loader
Dstv Habarileo  Mobile
Bandari ya Tanga ilivyojipanga  kudhibiti udanganyifu katika mizigo

Bandari ya Tanga ilivyojipanga kudhibiti udanganyifu katika mizigo

WAFANYABIASHARA wanaopitishia mizigo yao bandarini wengi kwa kawaida ni waaminifu. Kwamba kile wanachosema na kuonesha kwenye nyaraka, ndicho kilicho kwenye makontena yao.

Hata hivyo, wapo ambao ni wadanganyifu kuhusu kile wanachokipitisha. Kupitia udanganyifu huo, wafanyabiashara wanaweza kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya pesa ikiwa hakutakuwa na usimamizi madhubuti unaohusisha wataalamu mahiri na waaminifu pamoja na vifaa vya kisasa vinavyoweza kudhibiti udanganyifu.

Katika hili, Bandari ya Tanga imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa hakuna udanganyifu wowote unaoweza kufanywa na wafanyabiashara wanaopitisha mizigo yao bandarini hapo.

Njia ya kukagua na kuchunguza mizigo yote ili kung'amua kama kuna udanganyifu wowote ama la katika Bandari ya Tanga ni kwa kutumia mashine ya ung'amuzi (scanner).

Mashine hiyo ina uwezo wa kuhudumia makontena 40 kwa saa ikiwa ukaguzi unahusisha kontena na gari lake ambapo humlazimu dereva kushuka.

Mwendeshaji wa scanner katika Bandari ya Tanga, Simon Sayu anasema mashine hiyo ina uwezo wa kuhudumia makontena 100 hadi 200 kwa saa kama gari litapita moja kwa moja bila dereva kushuka. 

Hii maana yake ni kuwa ni kontena pekee linalochunguzwa na mashine badala ya gari zima ili kumkinga dereva dhidi ya mionzi ya scanner hiyo.

Kwa mujibu wa Sayu, Bandari ya Tanga imechukua hatua kadhaa kwa lengo la kudhibiti udanganyifu wa mizigo yote inayopitia hapo pamoja na kuharakisha utendaji kazi wa bandari.

Hatua ya kwanza anasema ni kuhakikisha kunakuwa na mashine zaidi ya moja ili kurahisisha utendaji wa kazi na kuzuia huduma kusimama wakati mashine moja itakapopata tatizo.

Anasema Bandari ya Tanga inazo mashine mbili za scanner ambazo ni guntry na mobile scanner ambayo ilinunuliwa na Hayati Rais John Magufuli kwa lengo la kuifanya bandari iwe na ufanisi katika utendaji wake ili kuzuia upotevu wa fedha kupitia udanganyifu wa wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.

Hatua ya pili ambayo Bandari ya Tanga imeichukuwa ni kuhakikisha kuwa ofisi ya scanner inakuwa na watu watano; watatu kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na wawili kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao kwa pamoja wanasaidia kuzuia upotevu wa mapato na udanganyifu mwingine katika mizigo.

Sayu anasema jukumu kubwa la watu wa TPA katika ofisi hiyo ni kuendesha mashine hiyo na kuingiza nyaraka mbalimbali za mizigo kwenye mfumo pamoja na watu wawili kutoka TRA ambao jukumu lao kubwa ni kutafsiri na kuichambua picha itakayotolewa na mashine hiyo baada ya kupiga picha kilichomo katika kontena.

Sayu anasema lengo la kuweka timu ya watu watano katika ofisi hiyo ni kuondoa makosa ya kibinadamu na kiufundi yanayoweza kujitokeza ikiwa mashine hiyo itakuwa katika mikono ya watu wachache.

“Ili tuweze kufanikisha shughuli yetu cha kwanza tunaanzia pale nje linapoingia gari lililobeba kontena, dereva akifika anasimama pale na kusubiri maelekezo kutoka chumba cha kuendeshea mashine akifika pale anashuka na kuja huku ili asipatwe na mionzi kisha tunatangaza mara tatu kwamba kama kuna mtu ndani ya gari atoke,” ameongeza Sayu.

Hatua hiyo inajumuisha matangazo ya sauti kubwa kuwapa angalizo watu wote waliokuwa karibu na mashine hiyo kuhusu kile kinachoenda kufanyika ili wachukue tahadhari. Pia mashine haiwezi kuwashwa ikiwa dereva hajaonekana katika mazingira salama.

Sayu anafafanua kuwa hakuna mzigo wowote katika makontena unaoingia katika mashine hiyo ukaacha kujulikana kilichomo ndani yake kutokana na ufanisi wa mashine hiyo. 

Anasema kupitia mashine hiyo, Bandari ya Tanga imefanikiwa kuzima majaribio kadhaa ya udanganyifu katika mizigo inayoelekea Zanzibar. Pia bandari imechukua hatua mbalimbali za kuwakinga madereva na watu wengine wasipatwe na mionzi hiyo hatari.

Anatolea mfano wa kisa kimoja cha mfanyabiashara aliyekuwa amebeba mchanga wenye madini lakini katika maelezo yake aliwaambia maafisa bandari kuwa amebeba mchanga wa baharini. 

Baada ya scanner kuchukua picha ikaonekana ndani kuna aina mbalimbali za mawe ya madini, wakawaita watalaamu wa madini na sheria zikafuatwa akalipa inavyostahili akaendelea na safari yake,

Kwa upande wake, Mhandisi anayeshughulikia scanner hiyo, Omari Saidi anasema ili kuhakikisha kuwa hakuna mizigo inayotoroshwa au kupita nje ya scanner, mashine hiyo imewezeshwa kuwa na ulinzi mkali kwa kufungwa kamera 18 zilizowekwa kuzunguka eneo hilo.

“Kamera hizi zinasaidia kufichua mbinu zozote ovu hususani udanganyifu unaoweza kufanywa na wafanyabiashara ambao sio waaminifu katika utendaji wa bandari ambao mwisho wa siku wanaiibia serikali mapato,” anafafanua Said.

Anasema ingawa teknolojia ya mashine hizo sio ya hali ya juu ikilinganishwa na mataifa makubwa kama Marekani na mataifa ya Ulaya, mashine hizo zinafanya kazi kwa usahihi na ufanisi wa hali ya juu kulingana na mizigo inayokuja katika bandari hiyo.

Kutokana na utendaji kazi wa kila siku, mashine hiyo kama zilivyo zingine inaweza kupata hitilafu na kutishia hali ya usalama katika upitishaji wa mizigo bandarini hapo. Katika mazingira hayo Mhandisi Said anasema hilo sio tatizo kwa bandari ya Tanga kwani kuna wataalamu wa mashine hiyo hivyo inaweza kutengenezwa kwa muda mfupi.

“Ikiwa tatizo ni kubwa ili tusiathiri shughuli za bandari na utendaji kazi wa kila siku tunalazimika kutumia mashine nyingine ambayo ni Mobile Scanner,” anasema Mhandisi Said.

Anasema kwa sasa kutokana na mobile scanner kupata hitilafu wanatumia Guntry Scanner kwa kiasi kikubwa. Hivyo ikitokea ikapata hitilafu kipindi hiki ambacho mobile haijatengenezwa wanachofanya ni kusimamisha mashine na kutatua tatizo kwa haraka.

Mkuu wa Usimamizi na Usambazaji wa Bidhaa wa Kampuni ya Vipodozi ya Tanga (TPPL), Rajab Ramesh anasema ukaguzi wa mizigo katika Bandari ya Tanga unafanywa haraka na kwa haki, wakati na kwa uwazi kiasi kwamba hauathiri shughuli za kampuni,

“Ikiwa maelezo uliyowapa yanayotambulisha mzigo wako hayaendani na kilichoonekana katika scanner hapo ndipo utapata usumbufu kwa sababui watakuchukulia sheria na mzigo wako utawekwa pembeni ili kupisha wengine wapate huduma,” anasema Ramesh. 

Ramesh anawataka wafanyabiashara wenye tabia ya kudanganya kuacha tabia hiyo kwa sababu sio tu kuwa itaathiri utendaji wa bandari bali pia itaathiri biashara ya kampuni husika kwa kujijengea hali ya kutoaminika katika jamii.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/283d3bb9e96d6763733be1809a3cd907.jpg

MISITU ni mkusanyiko wa uoto unaojumuisha ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi