loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mchango wa NHC katika mpango  wa serikali kuhamia Dodoma

Mchango wa NHC katika mpango wa serikali kuhamia Dodoma

MIONGONI mwa changamoto ambazo serikali ilikumbana nazo katika utekelezaji wa uamuzi wa kuhamia Dodoma ni uhaba wa majengo kwa ajili ya ofisi na nyumba za watumishi wa umma. Lakini Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lilisimama kidete na kuwa bega kwa bega na serikali katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya ujenzi.

Miradi mikubwa iliyofanywa na NHC ni pamoja na ujenzi wa majengo manne ya wizara katika eneo la mji wa serikali la Mtumba, Dodoma kwa gharama ya shilingi bilioni 3.99. Wizara hizo ni Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Fedha na Mipango, Viwanda na Biashara na Wizara ya Nishati.

Licha ya ujenzi wa majengo hayo muhimu kwa shughuli za serikali, shirika hilo pia limejenga jengo la makao makuu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) jijini Dodoma kwa gharama ya shilingi bilioni 7.7.

Meneja Habari na Mawasiliano wa NHC, Muungano Saguya, anasema kufikia mwezi Juni 2021 shirika hilo litakuwa limekamilisha mradi wa ujenzi wa nyumba 300 katika eneo la Iyumbu, wilayani Chamwino na kutoa fursa kwa watumishi wa umma na wananchi wengine kuzinunua.

Saguya anasema utekelezaji wa mradi huo utafanyika kwa awamu tatu ukilenga kukamilisha nyumba za kuishi 1,000 katika makao makuu ya nchi.

Awamu ya kwanza ya mradi huo unahusisha nyumba 100 Chamwino pamoja na majengo ya huduma na shule kwa gharama ya Sh bilioni 14.4.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uhandisi na Ujenzi wa NHC, Haikameni Mlekio, watu wanaweza kuomba mikopo kupitia Benki ya Azania ili kununua nyumba hizo 300. Anasema nyumba nyingine 100 zimejengwa kwa ajili ya kupangisha.

Mlekio anasema awamu ya pili ya mradi huo wa Dodoma utahusisha ujenzi wa nyumba 325 na majengo sita ya huduma, wakati nyumba 275 zitajengwa katika awamu ya mwisho.

Licha ya ujenzi wa miradi mikubwa ya shirika, NHC ambayo inamiliki leseni ya daraja la kwanza la ukandarasi, pia hupokea kandarasi za nje.

Miradi mingine inayotekelezwa na shirika hilo la nyumba, kama mkandarasi, ni pamoja na ujenzi wa machinjio ya kisasa ya Vingunguti jijini Dar es Salaam unaogharimu shilingi bilioni 12.49 na ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi kwa gharama ya shilingi bilioni 2.74. Shirika hilo pia linajenga makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe kwa shilingi bilioni 2.74.

Katika kusaidiana na serikali kuondoa tatizo la makazi na ofisi za watumishi wa umma kwenye taasisi mbalimbali, NHC imesanifu na kujenga majengo 44 ya Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na kukarabati shule kongwe mbalimbali nchini, chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Hivi sasa NHC inaendelea na ujenzi wa ofisi ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TDMA) kanda ya kati katika eneo la Swaswa jijini Dodoma. Kwa mujibu wa Saguya, ujenzi wa jengo hilo la ghorofa mbili ulioanza Mei 6 mwaka jana unaendelea kwa kasi nzuri na unatarajiwa kukabidhiwa mwezi Juni mwaka huu.

NHC imeshiriki pia katika ujenzi wa nyumba za wafanyakazi katika Halmashauri za Busokelo (Mbeya), Mlele (Katavi), Momba (Songwe), Muheza (Tanga) na Chato (Geita).

Meneja huyo ametaja miradi mingine iliyotekelezwa na NHC katika kipindi hiki kuwa ni ujenzi wa jengo la Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere (Musoma) na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere eneo la Kwangwa katika Manispaa ya Musoma. Hii ni hospitali iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1975 na ujenzi wake ulisimama hadi mwaka 2019 NHC ilipopewa Kandarasi ya kuumalizia ujenzi wake.

Miradi mingine ni jengo la makao makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam, jengo la Chuo Kikuu cha Ardhi na ujenzi wa shule ya watoto wenye mahitaji maalumu ya Mbuye mkoani Geita.

Pamoja na miradi hiyo, NHC vilevile inaendelea kutekeleza miradi ya uendelezaji miji ya pembezoni (satellite towns) katika maeneo ambayo yanamilikiwa na shirika hilo, ambayo ni Luguruni (Ubungo), eneo lenye ekari 156.53; Uvumba (Kigamboni), ekari 202 na Kawe (Kinondoni), ekari 267.71; Burka/Matevesi (Arusha jiji), ekari 579.2) na eneo la USA River (Meru), ekari 296).

NHC inaendelea kupangisha nyumba hizo na limepanga kuuza nyingine ili kuongeza kipato cha shirika.

 

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/028c96fb45f128302dcc95e3ea9ce9ce.jpg

MISITU ni mkusanyiko wa uoto unaojumuisha ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi