loader
Dstv Habarileo  Mobile
Umepata kuwasikia Wambugu?

Umepata kuwasikia Wambugu?

LEO katika mwendelezo wa makala za utamaduni, mila na desturi za makabila mbalimbali ya Tanzania, tunaangazia jamii ya Wambugu.

Wambugu ni kabila linalopatikana katika Wilaya ya Lushoto ambako wanaishi katika makundi miongoni mwa jamii ya Wasambaa. Maeneo wanakopatikana kwa wingi ni Kwemakame, Mazumbai, Kinko, Rangwi, Masare, Mavumo, Kitanga na Magamba.

Asili ya kabila hilo ni wafugaji wa Manyara au Magugu ambao wametawanyika maeneo mengi, ndani na nje ya Wilaya za Lushoto, Korogwe, Same na Bumbuli. Idadi ya Wambugu ni asilimia ndogo tu kulinganisha na Wasambaa wa Lushoto.

Kutokana na uchache wao lugha yao imekuwa inaingiliana sana na Kipare, na hivyo lugha yao hasa wanaiita Kimbugu cha ndani. Inaonekana ni lugha ngumu sana, na wenyeji wa Lushoto wanashindwa kuijua haraka.

Tofauti na makabila mengine, inasemekana kuwa Wambugu wana tabia ya asili ya kuzingatia uzazi wa mpango ili kudhibiti ongezeko la watu, na hii inaelezwa kuwa kuanzia enzi za mababu kabila hilo lilikuwa linapanga uzazi kulingana na mali za wazazi.

Kwa kuwa kila mtu alipenda kuishi katika eneo kubwa katikati ya misitu minene, hivyo Wambugu walikuwa makini katika suala la uzazi ili kuepuka kuwa na watoto wengi jambo ambalo lingeweza kuwasababishia mgogoro wa ardhi.

Hata hivyo, siku hizi watu wa kabila hilo wameacha utaratibu wa kuishi katikati ya misitu minene ingawa bado wanaendelea na utaratibu wao wa uzazi wa mpango ikilinganishwa na makabila mengine yanayowazunguka.

Historia ya Wambugu

Historia kuhusu kabila la Wambugu inaonesha kuwa kabila hilo linatokana na asili ya watu walio mchanganyiko wa Waafrika na Waasia, na kwamba walikuwa wakiishi Afrika ya Kaskazini kabla ya kuhamia Kenya na hatimaye kuja Tanzania.

Hivyo, asili ya mbali ya Wambugu ni Wakushi kutoka Mashariki ya Kati. Jamii ya Wakushi ni pamoja na Wasomali na baadhi ya Waethiopia na Waeritrea. Kwa walioko Tanzania, Wairaqw ni moja ya jamii ambayo asili yake ni Wakushi.

Miaka ya nyuma ilikuwa rahisi sana kuwatambua Wambugu kutokana na rangi yao lakini kadiri miaka inavyosonga mbele rangi yao inapotea kutokana na ndoa zenye mwingiliano wa makabila mbalimbali ya Kibantu hasa Wasambaa na Wapare.

Wambugu ni jamii yenye asili ya wafugaji wa kuhama hama na wanapenda kulisha mifugo yao katika misitu iliyopo sehemu za mwinuko.

Kabla ya kufika Tanzania, walipokuwa wanalisha mifugo yao walikuwa wanafuata mkondo wa mto wakitoka sehemu za kaskazini kuelekea upande wa kusini kwa sababu mto huo ulikuwa na maji mazuri na pia ilikuwa rahisi kupata maji ya mifugo yao.

Na hivyo, kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele ndivyo walivyokuwa wanasogea eneo la Kusini Mashariki hadi walipojikuta wakifika Kenya, na waliishi eneo la Laikipia, karibu na Mlima Kenya.

Baada ya kukaa eneo hilo kwa muda fulani walivamiwa na kabila la Masai ambao nao walipanua wigo wa ufugaji hadi eneo la Kusini.

Kwa kuwa Wamasai waliamini kuwa kila eneo linalofaa kwa kufuga ni mali yao, walianzisha vita na Wambugu ya kugombea ardhi.

Kwa sababu Wambugu ni watu wakimya na wanaopenda amani waliamua kuhama na kuelekea upande wa kusini kisha kwa kufuata safu za Milima ya Tao la Mashariki walijikuta wametokea Milima ya Pare Kusini katika Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo waliamua kuweka makao yao ya kudumu.

Baadhi ya machapisho yanaonesha kuwa kwa mara ya kwanza Wambugu waliweka makazi yao kusini mwa Pare katika eneo la Vudei na kuishi hapo kwa zaidi ya karne moja.

Kutokana na kuishi na wenyeji wao Wapare (ambao wakati huo walijulikana kama Waasu), walijikuta wakianza kuiga baadhi ya mila na desturi za Wapare.

Hata hivyo, haikuchukua muda kwa Wambugu kuamua kuhama toka katika Milima ya Upare na kwenda katika Milima ya Usambara Magharibi, eneo ambalo ndiko wanakoishi hadi sasa. Jambo moja ambalo halifahamiki hadi leo ni kwa nini Wambugu waliamua kuhama toka Pare hadi Usambara.

Lakini baadhi ya tafiti kuhusu makabila zinaonesha kwamba Wambugu walivutiwa zaidi na ukaribu wa Wasambaa na kuamua kwenda kuishi karibu nao.

Hata hivyo, zipo taarifa nyingine zinazobainisha kwamba Wambugu walihama baada ya kukosana na Wapare jambo lililosababisha izuke vita kati yao na Wapare wa Chome.

Matambiko na imani ya Wambugu

Ingawa inasemwa kwamba Wambugu walikosana na Wapare lakini hadi leo kabila hilo linaendelea kuheshimu na kutunza sehemu ya Milima ya Pare katika eneo la Vudei ambapo babu zao walizikwa kabla ya kabila hilo kuhamia kwa Wasambaa.

Tangu zamani Wambugu walipenda sana kufanya matambiko yao katika Milima ya Upare wakiamini kuwa nguvu za mababu zao ziko sehemu ya milimani.

Kwa hali hiyo, hadi leo Wambugu wana utaratibu wa kwenda kuhiji katika Milima ya Pare kwa lengo la kuwakumbuka babu zao.

Katika kabila la Wambugu vijana hufundishwa juu ya historia na chimbuko lao, na kabla kijana hajaoa ni lazima awe amekwenda katika Milima ya Pare eneo la Vudei kwa lengo la kuomba baraka na ulinzi kutoka kwa mababu.

Miaka ya nyuma Wambugu waliheshimu misitu kama kiini cha uhai wao, waliamini kwamba kitendo cha kukata miti kinasababisha Mungu akasirike na kuwanyima mvua na kukausha vyanzo vya maji.

Tabia ya kuheshimu miti ilitokana na mafundisho ya wazee wa kale yaliyoelekeza watu hao kutunza mazingira ili kuepuka laana inayotokana na nguvu isiyoonekana.

Waliamini kwamba ukataji wa miti husababisha mmomonyoko wa udongo, kimbunga, ukosefu wa mvua, nyuki na wanyama wadogo kukimbia na hivyo kusababisha baa la njaa na ukosefu wa amani kwa viumbe wa msituni.

Katika imani ya Wambugu, mababu wapo karibu na Mungu na ukitaka kufanikiwa ni lazima kuwaheshimu mababu hao ili maombi (sala) yako yaweze kumfikia Mungu.

Chakula cha asili cha Wambugu

Chakula cha asili cha Wambugu ni maziwa na mahindi, lakini pia hutegemea asali kama chakula hasa wakati wa kiangazi. Na pia asali hutumika kufanya matambiko mbalimbali kwa lengo la kufukuza mikosi, kuzuia laana na kuomba baraka kwa mababu zao.

Lakini pia asali ilitumika kutengeneza pombe ingawa siku hizi miwa imekuwa malighafi kuu kwa ajili ya kutengeneza pombe hiyo.

Pombe hiyo ya Wambugu ni maarufu pia kwa makabila jirani na Wambugu ya Wasambaa na Wapare, jambo linalofanya kuendelea kuimarishwa kwa uhusiano na kudumisha mila zinazoshabihiana.

Lugha ya Kimbugu

Lugha ya Wambugu (pia huitwa Kimaa au Kibwayo na wengine) inashabihiana na lugha za makabila yanayozungumza lugha za Gorowa, Barungi na Alawa na lugha nyingine jamii ya Kushi ambazo hutumiwa na makabila mengi yanayoishi Kusini mwa Ikweta.

Utafiti uliofanywa mwaka 2004 kuhusu lugha ya Wambugu unaonesha kwamba lugha ya kabila hilo imegawanyika katika lahaja za aina mbili.

Wambugu wanaozungumza kwa lahaja ya kawaida wanatumia Kimaa kilichochanganyika na Kibantu. Lugha hii ilijipenyeza katika kabila hilo baada ya kuishi na makabila ya Kibantu kwa miaka mingi.

Kimaa ni lugha ya Kikushi inayoshabihiana na lugha ya makabila yaliyopo Tanzania kama Wairaqw au Wambulu wanaoishi mikoa ya Arusha na Manyara.

Kundi la pili ni lile wanaotumia lahaja ya lugha fasaha ya Kimaa. Kundi hili linaonekana kuwa ndilo linalotunza na kuenzi asili licha ya kuishi na Wabantu kwa zaidi ya miaka 300. Wambugu wanaotunza lugha ya asili wanatumia lahaja sawa na lugha nyingine ya jamii ya Kikushi.

Hata hivyo, Wambugu wanaonekana kuwa wepesi na wataalamu wa lugha kwa sababu mtu mmoja anaweza kuzungumza lahaja tofauti kwa kuzingatia mtu anayezungumza naye.

Ndiyo maana imekuwa si rahisi kuwatambua Wambungu pale wanapochanganyika na wenyeji wao kwa kuwa wanazungumza Kisambaa na Kipare, ila wenyeji wao wanaweza kuwatambua kutokana na asili yao ya ukimya.

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari.

0685 666964 au bhiluka@gmail.com

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/8544ecd6350df12168690505bb274edd.jpg

MISITU ni mkusanyiko wa uoto unaojumuisha ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi