
Dstv Habarileo  Mobile
'Mapendekezo ni spidi 30 kwa vyombo vya moto katika maeneo ya shule, makazi'

'Mapendekezo ni spidi 30 kwa vyombo vya moto katika maeneo ya shule, makazi'

*SIKU YA KIMATAIFA YA USALAMA BARABARANI

 

TANZANIA inapoteza wastani wa watu 2,000 kila mwaka kutokana na vifo vya ajali za barabarani huku karibu watu 4,000 wakipata majeraha kutokana na ajali hizo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), ajali za barabarani zinazigharimu nchi nyingi asilimia tatu ya pato lao la mwaka. Hasara inayotokana na ajali za barabarani, licha ya kuwa kubwa kwa mujibu wa takwimu hizo, lakini pia zina taswira nyingi: kiuchumi, kifamilia, na kihisia.

Watembea kwa miguu wako katika hatari kwenye barabara za Tanzania, ambapo vifo vyao ni asilimia 26 ya vifo vya ajali na ajali zinazowahusu ni asilimia 25 ya ajali zote za barabarani.

Kuwalinda watembea kwa miguu na watumiaji wengine wa barabara ni jambo la muhimu iwapo Tanzania inahitaji kupiga hatua kulinda usalama barabarani.

Mwaka huu dunia inapoadhimisha kwa mara ya sita wiki ya Umoja wa Mataifa ya Usalama Barabarani, WHO inahimiza kuweka maeneo maalumu katika miji yetu na viunga vyake ambako kasi ya vyombo vya moto inadhibitiwa kwa kiwango cha juu zaidi.

Hatua hii ya kudhibiti mwendo wa vyombo vya moto, haitakuwa ngeni kwa Tanzania, kwani tayari madereva wanafahamu vizuia mwendo kama matuta ya barabarani, vivuko vya waenda kwa miguu na askari wa usalama barabarani.

Itakumbukwa kuwa Tanzania imekuwa ikifanya juhudi kubwa katika kuweka usalama wa watumiaji wa barabara. 

Juhudi hizo ni pamoja na kuongeza uelewa wa watumia barabara ili kila mmoja kutambua wajibu wake wa kufanya barabara ziwe salama kwa wote.

Jeshi la Polisi limekuwa likiwashirikisha wadau wengine kama wanahabari, wanasheria, wabunge na mashirika ya kijamii katika uhamasishaji na ufuatialiaji wa masuala ya usalama barabarani. 

Inatia moyo kuona kwamba sura ya 168 ya sheria ya Usalama Barabarani inafanyiwa marekebisho kuziba mianya ya inayotumiwa na wavunja sharia. Na pia tumeona juhudi za kuboresha miundombinu zikifanywa kwani miundombinu mibovu pia huchangia ajali za barabarani.

Imani uliopo ni kuwa wazo la kutenga maeneo ya mitaa yenye ukomo wa mwendokasi wa 30km/h halitakuwa mzigo kwa Tanzania. Vibao vya ukomo wa 30km/h si vigeni pia na ukomo huo wa 30km/h si wa kila barabara, yapo maeneo mahsusi yanayostahili ukomo huu, mfano, karibu na shule na kwenye mitaa ya makazi ya watu.

Kuna sababu kadhaa zinazofanya kuleta imani kuwa ukomo wa 30km/h kwamba utachangia kuwapatia usalama zaidi waenda kwa miguu wanapokuwa kwenye mitaa ya karibu na shuleni, na wanapokuwa maeneo ya nyumbani.

Mosi, ni ukweli kwamba mwendo mdogo hupunguza madhara ya ajali. Ushahidi toka sehemu mbalimbali duniani unaonesha kuwa mwendo kasi mdogo unapunguza hatari ya kupata majeraha na huokoa maisha.

Hapa Tanzania mradi wa AMEND SARSAI umeweza kupunguza ajali kwa asilimia 25. Kutokana na matokeo chanya mradi umepanuliwa kuzifikia shule 50 shule zilizo katika hatari na unapangwa kufikishwa kwenye nchi zingine tisa. 

Huko Toronto, Canada ajali zimepungua kwa asilimia 28 tangu kulipowekwa ukomo wa mwendo wa 40-30km/h tangu mwaka 2015, hatua ambayo ilipunguza ajali mbaya kwa theluthi mbili. 

Huko Colombia, jiji la Bogota limeweka viunga vya 30km/h kwenye mpango wake wa udhibiti wa mwendo na kufanikiwa kupunguza vifo kwa asilimia 32.

Pia utafiti kutoka London, Uingereza ulibaini kuwa spidi ndogo ya 30km/h ilipunguza vifo vya ajali kwa asilimia 42. Tafiti kwingineko zinahitimisha kuwa kwa kupunguza mwendo kutoka 50 hadi 49, kwa mfano, kunaleta punguzo la asilimia 6 la vifo vinavyotokana na ajalli kwenye barabara za mijini.

WHO imebaini kuwa ongezeko la spidi 1km/h linaongeza kwa asilimia tatu hatari ya kupata ajali na asilimia nne hadi tano ya kutokea kifo kitokanacho na ajali.

Kwa mujibu wa tafiti hizi,  spidi inapozidi 30km/h watembea kwa mguu wanakuwa kwenye hatari zaidi ya kifo kutokana na ajali. Madereva wanapoendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi sana uwezo wao wa kuona kinachoendelea kulia na kushoto hupungua.

Pili, watu hawapendi mwendo mkubwa maeneo wanayoishi. Mara zote watu wanasema wanapenda vyombo vya moto viende taratibu maeneo wanakoishi. 

Kwa miaka mingi tafiti duniani kote zimeonesha kuwa watu wengi wanakubali kuwa 30km/h ni mwendo sahihi kwa barabara zinazopita kwenye makazi ya watu. Kimsingi mwendo wa taratibu unaweza hata kupunguza mrundikano wa magari barabarani.

Utafiti wa hivi karibuni kupitia YouGov kwenye nchi 11 umebaini kuwa asilimia 74 ya watu wanaunga mkono kuzuia vyombo vya moto kuendeshwa kwa kasi karibu na shule, ili kuruhusu watoto kutembea ama kupanda baisikeli kwenda shuleni.

Pia zipo faida kubwa kiafya kutokana na mwendo wa taratibu barabarani, ikiwamo kuruhusu watu kutembea ama kuendesha baisikeli. Watu wasio na wasiwasi wa kupata ajali wataweza kuongea wawapo mtaani na hivyo kujenga jamii inayostawi. 

Mwendo wa taratibu barabarani unaondoa hatari barabarani, unapunguza kelele na kuimarisha muungano wa jamii.

Tatu, kuwa na mitaa ambako mwendo taratibu unahimzwa inawezekana kwenye nchi maskini na tajiri. Pamoja na ukweli kuwa hadi sasa ni nchi zenye kipato kikuwa ndizo zimeanza kutekeleza mitaa ya mwendo wa taratibu, mitaa hi inawezakana kwa nchi yoyote bila kujali kiwango cha maendeleo yake kiuchumi. 

Ukomo wa 30km/h umewekwa kwa mafanikio kwenye vitongoji barani Afrika, Amerika ya kaskazini, Asia, Ulaya, Marekani ya kusini na Australasia.

Mafanikio yake yalianza kwa kuzingatia kwanza maeneo ya shule, kwa mfano mradi wa AMEND nchini Tanzania, ambao ulishinda tuzo ya Ross ya Miji Salama. Pia hivi karibuni Zambia imeanzisha mpango wa spidi ndogo kwenye maeneo ya shule na yenye watembea kwa miguu wengi.

Nne, mitaa ya mwendo wa taratibu inapunguza foleni barabarani. Mwendo wa taratibu unasaidia kupunguza misururu ya magari na kuweka mazingira bora kiafya barabarani kwa kila mtu kufurahia. Halikadhalika inaboresha maisha ya madereva. 

Barabara zikiwa salama watu wa mijini hawatahitaji kutumia magari wanapoenda karibu, hivyo kupunguza foleni za magari na uzalishaji wa hewa ukaa. 

Uchafuzi wa hewa unawaathiri watumiaji wote wa barabara, lakini wale wanaofanya kazi ya udereva wanaathirika zaidi kwa kuwa hukaa barabarani muda mrefu.

Tano, ukomo wa 30km/h unatekelezeka kwa unafuu. Mwendo kasi wa 30km/h unapendekezwa kwa kuwa ndio spidi ya juu kabisa ambayo inaweza kuwa salama mahali ambapo magari na vyombo vya moto barabarani wanapochanganyika watumiaji wa barabara wasio na ulinzi wowote. 

Pia kiwango hiki kinawezesha watu kuweza kuchagua kutembea kwa mguu, kupanda baiskeli ama kutembea wakitazama vitu madukani.

Kimsingi barabara zapaswa kubuniwa katika namna ambayo inayaongoza magari kuwa katika mwendo mdogo. Zipo mbinu nyingi za kufanya hivyo, zikiwemo alama za barabarani kuonesha kikomo cha mwendo, matuta na mbinu nyingine kadha wa kadhaa.

 

Mbinu hizi ni za gharama nafuu na, zina faida kubwa katika kuongeza hata mwonekano wa mitaa yetu kwa mfano kuwezesha upandaji miti or vyungu vya maua, kuweka alama za njia za waenda kwa miguu. 

Ufuatiliaji kisheria utahusu tu wale wanaokiuka kwa makusudi na jambo la rufaa na si kigezo cha awali cha kuweka mazingira ya mwendo wa taratibu.

 

Ni wakati wa kuchukua hatua. Mwendo kasi wa 30km/h si wazo geni hapa Tanzania. Vibao vya ukomo huu wa mwendo vinaonekana maeneo kadhaa kwenye barabara na mitaa ya Tanzania. 

Hata hivyo ukomo wa mwendo unapaswa kuakisi matumizi ya barabara au mtaa husika. Ukomo huo wa 30km/h unapendekezwa karibu na shule, makazi na mitaa wanakopita watembea kwa miguu wengi kutokana na faida za lukuki kama ilivyokwisha elezwa hapa swali.

 Kwa muktadha wa miji yetu, barabara zinazopita maeneo hayo ziwekewe matuta ili kupunguza mwendo wa vyombo vya moto na jamii inapaswa kuelimishwa kwa nguvu zaidi hatari ya mwendo kasi barabarani.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/e12df3f83c844a0d78491241787816aa.jpg

MISITU ni mkusanyiko wa uoto unaojumuisha ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi