loader
Jamii inahitaji watu kwa maendeleo     

Jamii inahitaji watu kwa maendeleo     

IPO mitazamo tofauti kuhusu idadi ya watu na maendeleo. Wapo wanaoamini kuwa, watu wengi ni balaa na kikwazo kwa maendeleo, wengine wanasema, idadi kubwa ya watu ni njia kuelekea maendeleo kwani watu wanapokuwa wengi, wazalishaji nao huongezeka. Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (Prolife) Tanzania, EMIL HAGAMU anatumia vyanzo mbalimbali kueleza kwanini jamii inahitaji watu wengi. Fuatilia.

Akihitimisha taarifa iitwayo “Population Challenges and Development Goals” yaani Changamoto za Idadi ya Watu na Malengo ya Maendeleo ya mwaka 2005, Umoja wa Mataifa (UN), kupitia Idara yake ya Uchumi na Masuala ya Jamii, Kitengo cha Idadi ya Watu, ilionesha wasiwasi kuhusu mikinzano ya mienendo ya idadi ya watu katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea.

Taarifa ilisema nchi hizo zinatofautiana kimtazamo kuhusu idadi ya watu.

Mathalani, vifo vingi hasa vya watoto, vitokanavyo na uzazi na Ukimwi ni masuala yaliyotajwa kuumiza kichwa serikali katika nchi zinazoendelea wakati serikali za nchi zilizoendelea zinaumizwa kichwa na viwango vya chini vya kizazi na madhara yake.

Hii ni pamoja na idadi ya watu wanaozeeka, kupungua kwa watendaji kazi, maisha kuwa na gharama kubwa, kuongezeka kwa gharama za matibabu, kuvurugika kwa mifumo ya huduma za kijamii na kifedha kama vile elimu, mifuko ya hifadhi za jamii, pensheni, uwekezaji katika mabenki na nyumba kuhofiwa kubaki bila watu.

Mengine ni kuvurugika kwa maisha ya kifamilia, hivyo kutoweka maadili katika jamii na kushamiri kwa tabia za ubinafsi, familia kuzorota wakati idadi ya wanafamilia inasinyaa kwa kuwa na mtoto mmoja au wawili pekee, watu watashuhudia maisha ya upweke na hofu ya nguvu za kiuchumi kupungua na kuathiri shughuli za kisiasa na kiulinzi.

Kwa nchi zilizoendelea suluhisho ni mwito wa kuongeza vizazi, yaani wanawake kuzaa watoto wengi. Kwa nchi zinazoendelea suluhisho linatolewa na serikali za nchi zile ambazo idadi yao inapukutika, ambalo ni kudhibiti ukuaji wa idadi ya watu.

Novemba 1985, wakati akizungumza katika kongamano kuhusu tofauti za kizazi, Rais wa shirika moja linalojishughulisha na utafiti wa masuala ya idadi ya watu mjini Paris, Ufaransa, alionesha namna ndoa na uzao wa watoto ulivyokuwa ukiendelea kushuka katika nchi za viwanda na kutabiri kuwa, pangekuwa na matokeo mabaya kwa idadi ya watu siku zijazo.

Baada ya kuchaguliwa, Rais wa Ufaransa kati yam waka 1995 hadi 2007, Jacques Chirac, alionya; “Kama unatazama Ulaya na katika nchi nyingine, ulinganifu wa idadi ya watu unatisha. Katika hali ya idadi ya watu, Ulaya inatoweka. Miaka ishirini au zaidi kidogo baadaye nchi zetu zitakuwa tupu, hata kama tunao uwezo wa kiteknolojia tutashindwa kuitumia…”

Naye Giscard d’Estaing aliyekuwa Rais wa Ufaransa kati ya mwaka 1974 hadi 1981 alionya wazi kuwa takwimu za sensa haziridhishi, kwani jamii inayoshindwa kuzalisha kizazi kingine ni jamii inayokufa.

MWITO WA KUZAA WATOTO WENGI

Mwaka 1984 Bunge la Umoja wa Ulaya lilitoa azimio mintarafu hitaji la kuchukua hatua kuhamasisha ukuaji wa idadi ya watu barani Ulaya. 

Azimio hilo lilichukuliwa kwa kuzingatia kwamba, umaarufu wa nafasi ya Ulaya duniani unategemea idadi kubwa ya watu na kwamba idadi kubwa ya watu ni muhimu kwa maendeleo ya Ulaya na idadi kubwa ya watu itakuwa ndicho kipimo kitakachoonesha mchango utolewao na Ulaya duniani katika vizazi vijavyo.

KUGAWA MAFAO KWA FAMILIA

Baada ya miaka mingi ya kuaminishwa kwamba uzao wa watoto wengi huleta umaskini, na kwamba uzao wa mtoto mmoja au wawili ni ishara ya maendeleo, wanawake wa Ulaya waliendelea kugomea kuzaa wakitumia vidhibiti mimba, utoaji mimba na hata kufunga kizazi.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Sera za Familia inayojihusisha na masuala ya familia barani Ulaya iitwayo: Evolution of the Family in Europe 2009 ilionesha kuwa, hatua iliyofuata ni nchi za Ulaya kuamua kutoa motisha kwa familia kama njia ya kuhamasisha wanandoa kuzaa watoto wengi.

HILA KWA NCHI ZINAZOENDELEA

Jitihada zilizochukuliwa kukabiliana na kuporomoka kwa vizazi katika Bara la Ulaya hazijafaulu kuwafanya watu wazaliane sana. Hata hivyo wimbi la wahamiaji katika nchi hizo inasaidia kuziba nafasi ya kufanya bara hilo kuwa tupu.

Suala linalowasumbua kwa muda mrefu ni ‘je, watafanyaje kudhibiti ukuaji wa idadi ya watu katika nchi maskini ili zisiinuke dhidi yao’?

Tangu miaka ya 1960, bila kuweka mipango hiyo bayana, nchi za magharibi zilianza mikakati ya kudhibiti ukuaji wa idadi ya watu katika nchi maskini na zinazoendelea kwa kutumia lugha ya ‘uzazi wa mpango’ iliyohusishwa na misaada ya maendeleo.

KWANINI TUNAHITAJI WATU

Yapo mambo mengi yanayobainisha kwanini tunahitaji watu kwa maendeleo. Watu ni rasilimali pekee na kuu kwa ajili ya kuleta maendeleo, hivyo tunahitaji watu wanaoweza kufikiri na kubuni mipango ya maendeleo. Tunahitaji watu wengi kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya kilimo na mazao mengine ya baharini na misitu.

Aidha, tunahitaji watu wengi kwa ajili ya masoko ya mazao na huduma mbalimbali zinazozalishwa.

Tunahitaji watu kustawisha huduma za kijamii, kama vile aina mbalimbali za bima na mifuko ya kijamii na tunahitaji watu ili benki zetu zistawi maana zinahitaji fedha za wawekezaji ili zishamiri.

Aidha, tunahitaji watu ili kustawisha viwanda ambavyo navyo vinategemea mazao yanayozalishwa na watu na tunahitaji watu wengi kwa ajili ya ulinzi na usalama familia, jamii na nchi zetu.

Kadhalika, tunahitaji watu kwa ajili ya kukuza, kulinda na kurithisha utamaduni wetu maana watu ndio nguzo ya taifa lolote; bila watu hakuna taifa, bila watu uchumi na huduma za kijamii zinayumba na tunahitaji watu kuimarisha mifumo ya afya.

Kimsingi, tunahitaji kuwa na watu wengi ili kudhibiti magonjwa; wakati wa ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua na kuwezesha wanawake kupata elimu kupunguza vifo kwa wanawake na watoto.

Tanzania kuna msemo usemao “Ukimwelimisha mwanamke, umeelimisha taifa”. Hivyo, wanawake wapate elimu sahihi kuwakomboa dhidi ya umaskini.

Jibu kwa umaskini linapatikana katika kuheshimu hadhi ya watu maskini, si kuwaondoa kwa kutumia vidhibiti mimba, viua mimba na utoaji mimba. Wanawake wapate faraja wanapohudhuria kliniki na wanapojifungua.

Tabia za baadhi ya wakunga kuwafedhehesha na kuwadhalilisha akina mama wanapojifungua inarudisha nyuma jitihada za kukomesha vifo vya wanawake na watoto.

Wanaume na wanawake wanahitaji kuelimishwa ili wachangie kuunda sera za maendeleo ya taifa. Hii ihusishe elimu sahihi kuhusu madhara ya vidhibiti mimba na utoaji mimba.

Nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania zinahitaji elimu bora, si elimu ya ngono inayowafundishwa watoto.

Zinahitajika huduma bora na za hakika za afya katika hospitali na zahanati zetu, uhakika wa upatikanaji wa maji safi na salama kwa wote na uboreshaji wa miundombinu zikiwamo barabara nzuri, huduma za nishati ya umeme wa uhakika na gharama nafuu.

Vingine tunavyotaka vitufikishe mbele kimaendeleo ni mgawanyo mzuri wa pato la taifa ili wote tufaidi mapato yatokanayo na rasilimali za taifa na uwajibikaji wa kila mmoja katika uzalishaji.

Nchi zinazoendelea zikomeshe aina na viwango vyote vya ufisadi na kuondoa tofauti za kipato zinazowafanya wachache kutumia zaidi pato la taifa huku wengine ambao ni wengi wakilia katika umaskini. Maliasili zilizopo zinazopaswa kuwanufaisha wananchi wote na kuchangia kuondoa umaskini.

Utoroshaji wa wanyama hai, ujangiri, usafirishaji wa meno ya tembo, uhamishaji haramu wa samaki na mazao ya angani, kama ndege warukao ukomeshwe sambamba na uporaji na utoroshaji madini, ardhi na mazao ya bahari au maziwa.

China ni kati ya nchi zenye idadi kubwa ya watu, lakini imepiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na mipango madhubuti ya ulinzi wa rasilimali za nchi, uchapakazi, utii wa sheria na uadilifu.

Matumizi ya vidhibiti mimba kudhibiti ongezeko la watu hayataondoa umaskini, bali uongozi bora wa kisiasa na kiserikali unaombatana na uadilifu na umakini katika kutenda kazi.

 

 

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/ea328d197ad6080b0ccb90fc860d7128.jpg

NIPO nyumbani kwa Baba na Mama Chichi. ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi