loader
MARTHA KOOME Aweka historia kuwa Jaji Mkuu wa Kwanza Mwanamke

MARTHA KOOME Aweka historia kuwa Jaji Mkuu wa Kwanza Mwanamke

JAJI Martha Koome ni Mwanasheria na Mtetezi wa Haki za Binadamu, aliyeandika historia ya kuwa Jaji Mkuu mwanamke wa Jamhuri ya Kenya.

Wadhifa huo ameupata Mei 21, mwaka huu na kuweka alama ya kuwa Jaji Mkuu mwanamke wa kwanza wa nchi hiyo. Koome ana uzoefu wa miaka 33 katika taaluma ya Sheria.

Jaji Koome alizaliwa mwaka 1960, katika kijiji cha Kithiu, kaunti ya Meru. Ana Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na Shahada ya Pili ya Sheria ya Kimataifa ya Umma kutoka katika Chuo Kikuu cha London.

Baada ya kuhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi 1986, Jaji Koome alijiunga katika Shule ya Sheria cha Kenya mwaka uliofuata. Alihitimu Shahada ya Pili ya Sheria ya Kimataifa ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha London mwaka 2010.

Jaji Koome alianza hatua kwa hatua katika fani yake hiyo ya Sheria, akianza kama mshirika katika sheria katika kampuni ya mawakili ya Mathenge and Muchemi na alisajiliwa pia kama Wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya mwaka 1986.

Alifungua kampuni yake binafsi ya Sheria baada ya kuondoka kampuni ya Sheria ya Mathenge na Muchemi na kuwa patna katika nafasi ya meneja mpaka 2003. Alichaguliwa kuwa mwanachama wa Baraza la Chama cha Wanasheria Kenya kati ya mwaka 1993 hadi 1996.

Wakati wa uongozi wake katika Jumuiya ya Wanasheria wa Kenya, alichukua jukumu la kuongoza mageuzi ya Katiba na Sheria na alikuwa mjumbe kwenye mchakati wa marekebisho ya katiba yaliyofanyika miaka ya 2000 na kutoka rasimu ya katiba iliyojulikana kama Bomas Kenya na alisimamia eneo la Muswada wa Haki

Alishawahi kuwa mweka hazina wa Jumuiya ya Wanasheria wa Afrika Mashariki kati ya mwaka 1994 na 1996. Vile vile aliwahi kuwa Mwenyekiti wa FIDA, moja ya taasisi kubwa ya haki za binadamu nchini humo.

Jaji Mkuu huyo wa kwanza mwanamke amejitanabaisha kuwa mtetezi wa Haki za Binadamu na Jinsia. Ni mmoja wa wanasheria walioshiriki kikamilifu kufutwa kwa kifungu 2A cha Katiba na Uhuru wa Mahakama.

Ni Mtaalamu wa Sheria za Masuala ya Familia na anavutiwa na ustawi wa watoto. Alikuwa mshindi wa pili katika Shirikisho la Kimataifa la Umoja wa Mataifa la mwaka 2020.

Mwaka 1995 alichaguliwa katika mkutano wa wakuu wa nchi wa Umoja wa Afrika, kuwa Kamisha katika Kamati ya Afrika ya Haki na Ustawi wa Watoto.

Vile vile alishawahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la kikosi kazi maalum cha Utawala Sheria katika Masuala ya Watoto na alisaidia mapitio ya Sheria ya Watoto.

Kazi ya Kimahakama katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa

Jaji Koome alichaguliwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa mwaka Januari 2012 na kufanya kwa miaka nane.

Mwaka huo huo alichaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa, alichaguliwa kama Mwenyekiti wa Chama cha Mahakimu na Majaji Kenya.

Mwaka 2016 alikuwa miongoni mwa wanawake 13 waliopendekezwa na Tume ya Huduma ya Mahakama kwa ajili ya nafasi ya Naibu Jaji Mkuu, ambayo baadaye ilichukuliwa na Jaji Philomena Mwilu.

Koome alikuwa kati ya wagombea walioomba kuziba nafasi ya David Maraga aliyestaafu Januari 2021 na alishiriki usaili wa wazi Aprili 14, 2021.

Jaji huyo wakati wa usaili alihojiwa kuhusiana na maamuzi mbalimbali ya kimahakama aliyowahi kufanya na kusema mengine alipaswa kutii maagizo ya Rais wa Mahakama ya Rufani ikiwa ni pamoja na kuokoa mgogoro wa kikatiba.

Katika uasili wake alieleza pia maisha magumu aliyopitia wakati akikua Meru, katika eneo la kijijini lililopo mashariki mwa Kenya akitokea familia ya baba mwenye wake wengi na alizaliwa mwaka 1960, miaka mitatu kabla ya kukoma kwa utawala wa kikoloni.

“Mimi ni mwanakijiji halisi. Wazazi wangu ni wakulima na tulikuwa watoto 18 waliotokana na mama wawili. Kwa hiyo kwetu sotea hasa wasichana, tulipitia changamoto nyingi,” alisema Jaji Koome.

Vile vile amepitia vihunzi vingi hadi kufikia wadhifa huo wa Jaji Mkuu.

Wakati wote wa usaili Jaji Koome alikuwa mtulivu, mwenye kujiamini na kujibu kwa umakini kwa saa nne alizohojiwa akieleza mengi aliyoyasimamia ikiwa ni pamoja na kutetea haki za watoto na jinsia pamoja na mchango wake katika kuandaa Katiba ya Kenya ya Mwaka 2010.

Jaji Koome alizungumza kwa kujivunia jinsi katiba sasa inavyokabiliana na ubaguzi wa kijinsia tofauti ya awali ambayo ilikuwa ‘ikibagua kabisa wanawake.”

Mwisho wa usaili, Tume ya Huduma za Mahakama ilimteuwa Jaji Koome na kumfanya kuwa Jaji Mkuu wa Kwanza Mwanamke, Jaji Mkuu wa 15 na Jaji Mkuu wa tatu baada ya Katika ya mwaka 2010.

Jina la Jaji Koome ilipelekwa kwa Rais, ambaye alilipeleka bungeni kwa ajili ya uhakiki na kupitishwa kabla ya uteuzi rasmi.

Kamati ya Bunge ya Mahakama na Masuala ya Sheria ya Bunge ilifanya uhakiki Mei 13 na kupendekeza bunge zima limpitishe mteule huyo. Kisha ripoti ya kamati iliwasilishwa Mei 19 kwa majadiliano. Bunge zima lilipiga kura kumpitisha mteule huyo Mei 19, mwaka huu na kufanikisha mwanamama huyo kuchaguliwa kuwa Jaji Mkuu.

Ndani ya saa chache, Bunge lilithibitisha kura na Rais Uhuru Kenyatta alimchagua Koome kuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Kenya.

Alikula kiapo cha kuwa Jaji Mkuu, Ikulu, Nairobi Mei 21, mwaka huu na kuandika historia ya kuwa Jaji Mkuu wa Kwanza Mwanamke nchini humo.

Jaji Koome ameteuliwa kukiwa na majukumu kadhaa ambayo Wakenya wanatazamia kuona akiyasimamiwa ikiwa ni pamoja na kulinda uhuru wa mahakama ambao sasa umeonekana kutishiwa kufuatia uamuzi wa majaji kwamba mchakato wa kuirekebisha katiba kupitia Jopo la Maridhiano(BBI) ulikiuka Sheria na ni kinyume na katiba .

Lakini kumekuwa na hofu kwamba uhuru wa idara ya mahakama utakuwa hatarini endapo ofisi nyingine ya kudhibiti shughuli za mahakama itaundwa kama ilivyopendekezwa.

Vile vile katika masuala ya kisiasa, Koome atatakiwa kuwa mstaarabu na makini kusimamia masuala hayo kwani itakapotokea kesi kubwa inaweza kufikishwa mbele ya mahakama ya juu zaidi ambayo yeye ndiye rais wa korti hiyo.

Familia

Jaji Koome ni mke wa Koome Kiragu na mama wa watoto watatu wakubwa na mzoezi wa taaluma ya sheria kwa miongo mitatu sasa tangu alipohitimu Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi mwaka 1986.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/06bd440e019e63be38dadba87ec9cc5b.jpeg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi