loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kilimo sayansi kinavyoweza kupaisha ASDP ll  Njia sahihi……

Kilimo sayansi kinavyoweza kupaisha ASDP ll Njia sahihi……

MAENDELEO katika sekta ya kilimo ni muhimu hasa katika kukuza uchumi wa taifa na kuleta msukumo kwenye ukuaji wa sekta ya viwanda. Ukuaji wa sekta ya kilimo una umuhimu mkubwa katika kuzalisha chakula cha kutosha ili kuhakikisha uwepo wa usalama wa chakula na lishe kwa wananchi wakati wote.

Ukweli sekta ya kilimo kwa miaka ya karibuni inachangia takribani asilimia 29.1 ya pato la taifa, asilimia 65 ya ajira, asilimia 65 ya malighafi inayotumika katika sekta ya viwanda na asilimia 30 ya pato la bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.

Kutokana na nchi kuingia katika uchumi wa kati wa chini, miaka ya karibuni na hadi sasa taifa limejielekeza katika kilimo sayansi ili kuinua wakulima wadogo ambao hasa ndio msingi wa kilimo nchini.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kilimo za mwaka 2019/2020 asilimia 90 ya ardhi ya Tanzania hulimwa na wakulima wadogo. Ili kuendeleza sekta ya kilimo, serikali inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II).

Programu hiyo ina lengo la kuleta mageuzi ya sekta ya kilimo (kilimo, mifugo na uvuvi) ili kuongeza uzalishaji na tija, kufanya kilimo kiwe cha kibiashara zaidi na kuongeza pato la wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha yao, uhakika wa usalama wa chakula na lishe, na kuchangia katika pato la taifa. 

Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda ASDP II imeandaliwa kwa kuzingatia mikakati yote ya taifa: Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025; Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu (2012-2021); Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016- 2021); Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo (2015) na Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo (Tanzania Agriculture and Food Security Investment Plan – TAFSIP 2011). 

Ajenda ya Mageuzi ya Sekta ya Kilimo imezingatia kilimo sayansi katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kipaumbele na ikolojia ya kanda ya kilimo. 

 

Malengo makuu ya ASDP II ni kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo (kilimo, mifugo na uvuvi) ili kuongeza uzalishaji na tija, kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara zaidi na kuongeza pato la wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha yao, usalama wa chakula na lishe.

Mageuzi katika kilimo hayajaanza leo kwani mwaka 1972, Mwalimu Julius Nyerere akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitangaza Azimio la Iringa lililokuwa na kauli mbiu ya Siasa ni Kilimo.

Ilikuwa ni baada ya kufafanua falsafa ya maendeleo kwamba ili tuendelee tuna hitaji vitu vine; watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Tafsiri ya maneno haya ni kwamba nguvu kazi na ardhi ni muhimu katika maendeleo ya kilimo nchini. Kipindi hicho sekta ya kilimo ilikuwa inakua kwa asilimia nne, ikiajiri asilimia 75 ya Watanzania, wengi wao wakiwa ni wakulima wadogo.

Ukiangalia mwenendo wa kilimo, serikali zote zilizotangulia hadi awamu hii ya sita imejitahidi kuhamasisha kilimo kwa kuwaandaa wataalamu na kutumia wanasiasa katika majukwaa yao ili kuhimiza kilimo ambacho mpaka sasa hakijawa na mafanikio ya yanayotakiwa.

Ukisoma nyaraka zinazogusa ASDP ll unaona kwamba kuna maeneo makuu manne ya kipaumbele ambayo ni Usimamizi Endelevu wa Matumizi ya Maji na Ardhi; lengo likiwa ni kuongeza wigo wa upatikanaji wa maji na matumizi bora ya ardhi kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi.

Pili ni kuongeza tija na faida kwa lengo la kuongeza uzalishaji wenye tija hasa kwenye mazao ya kipaumbele hasa yale ya kimkakati; tatu kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuleta ushindani kwenye soko na sekta binafsi na kuhakikisha uanzishwaji wa vyama vya wakulima na mwisho kuweka mazingira wezeshi ya kuendeleza sekta ya kilimo na kuwezesha uratibu, ufuatiliaji na kufanya tathmini ya sekta ikiwa ni pamoja na kuimarisha taasisi na kuweka mazingira wezeshi ya uratibu.

Pamoja na kuwa na maelekezo ya kutosha kuhusiana na ASDP ll ukweli unabaki palepale kwamba bila kuimarisha sayansi ya kilimo ( agricultural science) kwa kuwa na rasilimali watu na vifaa vya kilimo  ni dhahiri kuwa lengo halitafikiwa na kilimo kitabaki kuwa cha kujikimu.

Wataalamu wa sayansi ya kilimo ndio hasa watakaotumika kusambaza elimu kuanzia ya kibaiolojia hadi kifizikia kwa kushawishi mabadiliko ya fikira na uchambuzi wa maeneo ya kilimo na msaada katika kukiimarisha kwa kuwapatia wananchi mitaji.

Ifahamike kuwa kilimo ni utaalamu (Sayansi) kama ilivyo udaktari au uhandisi au fani yoyote ile inayohitaji maarifa. Ndio unapokuwa na wataalamu wanaoweza kuwasaidia wananchi ambao ndio wakulima kuijua mimea na mahitaji yake kwa wakati sahihi au la wakubali kushindwa kuiweka hai na yenye tija kwa kupata mavuno hafifu.

Unapokuwa na rasilimali watu wenye maarifa wanaweza kuambukiza wahusika katika sekta kwa kutambua kama wanataka kuzalisha kwa faida ni lazima wakajifunza maarifa ya kilimo bora na cha kisasa. Maana yake ni rahisi ni kupata maarifa sahihi ya kitu gani unataka kuzalisha, mbegu gani utatumia, viuatilifu, mbolea, wadudu gani waharibfu utakabiliana nao vipi, utahifadhi vipi mazao yako baada ya kuvuna na mambo mengine mengi.

Ikizingatiwa kwamba ASDP ll inafanyika wakati wa soko huria ni vyema maarifa yakawa sahihi zaidi ili kukabiliana na tabia za soko huria katika pembejeo (kufanyiziwa vibaya kwa kupewa vitu feki) na namna ya kupata bei yenye tija kwa kuwa na mifumo ya utunzaji na uuzaji bidhaa katika kipindi ambacho kina mahitaji.

Bwana Mifugo Chamwino, Dk David Beda anasema ukikosa maarifa sahihi katika sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji utakuwa mtu wa kutangatanga tu na wala hutaona faida ya kile unachofanya.

Sayansi ya kilimo anasema Dk Beda ni pamoja na utafiti na maendeleo ya ukuzaji wa mimea na jenetikia kwa kutambua kisahihi kabisa magonjwa, sayansi ya udongo, sayansi ya udongo, mbinu za uzalishaji (kwa mfano umwagiliaji, matumizi ya mbolea) na kuboresha uzalishaji wa kilimo kwa viwango na ubora.

Kwa mfano, uteuzi wa mazao na wanyama wanyamapori vumilivu na mabadiliko ya tabia nchi, kukuza dawa mpya na teknolojia ya kuboresha mavuno.

Ndio kusema sayansi anuwai zinazohusiana kilimo na mazingira (kwa mfano sayansi ya udongo, taaluma ya hali ya hewa kwa kilimo); biolojia ya mazao ya kilimo na mifugo; nyanja kama uchumi wa kilimo na sosholojia ya vijijini; taaluma mbalimbali zilizojumuishwa katika uhandisi wa kilimo ndio zinafanya sayansi kilimo kuwa na maana katika utekelezaji wa ASDP ll.

Katika mazungumzo na Msimamizi wa Idara ya Uhaulishaji Teknolojia na Mahusiano, Dk Richard Kasuga alisema japo ASDP II haijazungumzia nadharia ya sayansi ya kilimo, kiukweli imejikita kwenye matumzi ya sayansi ya kilimo katika kuongeza uzalishaji na tija katika mnyororo wa thamani kwenye mazao, mifugo na samaki.

Anasema maarifa yaliyomo katika sayansi kilimo yakitumika inavyostahili uzalishaji utaongezeka sana. Kwa mfano kwa kutumia sayansi kilimo watu wa ugani na wadau wao watatambua aina ya udongo na mahitaji yake na pia aina ya mbegu ya zao linalostahili kuzalishwa katika eneo hilo na hivyo kuweka kila kitu katika mtiririko wake badala ya kukosa maarifa na badala ya kuweka mbolea ya kukuzia wewe unaweka mbolea ya kupandia.

Wakati wa kuweka dawa za kukinga mimea yako na ukungu wewe unaweka dawa za kuua wadudu, aina fulani ya dawa hazifai kuua magugu ukiwa umeshapanda mimea wewe utatumia tu kiua gugu chochote herbicides bila kujua ipi inafaa wakati gani.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/fc3fe4bd079f40bad26933c57f53acb7.JPG

RAIS wa Zanzibar,  Dk Hussein Mwinyi amesema wakati umefika kwa ...

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi