loader
Dstv Habarileo  Mobile
Tamu, chungu Ligi Daraja la Kwanza

Tamu, chungu Ligi Daraja la Kwanza

MSIMU wa 2020/2021 wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) umefikia tamati, japo kuna timu ambazo bado zinatakiwa kucheza michezo ya mtoano.

Mpaka sasa timu za Mbeya Kwanza na Geita Gold zimepanda Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2021/2022 baada ya kuongoza katika makundi yao.

BINGWA

Ligi hiyo ambayo iliendeshwa katika makundi mawili yenye timu 10 kila moja, vinara wa kila kundi walicheza mchezo wa kutafuta bingwa, na Geita akaibuka bingwa kwa kumfunga Mbeya Kwanza kwa bao 1-0.

Geita Gold licha ya kuwa bingwa pia ilitoa kocha bora ambaye ni Felix Minziro, mchezaji bora Geofrey Julius na kipa bora, John Mwanda.

Minziro ‘ Baba Isaya’ amefanikiwa kuipandisha timu ya Geita Gold  ikiwa ni  mara ya tatu kwa kocha huyo kupandisha timu kwenda Ligi Kuu, alishawahi kupandisha Singida United kwa msimu wa 2016/17, akaipandisha KMC kwa msimu wa 2017/18 na baada ya kuzipandisha timu hizo kocha huyo haendelei nazo.

Mbeya Kwanza ambao ni vinara wa Kundi A ilikuwa timu ya kwanza kupanda Ligi Kuu ikiwa imebakisha michezo minne, imeshika nafasi ya pili baada ya kufungwa katika mchezo wa fainali na Geita Gold kwa bao 1-0.

Licha ya kushika nafasi ya pili, Mbeya Kwanza inayonolewa na Steven Matata ilitoa mfungaji bora, ambaye ni Wiliam Mwampangama.

ZILIZOSHUKA SDL

Katika Kundi A timu za Boma, Mawenzi Market, Mji Njombe na Majimaji zimeshuka Daraja la Pili baada ya kufanya vibaya katika kundi lao na Kundi B ni timu za Singida United, Alliance FC, Mbao na Rhino Rangers.

KUCHEZA MTOANO FDL

Arusha FC ilicheza mchezo wa mtoano na Ndanda FC na Ndanda ilifanikiwa kubaki kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-2  na sasa Arusha FC itacheza tena mtoano na timu ya DTB kutoka Daraja la Pili kwa ajili ya kutafuta kubaki FDL. Endapo Arusha FC itashinda, basi itabaki Daraja la Kwanza, lakini ikifungwa itashuka Daraja la Pili na DTB kupanda FDL.

Fountain Gate ilifanikiwa kubaki FDL baada ya kuifunga  Lipuli FC kwa jumla ya mabao 2-1 na sasa Lipuli itapamba na Pan African kutoka Daraja la Pili na endapo itashinda itabaki FDL, lakini ikifungwa itashuka Daraja la Pili na Pan African itapanda FDL.

MCHUJO KUPANDA VPL

Licha ya kucheza mtoano wenyewe kwa wenyewe, ambapo Transit Camp iliifunga African Sports kwa penalti 5-4 baada ya kutoka sare ya 1-1, sasa  Transit Camp itacheza mchezo mwingine wa mtoano na timu inayoshika nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi Kuu (VPL).

Endapo Transit Camp itashinda katika michezo yote miwili basi itapanda ligi kuu na endapo timu ya Ligi Kuu itafungwa, itashuka Daraja la Kwanza.

Pamba ambayo  iliifunga Kengold kwa jumla ya mabao 4-3, sasa itakutana na timu ya Ligi Kuu itakayoshika nafasi ya 13.

Endapo Pamba itashinda katika michezo yote miwili, basi itapanda Ligi Kuu na endapo timu ya Ligi Kuu itafungwa itashuka Daraja la Kwanza.

WAAMUZI

Waamuzi kulalamikiwa ni jambo la kawaida kwani kila timu hupenda kushinda hata kama haina uwezo na ni mara chache sana utasikia kocha akikubali kufungwa kutokana na kuzidiwa mbinu na ufundi na wapinzani.

Hata hivyo waamuzi waliochezesha Ligi Daraja la Kwanza wamefanya vizuri na kama kulikuwa na malalamiko basi ni yale mapungufu ya kibinadamu, kwani miaka ya nyuma waamuzi kupigwa ilikuwa jambo la kawaida.

Msimu huu tukio la kupigwa kwa waamuzi lilitokea katika mchezo wa Pamba na Rhino Rangers uliochezwa Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, ambapo maafande wa Rhino Rangers walivamia uwanja na kumpiga mwamuzi  wakati mchezo ukiendelea baada ya timu yao kuwa ipo nyuma kwa mabao 2-0.

Wakati FDL ikihitimishwa, Amina Kyando aliibuka kuwa mwamuzi bora na Recpisous Dismas akiibuka mwamuzi msaidizi bora.

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi