loader
Tanzania inavyoweza kunufaika na Kiswahili kisiasa

Tanzania inavyoweza kunufaika na Kiswahili kisiasa

TANZANIA ina nafasi kubwa ya kuwa dola kiongozi Afrika endapo itaamua kutumia nafasi ya lugha ya Kiswahili kama nyenzo ya ushawishi.

Mtu anaweza kushangaa hili lakini tujiulize, tuliwezaje miaka ile ya 1960-1980 ambapo hata katika vikao vya Umoja wa Mataifa nchi nyingine zote za Afrika zilikuwa zikisubiri kusikia nini kitasemwa kutoka Tanzania kabla hazijazungumza? Huu ulikuwa ushawishi wa hali ya juu.

Mei 25, 2021 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Liberata Mulamula, aliongoza kikao cha mabalozi wa Afrika katika kusherehekea siku ya Umoja wa Afrika, akasema Kiswahili kimepitishwa rasmi kutumika kama lugha ya mawasiliano katika mikutano rasmi ya Umoja wa Afrika.

Tukumbuke pia kuwa mwaka 2019 Tanzania iliomba na kufanikiwa kufanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne ya kuendeshea mikutano ya SADC na sasa katika mikutano ya kisekta ya jumuiya hiyo.

Kiswahili ni fursa adhimu kwa serikali, wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi wa kawaida katika kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika kiuchumi, kisiasa na kijamii Afrika na duniani kwa ujumla.

Kwa nini naamini hivi? Ni kwa sababu mwaka 2013 wakati Umoja wa Afrika ukitimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1963 nchi za Afrika zilikuja na mpango wa maendeleo wa Afrika ujulikanao kama Ajenda 2063 ambayo inalenga kuliunganisha Bara la Afrika katika nyanja zote: kijamii, kisiasa, kisayansi, kiuchumi, kibiashara na kiutamaduni.

Kutokana na mpango huu mkakati wa Afrika 2063 na utumikaji wa Kiswahili kama lugha ya mawasiliano utainufaisha na kuiwezesha Tanzania kuyafikia malengo yake ya kisera.

Kwa kutazama changamoto ya lugha nyingine kama Kingereza, Kifaransa, Kireno au Kiarabu tunaona kuwa ni Kiswahili pekee ambacho kinaweza kutumika kuziunganisha nchi za Afrika na hili litainufaisha sana Tanzania kuongeza ushawishi katika uamuzi wa kisera na ya kimkakati ya Umoja wa Afrika.

Adebayo na wenzake katika kitabu chao Marginality and Crisis cha mwaka 2010 (2010:62) waliandika: Kiswahili kimetambuliwa na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) kama lugha yenye kuleta umoja katika nyanja za maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kielimu, kisayansi na kiteknolojia.

Lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha kubwa na kongwe duniani ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika uhusiano wa kidiplomasia kabla na baada ya Uhuru wa Bara letu la Afrika.

Adebayo na wenzake wanaandika: “Kihistoria, Kiswahili kimekuwa lugha ya mawasiliano kwa jamii ya mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki tangu karne ya 14. Ni lugha ambayo inazungumzwa na zaidi ya watu 120 katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.

Mbali na Tanzania Kiswahili pia kinazungumzwa Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Congo (DRC), Somalia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Msumbiji, Zambia, Malawi, Zimbabwe na Afrika Kusini.

Kidiplomasia ukuaji wa ushirikiano kati ya ukanda wa Afrika Mashariki na mashariki ya mbali pamoja na mashariki ya kati ulitegemea ukuaji wa Kiswahili. Kiswahili kimetumika kama kiungo kati ya wafanyabiashara wa nje na wa ndani.

Kilitumika pia kama lugha ya ukombozi wa Bara la Afrika. Kilitumiwa na chama cha TANU kuwaunganisha na kufanikisha ukombozi na uhuru wa Tanganyika, pia kikatumika kwenye mapinduzi Zanzibar hadi kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lugha ya Kiswahili ilitumika kama lugha ya ukombozi wa nchi za Kusini na Kaskazini mwa Afrika. Mashujaa wa FRELIMO, PAC, ANC, MPLA, POLISARIO na ZANU-PF walipokea mafunzo yao na msaada wa ukombozi kwa mchango wa Kiswahili.

Hivyo basi hatua za awali za utekelezaji wa sera ya kwanza ya mambo ya nje nchini lugha ya Kiswahili ilikuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wake, hususan kwenye eneo la ukombozi.

Kiswahili kilitumika pia kama lugha ya ukombozi katika nchi za Msumbiji, Zimbabwe na Afrika Kusini (wakati wa ubaguzi wa rangi), Uganda (wakati wa kuikomboa Uganda dhidi ya dikteta Idd Amin), Rwanda, Burundi, Afrika ya Kati na Congo (DRC).

Kiswahili pia kinatumika kama lugha ya utafiti katika vyuo vikuu mbalimbali vya Afrika, Ulaya, Asia, na Marekani. Hizi ni miongoni mwa sababu zilizofanya Sekretarieti ya Umoja wa Afrika (AU) kukichagua Kiswahili kama lugha yake rasmi ya kazi.

 

Tunapozungumzia utaifa na demokrasia leo hii katika Afrika tunapaswa kufahamu kuwa msingi wake ni lugha ya Kiswahili.

Katika kuthibitisha hili Muthwii na Kioko (2004) wanasema kwamba harakati mbalimbali zilifanyika na zinaendelea kufanyika ili kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya mawasiliano barani Afrika.

Mwaka 1958 Baraza la Pili la Waandishi na Wachoraji Weusi lilipitisha Azimio la kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya mawasiliano kwa bara zima la Afrika. Nina hakika jambo hili litatimia siku moja lakini kunahitajika juhudi za dhati na utashi.

Pendekezo kama hilo liliwasilishwa na Mawaziri wa Afrika wa Utamaduni wakati wa Mkutano wa OAU uliofanyika Port Louis, Mauritius mwaka 1986 na katika mwendelezo wa Tamasha la Kwanza la Kuhanikiza Kiswahili kama lugha ya mawasiliano ya Afrika lilofanyika Zanzibar.

Sambamba na juhudi hizo, viongozi wa nchi za Afrika walikutana Julai 2002 jijini Durban, Afrika ya Kusini na kutangaza kwa pamoja kuwa Kiswahili ni moja ya lugha rasmi za kiutendaji za Jumuiya ya Umoja wa Afrika (Sasa Umoja wa Afrika).

Nafikiri kuna haja ya kuwa na Tamasha la Kiswahili Afrika litakaloleta wataalamu wa Kiswahili kutoka nchi mbalimbali za Afrika ambalo litakuwa likifanyika hapa Tanzania kila mwaka na hivyo kupenyeza ushawishi katika sera na uamuzi unaofanywa na Umoja wa Afrika.

Ni wazi kuwa kuanzia mwanzoni mwa karne ya 21 lugha ya Kiswahili imepiga hatua kubwa katika uwanda wa diplomasia.

Hili alilosema Waziri Mulamula lilianza mwaka 2002 kwenye mkutano uliofanyika Durban, Afrika Kusini ambapo AU kwa pamoja uliazimia na kuanza kutumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano.

Ninaamini uamuzi huo umetokana na kutambua utimilifu wa lugha hii, lakini pia historia yake katika ujenzi wa amani.

Ushawishi wa Kiswahili katika majeshi ya Rwanda, Burundi, Uganda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kunaonesha jinsi ambavyo Kiswahili kinabeba ujumbe wa amani.

Zipo sababu kadhaa zinazoashiria mafanikio haya ya kukua kwa Kiswahili ikiwemo nchi ya Afrika Kusini kuanza kukitumia Kiswahili katika mitaala ya shule zake nchini humo katika ngazi mbalimbali.

Mbali na hilo, kuwepo kwa idhaa za Kiswahili za Mataifa kama Ufaransa (RFI), Marekani (VoA Kiswahili), Uingereza (BBC Kiswahili), Ujerumani (DW Kiswahili), China (CRI), Japan (Redio Japan Kiswahili) sambamba na redio ya Umoja wa Mataifa (UN) inayorusha matangazo kwa lugha ya Kiswahili ni chachu ya kukipaisha Kiswahili.

Mbali na nchi hizo na UN nchi ya Urusi ina vyuo vikuu vitatu vinavyofundisha Kiswahili. Kiswahili kinaweza kutumika kama nyenzo ya ushawishi ambayo kwa lugha ya Kingereza huitwa soft power yaani nguvu isiyo ya shuruti.

Joseph Nye ameifafanua nguvu hii isiyo na shuruti akisema (kwa tafsiri yangu); “Nguvu isiyo na shuruti ni uwezo wa kujenga ajenda au hoja katika siasa za dunia kupitia ushawishi na kuwavutia wengine kupitia nguvu ya imani ya mtu, misingi na mawazo, na si kupitia majeshi au vikwazo kiuchumi.”

Kumbe tunaweza kushawishi nchi za Afrika zote zikatumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano katika nchi zao kama tutajenga hoja imara na madhubuti na kuwashawishi kwa kuwajengea imani juu ya misingi ya kiafrika iliyoachwa na waasisi wa Umoja wa Afrika.

Tunaweza kuanzia kwa mabalozi waliopo nchini wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania. Katika hili serikali inaweza kuandaa utaratibu wa kuhakikisha mabalozi wote wa nchi za kigeni wanapatiwa mafunzo ya Kiswahili katika Chuo cha Diplomasia (CFR).

Hii ni kwa sababu CFR si chuo tu bali ni kituo chenye hadhi ya kibalozi kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya mwaka 1986 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayohusu Upendeleo na Kinga za Mabalozi kama ilivyotoholewa kutoka kwenye Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 na ule wa 1963 inayohusu Mahusiano ya Kidiplomasia na Kikonseli. Hivyo Chuo hiki ni sawa na ubalozi wowote uliopo nchini.

Mbali na hilo, tunahitaji kujenga vituo vya kufundisha lugha ya Kiswahili katika nchi mkakati kama Nigeria, Misri, Senegal, DRC na Afrika Kusini, hivi vitasaidia kueneza na kusambaza Kiswahili katika nchi hizo na jirani.

Balozi zetu zote nje zinaweza kuwekewa kiunganishi (link) maalumu kwa wageni kujifunza Kiswahili katika tovuti za balozi zetu na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda ili kuwavutia wageni kukijua Kiswahili.

Lingine la kufanyika ni kuwa na Tamasha kubwa la Kiswahili Afrika ambalo kama nilivyogusia awali litakuwa likifanyika hapa Tanzania. Hili linawezekana kwa sababu tayari AU imeazimia kujenga Kituo Kikuu cha Urithi wa Ukombozi Afrika hivyo kupitia kituo hicho tunaweza kupenyeza ushawishi kukifanya Kiswahili lugha ya Waafrika wote.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili. +255 719 258 484

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/83802d314076bbface93e3beded1eca7.jpg

NIPO nyumbani kwa Baba na Mama Chichi. ...

foto
Mwandishi: Abbas Mwalimu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi