loader
Dstv Habarileo  Mobile
Serikali yafikiria kuwapa viwanja askari wadogo

Serikali yafikiria kuwapa viwanja askari wadogo

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema wizara yake itakutana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kuangalia uwezekano kuwapa viwanja hususani kwa askari wa vyeo vidogo.

Simbachawene aliyasema hayo jana wakati akitoa maelezo ya ziada katika kipindi cha Maswali na Majibu Bungeni.

Alisema: "Ni kweli askari ya Jeshi la Polisi wanafanya kazi nzuri kwa nchi yao, lakini kulingana na vyeo vyao, ni ngumu kwa askari wa vyeo vya chini kujikomboa na kuwa na maisha mazuri baada ya kumaliza utumishi wao."

"Sisi kama wizara tunalichukua hili tujadiliane na wenzetu wa Wizara ya Ardhi kwani jambo hili ni jema na ni kweli wengine wanastaafu hawana nyumba wala kiwanja, tunalifanyia kazi tuone jinsi ya kuwapa viwanja hususani askari wasiopewa kipaumbele,” alisema Simbachawene.

Katika swali lake la msingi, Mbunge Agnesta Kaiza (Chadema) alitaka kujua ni kwa nini askari polisi wasiwekewe utaratibu wa kusamehewa kodi katika vifaa vya ujenzi na kupewa viwanja kwa bei elekezi, ili wawe na moyo wa kulitumikia taifa bila kujiingiza katika njia za udanganyifu kwa lengo la kujiandaa na maisha baada ya kustaafu.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Khamis Hamza Chilo, alisema utaratibu wa utoaji msamaha wa kodi kwa bidhaa mbalimbali vikiwemo vifaa vya ujenzi kwa askari wa Jeshi la Polisi ulikuwa unatekelezwa kupitia Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Alisema kutokana na changamoto za kimuundo na mfumo uliosababisha uvujaji wa mapato na utozaji kodi usio na usawa, serikali ilifanya marekebisho yaliyosababisha kufutwa kwa baadhi ya misamaha ya kodi ikiwemo ya vifaa vya ujenzi kwa vyombo vya ulinzi na usalama.

Chilo alisema serikali kwa kutambua kazi kubwa na nzuri katika kulitumikia taifa inayofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama likiwemo Jeshi la Polisi, ilianzisha utaratibu mwingine wa kibajeti wa kutoa nyongeza ya posho maalumu kwa kila askari ili kufidia gharama za kodi wanapofanya manunuzi ya vifaa vya ujenzi pamoja na mahitaji yao mengine.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/0e4ee22c8e0471c007c6db9ce29f8bf2.jpeg

RAIS wa Zanzibar,  Dk Hussein Mwinyi amesema wakati umefika kwa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi