loader
Dstv Habarileo  Mobile
Tanzania inavyobebwa na ubora wa viongozi wake

Tanzania inavyobebwa na ubora wa viongozi wake

MAFANIKIO ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana (2020), yanatokana na ushirikiano wa watu mbalimbali wakiwamo wanachama wake, viongozi na wananchi kutambua kazi iliyofanyika miaka iliyopita.

Mmoja wa wanachama anayetajwa kuchangia mafanikio hayo pia ni anayewawakilisha vijana katika Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC) upande wa Tanzania Bara, Mussa Mwakitinya, mzaliwa wa Kibakwe mkoani Dodoma miaka 29 iliyopota.

Mwakitinya, mhitimu wa shahada ya juu ya uzamili (masters) katika taaluma ya ununuzi na ugavi kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) cha mkoani Dodoma na shahada ya awali ya chuo hicho hicho, Dar es Salaam, anaelezwa kutumia muda wake vilivyo katika kufanikisha kampeni.

Mjasiriamali huyo msomi anayejishughulisha na shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato na aliye tayari kuajiriwa fursa ikitokea, alipita katika majimbo mbalimbali na kuongozana na wagombea wa nafasi ya ubunge katika majukwaa kuwaombea kura.

Anasema kwake hilo lilikuwa jambo la faraja kubwa kutokana na hamasa aliyokuwa akiitoa na kuiona katika kampeni hizo kiasi cha kumfanya azidi kujijenga kisiasa na kuimarisha uhusiano kati yake na wanachama wengine wa chama hicho waliopo maeneo mbalimbali ambapo kampeni hizo zilifanyika.

Mwakitinya pamoja na kwamba ni mwanasiasa kijana, anapendezwa sana na wafanyabiashara wakubwa waliowahi kuwa wanasiasa akiwamo Mohammed Dewji aliyewahi kuwa Mbunge wa Singida (CCM).

Katika uchaguzi wa mwaka jana, alijitokeza na kuwania kiti cha Ubunge katika Jimbo la Mpwapwa mkoani Dodoma lakini kura zake hazikutosha kupata nafasi kukiwakilisha chama chake katika uchaguzi huo, jambo ambalo hata hivyo anasema halijamfanya kukata tamaa.

“Ukweli hakuna ubishi, kuna faida nyingi kuwa ndani ya chama hiki (CCM), kwanza unakuwa katika nafasi nzuri za kuvuna busara nzuri kutoka kwa viongozi wake na kufahamu historia mbalimbali ya wapi tulipo na kujua wapi tunakwenda, lakini pamoja na hilo viongozi wengi wakubwa wametokana na chama hiki, hivyo kitendo cha kuwa karibu nao kinakupa walau harufu harufu ya kuja kuwa kiongozi mzuri baadae” anasema Mwakitinya.

Anasema uongozi ndani ya Taifa hili ndicho kitu anachokipenda kwa kuwa ameona changamoto zinazowakumba watu wengi katika jamii akitaka kutumia nafasi hiyo kuzitatua akiamini kuwa kwa kufanya hivyo kutazidi kuliletea taifa sifa na ustawi bora wa maisha ya kila mtu kama ambavyo ameonesha Rais Samia Suluhu Hassan muda mfupi tangu Machi mwaka huu alipoapishwa kuliongoza Taifa hili.

“Rais wetu Samia Suluhu Hassan anastahili pongezi za hali ya juu, ndani ya muda mfupi tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ameonesha ujabali wa kisiasa na kutoa ishara ya upendo, amani, mshikamano sambamba na kuwapa matumaini makubwa Watanzania, huyu ni aina ya viongozi wachache ambao unaweza kukutana nao mahali popote duniani.

“Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, Rais Samia anafanya vizuri na zaidi nawaomba Watanzania tuzidi kumuombea kwa Mungu ili amkinge kwa kila kitu na aweze kufanya kazi yake kwa amani na utulivu katika kututumikia Watanzania ambao wengi tumejawa na imani za matumini sana kwake,” anasema. 

Anasema akiwa kijana anapambana kwa kila hali katika kujenga mahusiano mazuri na vijana wenzake na kuwaelimisha katika mambo anayoyaona kuwa yana umuhimu kwa vijana hao na Taifa kwa ujumla akiamini kufanya hivyo kutawasiadia vijana wote kupita katika mstari ulionyooka ili wapate mafanikio na hamasa ya kulitumikia taifa lao.

Anasema sababu ya kufanya hivyo ni kuwaweka sawa vijana hao kupigania maslahi ya taifa lao kupitia uongozi kutokana na uwepo wa mahitaji makubwa ya vijana katika nafasi mbalimbali za uongozi hasa wakati huu ambao vijana wengi wameaminiwa na kupewa kazi.

Mwakitinya anasema hatua hiyo imekuja kama muendelezo kutoka kwa kiongozi huyo wa juu wa taifa hili kwani hata akiwa makamu wa Rais, Samia alitumia nafasi nyingi kutetea na kuwasimamia vijana na wanawake katika nyanja mbalimbali.

Anasema Serikali ina mambo mengi ya kufanya kwa ajili ya Watanzania hivyo ni vyema kukawa na ushirikiano kutoka kwa wadau kwa ajili ya kutoa usaidizi katika kutatua changamoto hizo hatua itakayosaidia kuleta ustawi wa maisha ya kila mwananchi katika jamii na hatimaye kumfanya kila mtu kuwa na tabasamu lenye ‘matumaini’ tele kwa kila mtu nchini.

Mwakitinya anaamini katika uongozi wa kuwajibika kwa wananchi, hapa anatumia fursa hii kuwapongeza wateule wa nafasi mbalimbali za uongozi wakiwemo wakuu wa mikoa, mabalozi, majaji na wengine na kuwasisitiza kuziheshimu nafasi hizo walizoaminiwa na Rais Samia na wamsaidie katika kazi.

Anasema Tanzania yenye watu zaidi ya milioni 50, angeweza kuteuliwa mtu yeyote katika nafasi hizo hivyo kitendo cha wao kuaminiwa hadi kupewa nafasi hizo kinapaswa kuwa kama deni kwao na kutumia nafasi hiyo kujituma zaidi ili kutoa matokeo chanya kama ambavyo mkuu huyo wa nchi anatarajia kutoka kwao.

Anasema kila mtu kwa nafasi yake anapaswa kwenda kusimama kikamilifu katika majukumu aliyopewa ili kumdhihirishia Rais kuwa yupo pamoja naye katika ujenzi wa Taifa hili huku wakiwatumikia wananchi kwa upendo na mshikamano kama ambavyo wameoneshwa mfano wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Wanapaswa kuepuka kujiona miungu watu, wakafanye kazi kama walivyoagizwa, wakasimame pamoja na wananchi na kuchapa kazi kama ambavyo imesisitizwa na rais wetu kuwa kazi iendelee, vinginevyo watakuwa wanamkosea kiongozi wetu” anasisitiza Mwakitinya.

Anasema, viongozi wanaotazamiwa kuleta matokeo chanya kwa jamii ni wale watakaoibeba Tanzania kizalendo, kuwajibika na kuhakikisha huduma za jamii zinaimarika kwa kutekeleza ipasavyo Ilani ya CCM iliyosababisha wawepo madarakani.

Mwito wake kwa vijana waliopewa madaraka nao ni kuibeba nchi na kutoa mrejesho kwamba, vijana wanaweza na hata ikitokea kutokana na ujana, mmoja amekengeuka, isiwe Samaki mmoja akioza ni wote, bali achambuliwe aliyeoza aondolewe na waliobaki wakaangwe tayari kwa mlo.

Anaamini mchango wa viongozi ni mkubwa kwa taifa na kwa uongozi wa Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani, ni dhahiri kazi inafanyika na kwa hakika “Kazi Inaendelea”.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/2fe92a4454d0aa26d3334bbdde88fc49.jpg

*Ni salama asilimia 99.99

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi