loader
Dstv Habarileo  Mobile
Ndugulile ataka maudhui  ya elimu kwa mtandao

Ndugulile ataka maudhui ya elimu kwa mtandao

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile amewataka wadau wa elimu kutengeneza maudhui ya elimu kwa njia ya mtandao ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi na kuwasaidia kupata elimu bora.

Alitoa rai hiyo alipotembelea ofisi ya kampuni ya Shule Direct inayotengeneza maudhui kwa njia ya mtandao hasa ya elimu ya kwa wanafunzi nchini.

“Kutengeneza maudhui kimtandao yanayoakisi maisha ya Watanzania itasaidia kuifikisha elimu kwa ukaribu zaidi kwa vijana, huku ikichagiza upatikanaji wa ajira kwa kuwa kazi ya kutengeneza maudhui pia ni fursa ya kujiajiri,” alisema.

Dk Ndugulile alisema licha ya mtandao wa intaneti kufikia takribani asilimia 60 ya nchi nzima kwa kiwango cha 3G, takwimu zinaonesha ni asilimia 28 tu ya Watanzania ndio wanatumia huduma hizo kila siku.

“Pamoja na intaneti kuwapo bado kuna gharama ya vifaa na data kuweza kuitumia. Serikali ipo kwenye mchakato wa kuendelea kutandaza mkongo wa taifa katika kila kona ya Tanzania ili kuhakikisha upatikanaji wa mtandao wa intaneti nchi nzima na kisha kuuza nchi za Zambia, Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),” alisema.

Alisema wizara yake kupitia taasisi zake inaratibu mpango wa kugawa kompyuta zilizounganishwa na huduma za intaneti katika shule za sekondari kama nyenzo ya kujifunzia na kufundishia.

“Tunaangalia upya mifumo ya ada na leseni mbalimbali zinazohitajika kufikia maudhui ya mtandaoni, nimeguswa na ubunifu mnaofanywa na Shule Direct hasa huyu Ticha Kidevu, mwalimu wa kwanza wa kidijiti nchini anayetumia majukwaa ya kidijiti kuwafikia watu wengi zaidi,” alisema.

Shule Direct ni shirika lisilo la kiserikali lililoanzishwa na kusimamiwa na vijana wa Kitanzania kwa lengo la kutumia teknolojia kuwezesha upatikanaji wa nyenzo bora za kujifunzia na kufundishia kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini.

Mmoja wa wakurugenzi wa Shule Direct, Rajabu Mgeni alisema tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2013 mpaka sasa watumiaji zaidi ya milioni tatu wameshatumia majukwaa hayo ya kidijiti ambayo yanapatikana katika mifumo mbalimbali.

“Shule Direct imemtengeneza mwalimu anayefundisha mtandaoni anayejulikana kwa jina la Ticha Kidevu ambaye kwa kupitia jukwaa maalumu kwa wanafunzi wa sekondari anafundisha masomo 13 ya kidato cha kwanza hadi cha nne kwa kuzingatia mtaala wa taifa wa elimu ya sekondari,” alisema.

Alisema mbali na mafanikio hayo, kuna changamoto  zinazokwamisha azma ya Shule Direct kufikia idadi kubwa zaidi ya watoto ikiwamo gharama ya upatikanaji wa intaneti hali inayosababisha matumizi hafifu ya huduma za Shule Direct na hata huduma nyingine za elimu kwa njia ya mtandao.

“Kuna changamoto pia katika uelewa wa matumizi ya huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa baadhi ya walimu wa shule, lakini pia kuna katazo la wanafunzi kutumia simu wakiwa darasani,” alisema.

Alisema pia kuna gharama za usajili na kuhuisha leseni kwa ajili ya maudhui ya mtandaoni, matumizi ya namba maalumu kwa ajili ya huduma za simu kwa kutumia ujumbe mfupi wa maneno.

“Tunashauri uwapo wa namba maalumu zitakazopatikana bure kwa kila Mtanzania kuweza kupata huduma muhimu za kijamii zikiwamo za elimu au afya,” alisema.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/724d704c9d1094c9d7abbc7acac9309c.jpeg

MKUU wa Chuo cha Uhasibu Arusha ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi