loader
Dstv Habarileo  Mobile
            Ubidhaishaji wa Kiswahili kitaifa na kimataifa

           Ubidhaishaji wa Kiswahili kitaifa na kimataifa

WIKI iliyopita katika makala haya tulianza kuangalia suala zima la ubidhaishaji wa Kiswahili kitaifa na kimataiafa. Tuliona namna Kiswahili kinavyokuwa bidhaa kwa kuangalia fursa zilizopo hapa nchini na nje ya nchi.

Tukasema chakato wa ubidhaishaji wa Kiswahili unahusisha shughuli mbalimbali ambazo Watanzania wenye utaalamu wa lugha ya Kiswahili wanaweza kuzifanya. Shughuli hizo ni kama vile ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni, uandishi wa vitabu, tafsiri na ukalimani, uandishi na utangazaji wa habari, shughuli za sanaa n.k.

Katika makala ile tuliangalia namna Kiswahili kinavyoweza kubidhaishwa kupitia ufundishaji, uandishi wa bitabu, ukalimani na uandishi na utangazaji wa habari. Leo tunaendelea kuangalia maeneo mengine ya kuchangamkia katika kubishaisha Kiswahili.

Shuguli za Sanaa

Uwanja mwigine wa kukibidhaisha Kiswahili kitaifa na kimataifa ni ule wa sanaa. Hapa tunazungumzia muziki, filamu na michezo ya kuigiza. Kiswahili kimetamalaki sana katika kipindi hiki katika tasnia hii ya sanaa hapa nchini na nje ya nchi. Tasnia hii inakua kwa kasi sana miongoni mwa jamii zinazotumia Kiswahili. 

Wanamuziki, wacheza filamu na waandaaji wa michezo ya kuigiza wameona fursa hii kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Kwa kuwa jamii kubwa ya watu wa Afrika Mashariki inatumia Kiswahili, muziki, filamu na michezo ya kuigiza ya Kiswahili inapata soko kubwa hapa nchini, Afrika Mashariki na dunia nzima kwa ujumla. Washiriki wa tasnia hii wa Tanzania wana uwezo wa kuuza bidhaa zao katika nchi zote za Afrika Mashariki na dunia nzima.

Aidha, Kiswahili kimekamata soko la filamu na michezo ya kuigiza katika nchi za Bara la Asia na Ulaya. Kutokana na kuwapo kwa jamii kubwa inayotumia lugha ya Kiswahili, watu wameamua kutafsiri filamu zao na kuziweka katika lugha ya Kiswahili. Lengo ni kuwa na soko kubwa katika Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania.

Bila shaka, wafasiri na wanaoweka maneno ya Kiswahili katika filamu hizi wengi wao ni Waswahili wa Tanzania. Kazi hii ni kubwa na haiwezi kufanywa bure, kwa vyovyote kazi hii ina manufaa makubwa kwa washiriki. Kutokana na kodi na ushuru wa filamu hizi taifa nalo linanufaika na filamu na michezo hii. Hii nayo ni fursa muhimu  kwa Waswahili wote wanotumia lugha ya Kiswahili na wenye ujuzi wa kufanya kazi hii.

Wajibu wa Serikali

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawezesha ubidhaishaji huu wa Kiswahili kwa kuweka mazingira bora ya utendekaji wa shughuli za ubidhaishaji. Aidha, kupitia katika vyuo vikuu vya serikali na visivyo vya serikali wataalamu wa ukalimani, tafsiri, uandishi, utangazaji, sanaa, walimu wa Kiswahili kwa wageni n.k., wanaandaliwa na kuhitimu kila mwaka. Vilevile, serikali kupitia BAKITA inawasajili wataalamu wote wa Kiswahili waliohitimu katika vyuo vikuu.

Usajili huu unalenga kuiwezesha serikali kuwa na kanzidata ambayo itatumika pindi mahitaji ya wataalamu wa Kiswahili yatakapoletwa nchini na nchi zinazohitaji. Pia, serikali kupitia BAKITA imekuwa ikitoa kozi mbalimbali za msasa kwa walimu wa Kiswahili kwa wageni, waandishi wa habari, wasanii, wakalimani na wafasiri ili kuwajengea uwezo zaidi. Hatua nyingine iliyochukuliwa na serikali kupitia BAKITA ni kuandika kitabu cha Mwongozo wa Taifa wa Ufundishaji wa Kiswahili kwa Wageni – Hatua ya Awali, Kati na Juu.

Kitabu hiki kilizinduliwa na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye sasa ni Rais wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili yaliyofanyika Jijini Dodoma tarehe 19 Januari, 2021. Kimekusudiwa kuwa marejeo muhimu kwa walimu, waandishi wa vitabu na wadau wengine wote wa mafunzo ya Kiswahili kwa wageni.  

Wajibu wa Mtu Binafsi

Kila mtu binafsi mwenye utaalamu wa lugha ya Kiswahili ana jukumu la kutekeleza katika Ubidhaishaji wa Kiswahili Kitaifa na Kimataifa. Miongoni mwa wajibu wa mtu binafsi ni kuhakikisha kwamba anahitimu au kupata mafunzo ya taaluma zinazohusiana na Kiswahili.

Mtu binafsi anaweza kupata mafunzo na cheti cha ukalimani, tafsiri, uhariri, utangazaji, sanaa, ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni n.k. Aidha, mtu binafsi mtaalamu wa lugha ya Kiswahili anashauriwa kujisajili kwenye kanzidata ya BAKITA ili apate fursa pindi serikali itakapopata mahitaji rasmi ya wataalamu wa Kiswahili kutoka katika mataifa mengine.

Vilevile, mtu binafsi mtaalamu wa lugha ya Kiswahili anapaswa kutafuta taarifa mitandaoni kuhusu fursa za Kiswahili ndani na nje ya nchi na kutuma maombi. Wajibu mwingine wa mtaalamu wa Kiswahili ni kuandika vitabu vya Kiswahli vinavyoweza kutumika katika mitaala ya Kiswahili katika elimu ndani na nje ya nchi.

Aidha, anaweza kuandika vitabu vya taaluma mbalimbali kwa Kiswahili, vitabu vya hadithi fupi, riwaya, tamthiliya, tenzi, mashairi, hadithi za watoto n.k., na kujipatia soko la vitabu hivyo ndani na nje ya nchi. Pia, wataalamu wa Kiswahili wanaweza kujiunga na kuanzisha taasisi zao za Kiswahili kama vile za vituo vya ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni, tafsiri, ukalimani, uhariri, uandishi na utangazaji n.k.

Hitimisho

Kwa kuhitimisha, fursa zinazotokana na ubidhaishaji wa Kiswahili kitaifa na kimataifa ni nyingi. Watanzania tusibweteke na kuogopa kupambana kwa ajili ya kuzitafuta fursa hizi.

Fursa zipo lakini zinahitaji uthubutu na kuzitafuta. Haziwezi kuja na kumfikia mtu chumbani mwake akiwa anazisubiri, ni vyema kuzifuata na kuzichangamkia.

Watanzania wataalamu wa Kiswahili tunapaswa tupambane katika kukibidhaisha Kiswahili ili kitufae kama watu binafsi na kuwa na manufaa kwa taifa letu kwa ujumla kwani chimbuko la Kiswahili ni Pwani ya Afrika Mashariki, na lahaja sanifu ya Kiswahili asili yake ni Tanzania.

 

 

 

 

 

 

 

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/299ac60f61c5e3b58e13c6e6b9dc39f8.jpeg

MISITU ni mkusanyiko wa uoto unaojumuisha ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi