loader
Dstv Habarileo  Mobile
Ufugaji bundi ulivyo na manufaa lukuki kwa wakulima

Ufugaji bundi ulivyo na manufaa lukuki kwa wakulima

BUNDI ni ndege mwenye sura inayotisha kidogo kulinganisha na ndege wengine hasa kutokana na kuwa na uso mkubwa wa mviringo, macho makubwa ya mviringo na masikio makubwa.

Unaweza kusema ndege huyu ambaye hupenda kula nyama na wadudu ana kichwa mithili ya paka.

Bundi hufanya mawindo yao nyakati za usiku na kupumzika wakati wa mchana.

Kutokana na uwezo wao wa kuona usiku, bundi huwinda wanyama wadogo kama panya, mijusi, wadudu, ndege wakiwemo kweleakwelea na nzige.

Baadhi ya aina za bundi wanakula samaki hivyo huishi karibu na mito, mabwawa na maziwa ili iwe rahisi kwao kuwinda samaki kwenye kina kifupi cha maji.

Ripoti mbalimbali za utafiti wa kisayansi kuhusu maisha ya ndege zinaeleza kuwa bundi ni miongoni mwa ndege wa kale ambao wamekuwepo kwa zaidi ya miaka milioni 57 na kwamba kuna zaidi ya aina 250 za bundi, wakitofautiana tabia kutokana na mazingira wanayoishi.

Hata hivyo, inaelezwa kwamba bundi wameanza kutoweka maeneo mengi kwa sababu mbalimbali ikiwamo ya mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira. Wengine hushambuliwa na mwanadamu wakionekana kama uchuro.

Kwa mujibu wa taarifa ya watafiti wa ndege iliyotolewa na Alvarenga Herculano na Höfling Elizabeth ya mwaka 2003, baadhi ya aina za bundi tayari zimetoweka kabisa duniani.

Taarifa hiyo inaonesha kuna bundi wadogo walionekana kwa mara ya mwisho mwaka 1506 na sasa hawapo na aina nyingine maarufu kama bundi kicheko walitoweka tangu mwaka 1914.

KWA NINI BUNDI HUTOKA USIKU?

Bundi wana tabia ya kuwinda ama kutafuta chakula usiku ili kuepuka msongamano ama ushindani wa utafutaji wa chakula baina yao na ndege wengine wakiwemo mwewe na tai ambao wanakula vyakula vinavyofanana na anavyokula bundi.

 

Pia bundi wana uwezo wa kuona vizuri hasa kunapokuwa na mwanga hafifu kuliko mkali na masikio yao makubwa huwasaidia kusikia sauti ndogo ambayo binadamu hawezi kusikia.

Uwezo wao wa kusikia na kuona katika mwanga hafifu huwawezesha kushika mawindo kwa urahisi.

MSAADA KWA WAKULIMA

Katika maeneo yenye panya wengi, wadudu na ndege waharibifu wa mazao bundi wamekuwa walinzi na msaada mkubwa kwa kuwala au kuwafanya wakimbie eneo husika na kuwa msaada kwa wakulima.

Pia inaelezwa kuwa katika hali ya kawaida bundi huweza kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta chakula na hasa anapokuwa na vifaranga.

Kama chakula kinapatikana kwa shida porini na mashambani bundi hulazimika kutua kwenye makazi ya watu kwa ajili ya kuwinda panya na mijusi.

Kwa lugha nyingine, sehemu yenye bundi wengi huwa na ahueni kubwa dhidi ya wadudu na ndege wengi waharibifu.

SIFA MBAYA

Igawa bundi ana sifa nzuri na ana manufaa kwa wakulima hali imekuwa ni tofauti kwa Waafrika na hata baadhi ya maeneo ya Asia na Latin Amerika.

Katika maeneo hayo bundi anahusishwa na masuala ya uchawi, vifo na ushirikina. Ni kutokana na mtazamo hasi dhidi ya ndege huyu mwema, anapotua kwenye makazi ya watu husababisha taharuki na hofu katika jamii.

Taharuki hiyo na hofu inatokana na imani kuwa ndege huyo ana uwezo wa kutabiri kifo, maradhi au kutumika kuleta balaa ndani ya familia. Hata hivyo, hii ni dhana tu ambayo haina ushahidi wowote wa kisayansi.

Licha ya mtazamo hasi dhidi ya bundi walio nao wana jamii wakiwemo Watanzania, Kituo cha Kudhibiti Viumbe Hai Waharifu cha Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimekuja na mtazamo chanya kupitia tafiti zake zinazofanywa kuhusu bundi.

Mtafiti wa Kitengo hicho, Profesa Loth Mulungu anasema kwamba kuna aina zaidi ya 200 za bundi na wanapatikana katika mapori na maeneo ya nyika.

Pia wapo bundi wanaoishi mmoja mmoja na wengine kwa makundi na mara zote wanatafuta chakula wakiwemo panya nyakati za usiku.

 

Profesa Mulungu anasema, wanapokuwa wengi katika maeneo ya mashamba wanapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la panya waharibifu wa mazao.

Anasema baadhi ya bundi huishi kwa makundi na kuwinda kwa pamoja, hivyo ndani ya msimu mmoja kundi moja la bundi hao linaweza kula mamia ya panya wadogo.

“Tafiti zinaonesha bundi mmoja ana uwezo wa kula zaidi ya panya kumi kwa siku moja. Kwa hiyo bundi wanaweza kudhibiti panya na wadudu wengine waharibifu kirahisi na kumsaidia mkulima kupunguza matumizi ya kemikali mashambani,” anaelezea Profesa Mulungu.

Anafafanua kwamba bundi wadogo wanakula wadudu wanaoharibu mazao, hivyo shamba linapokuwa na ndege hao wengi, athari za panya na wadudu kwa mazao zinapungua kwa kiasi kikubwa.

“Ili bundi wavutiwe na kuzaana kwa wingi kwenye shamba lako, wanahitaji kutengenezewa mazingira mazuri,” anasema Profesa Mulungu.

Mazingira hayo anasema ni kama vile kujengwa viota kwa ajili ya kuishi na nguzo kwa ajili ya kusimama nyakati za usiku wanapokuwa wanawinda.

Profesa Mulungu anasema viota hivyo vinaweza kutengenezwa mithili ya masaduku na kuning’inizwa kwenye miti au nguzo. Anasema uwekezaji wa viota kwenye nguzo unafanyika pale ambapo hakuna miti ya kutosha kwenye shamba husika.

Anasema bundi anayesimama mmoja mmoja mahala tofauti nyakati za usiku na kutoa sauti yake huwa anafanya mawasiliano na wenzake kuwa yupo sehemu fulani katika uwindaji.

Akiwasilisha hotuba yake bungeni hivi karibuni kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2021/2022, Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, katika eneo la Udhibiti wa Visumbufu vya Mimea na Mazao, alisema wizara imedhibiti makundi ya nzige wa jangwani, kweleakwelea na panya.

Alisema wizara pia imefanikiwa kudhibiti makundi yote ya nzige wa jangwani waliovamia nchi yetu pamoja na nzige wachanga walioanguliwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

Profesa Mkenda anasema katika mwaka 2020, mchango wa kilimo katika Pato la Taifa (GDP) ulikuwa ni asilimia 26.9 na kwamba katika kipindi hicho, sekta ya kilimo imekua kwa asilimia 4.9 ikilinganishwa na asilimia 4.4 ya mwaka 2019.

Kinachoonekana ni kwamba ufugaji wa bundi unaweza kuwasaidia sana wakulima kupamba na panya, ndege na wadudu waharibifu mashambani. Hivyo ni wakati wa teknolojia hii ya matumizi ya bundi ikaanza kutolewa kwa wakulima na elimu kuhusu bundi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/6e4bca057133f87327d777a7be602ae1.jpg

MISITU ni mkusanyiko wa uoto unaojumuisha ...

foto
Mwandishi: John Nditi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi