loader
Dstv Habarileo  Mobile
Chakula, mavazi yanayotakiwa kukabiliana na baridi msimu wa kipupwe

Chakula, mavazi yanayotakiwa kukabiliana na baridi msimu wa kipupwe

HIVI Karibuni Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa miezi ya Juni, Julai na Agosti (JJA) na kuonesha kuwepo kwa baridi kali hadi kufikia chini ya nyuzi joto sita hususan katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Songwe, Njombe na Kusini mwa Morogoro hususan Julai.

Hata hivyo maeneo ya katikati ya nchi mikoa ya Dodoma na Singida yanatarajiwa kuwa na kiwango cha chini cha joto la kawaida ambacho ni kati ya nyuzi joto 11 hadi 14 kikiambatana na vipindi vya upepo mkali.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agnes Kijazi anasema mifumo inaonesha kuwepo kwa joto la kawaida kwa ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi na chini ya kawaida kwa maeneo ya nyanda za juu kusini magharibi na maeneo ya miinuko.

Anasema vipindi vya baridi kali vinatarajiwa kujitokeza Julai hasa maeneo ya miinuko ya nyanda za juu kusini magharibi na vitakuwepo zaidi nyakati za usiku na asubuhi.

Anasema katika maeneo ya Ziwa Victoria mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Simiyu na Shinyanga, kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa cha kawaida hadi juu ya kawaida kati ya nyuzi joto 14 hadi 19.

Kuhusu Pwani ya Bahari ya Hindi, Dk. Kijazi ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, alisema mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo la kaskazini mwa mkoa wa Morogoro inatarajiwa kuwa na joto la hadi juu ya kawaida kwa nyuzi joto kati ya 18 na 23.

Anaeleza kuwa katika ukanda wa nyanda za juu kaskazini mashariki mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara kwa ujumla kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa hadi juu ya kawaida kwa nyuzi joto kati ya 10 na 17 kwenye maeneo mengi.

“...Kanda ya magharibi mikoa ya Rukwa, Tabora, Kigoma na Katavi inatarajiwa kuwa na joto la chini au kawaida hadi juu ya kawaida kwa nyuzi joyo 13 na 19 kwa maeneo mengi,” anasisitiza Dk. Kijazi.

Katika ukanda wa pwani ya kusini mikoa ya Lindi na Mtwara inatarajiwa kuwa na hali ya joto kati ya nyuzi joto 18 na 23 katika maeneo mengi ya mikoa hiyo.

Ili kukabiliana na hali ya hewa katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na maeneo ya kusini mwa Morogoro na maeneo mengine katika msimu huu wa baridi na upepo, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichalwe anasema kutokana na taarifa hiyo ya TMA, wananchi kwenye mikoa hiyo ya kusini wanapaswa kuepuka kutumia mkaa wanapokuwa ndani kwa ajili ya kujipatia joto na endapo watatumia mkaa wahakikishe madirisha yanaruhusu hewa kupita.

Anawataka kuvaa nguo zinazowawezesha kupata joto muda wote yakiwemo sueta, nguo za kubana mwili ambazo zitawapa joto, mablanketi, soksi, kula chakula bora pamoja na kufanya mazoezi.

Daktari bingwa wa magonjwa ya damu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Mbonea Yonazi, anataka watoto na wanawake kuwa makini katika kipindi hicho kwani wanaathirika zaidi kwa baridi.

Anataka watoto kuvalishwa mavazi yanayofunika mwili kwa kuwavalisha mavazi mazito na hata watoto wanaobebwa migongoni kuhakikisha wanavalishwa nguo zinazowafunika mwili mzima na kuwafunga kwa kitenge kizito.

“Lakini pia Watanzania wengi katika jamii za wakulima wamekuwa wakibeba chakula na kwenda nacho shambani huku watoto wakiwaacha bila kuwa na mavazi yaliyofunika mwili jambo ambalo ni hatari ni vema sasa kuhakikisha wanakula chakula cha moto na kuwavalisha watoto mavazi yanayowakinga na baridi,” anasema.

Anaeleza kuwa watoto wako hatarini katika kipindi hicho kwa kukabiliwa na magonjwa ya kifua, nimonia ambayo wakiipata kinga ya mwili inashuka pamoja na homa ya mapafu.

Anaeleza kuwa kwa watu wazima wanaosumbuliwa na magonjwa kama ya pumu wanatakiwa kuwa waangalifu kwani inaweza kupata shambulio huku wanawake wanatakiwa kujikinga na baridi kwa kuvaa mavazi yanayowakinga na baridi.

Anasema kutokana na maumbile pamoja na homoni wanawake wamekuwa wakipatwa na baridi kuliko wanaume na ndiyo sababu utakuwa mahali wanaume hawasikii baridi lakini wanawake wanalalamika hivyo ni vema kuwa makini.

“Lakini kwa ujumla vyakula vinavyotakiwa kutumika kwa sasa ni vya moto na vile vya mafuta na wanga kwani vinatengeneza nishati mwilini,” anasisitiza.

Dk Kijazi anasema hali ya ukavu, upepo na ubaridi inaweza kusababisha athari kwa binadamu, wanyama na mazao hivyo kuzishauri mamlaka na wadau wa sekta mbalimbali kuchukua hatua za tahadhari ikiwemo kuzingatia matumizi mazuri ya maji na kujikinga ili kupunguza athari mbaya zinazoweza kujitokeza.

Awali katika taarifa ya Dk Kijazi alieleza kuwa katika kipindi cha Juni na Agosti, 2021 vipindi vya upepo mkali wa kusi vinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. 

“Zaidi ya hapo, katika msimu wa mwaka huu, vipindi vya upepo unaovuma kutoka kusini mashariki na mashariki (Matlai) vinatarajiwa katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya mwambao wa pwani hususan Juni, 2021,” anasema.

Anasema hali hiyo inatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika Bahari ya Hindi na kusababisha vipindi vifupi vya mvua nyepesi katika maeneo machache ya visiwa vya Unguja na Pemba, pamoja na ukanda wa pwani (Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara).

Anaeleza kuwa hali ya ukavu, upepo na ubaridi inaweza kusababisha athari kwa binadamu, wanyama na mazao.

“Jamii inashauriwa kuchukua hatua za tahadhari ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi mazuri ya maji na kujikinga ili kupunguza athari mbaya zinazoweza kusababishwa na hali ya hewa inayotarajiwa,” anasema Dk Kijazi.  

Anaeleza kuwa hali ya baridi hususan maeneo yenye miinuko ya nyanda za juu Kusini Magharibi (Mikoa ya Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa na Njombe), inaweza kuleta athari kwa binadamu, wanyama, samaki pamoja na ustawi wa mazao mashambani hususani mazao ya muda mrefu kama migomba yanaweza kupata magonjwa ya fangasi na kudhoofisha ustawi wake. 

“Kutokana na hali ya joto katika Bahari ya Hindi kuwa juu ya wastani, ongezeko la tija katika shughuli za uvuvi katika kipindi cha msimu huu linatarajiwa,” anasisitiza. 

Anasema hali ya ukavu na upepo inaweza kuongeza upotevu wa maji kwa njia ya mvukizo na kuathiri upatikanaji wa maji kwa mazao, mifugo na matumizi mengine.

“Jamii inashauriwa kuchukua hatua za tahadhari ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi mazuri ya maji na kujikinga ili kupunguza athari mbaya zinazoweza kusababishwa na hali ya hewa inayotarajiwa” anasisitiza. 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/a35db483d86d7c7e561c0d7bf80c7960.jpg

MISITU ni mkusanyiko wa uoto unaojumuisha ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi