loader
Dstv Habarileo  Mobile
Jukumu la wazazi kwa malezi ya watoto lilindwe kisheria

Jukumu la wazazi kwa malezi ya watoto lilindwe kisheria

JUNI 16 kila mwaka nchi za Afrika wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) hufanya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ikiwa ni kumbukumbu ya mamia ya watoto waliouawa katika eneo la Soweto, Afrika Kusini.

Mauaji ya watoto hao yalifanyika mwaka 1976 katika maandamano ambayo wanafunzi walikuwa wakipigania kuboreshwa kwa mfumo wa kufundishia kwenye sekta ya elimu.

Inaelezwa kwamba watu zaidi ya 20,000 walishiriki katika maandamano na watoto zaidi 176 waliuawa huku taarifa nyingine zikieleza waliouawa ni zaidi ya 700.

Kutokana na mauaji hayo nchi 47 za Afrika zilikutana na kufikia azimio la kuanzishwa kwa maadhimisho hayo mwaka 1991 kwa wakati huo chini ya Umoja wa Nchi za Afrika (OAU).

Tunapoadhimisha tukio hili ni vyema tukakumbushana wajibu wa wazazi na walezi kuzingatia umuhimu wa malezi bora kwa watoto hasa katika kuwapatia mahitaji yao muhimu ya kibinadamu ikiwemo malazi, chakula na elimu bila kusahau kuwa upendo ambao ndiyo nguzo muhimu katika malezi bora ya watoto hao.

Takwimu zilizotolewa na Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) nchini zinaonesha kuwa jumla ya makosa elfu 36,940 ya ukatili wa kingono, ubakaji na ulawiti dhidi ya watoto yameripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini katika kipindi cha miaka mitano.

Mkoa wa Kigoma unatajwa kuwa miongoni mwa mikoa 10 inayoongoza kwa ukatili wa kingono kwa watoto. Mkoa wa Arusha unaongoza kwa kushika nafasi ya kwanza katika takwimu hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa CDF, Koshuma Mtengeti, katika mahojiano na gazeti hili anasema kuwa, chanzo kikubwa cha ukatili huo sehemu kubwa ni ndugu wa karibu wa familia ambao licha ya kufanya vitendo hivyo hakuna hatua stahili za kisheria zilizochukuliwa na kesi nyingi zilizofunguliwa zimefutwa kwa madai ya kukosa ushahidi.

Anasema katika mwaka 2020, matukio 26,544 ya ukatili dhidi ya wanawake yaliripotiwa katika vituo vya polisi nchini ambapo makosa 45 tu kutoka mikoa 13 ndio yaliotolewa hukumu na mahakama.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Mkurugenzi huyo wa CDF anasema shirika lake kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) linalohusika na programu za afya ya uzazi, linaendesha kampeni maalum mashuleni kufundisha wanafunzi shule za msingi kujua haki zao katika kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia wanaofanyiwa.

Mtengeti anasema kuwa mapambano dhidi ya ukatili na unyanyasaji kijinsia kwa watoto na wanawake unahitaji njia mbalimbali za mapambano na kwamba kwa sasa shirika lake linatumia njia hiyo kutoa elimu kwa wanafunzi kujua hasa makosa yake lakini pia kutoa taarifa kwa mamlaka mabalimbali kuhusu wale wanaofanya vitendo hivyo.

“Katika hilo tumeunganisha mpango huo na madawati ya jinsia ya jeshi la polisi ambapo wanafunzi wanapaswa kuripoti matukio ya ukatili na unyanyasaji kijinsia kwa madawati hayo ili hatua zichukuliwe na kwa sasa tunafanya kazi katika wilaya ya Buhigwe na Uvinza, mkoani Kigoma, Tarime mkoani Mara, Mpwawa mkoani Dodoma na Ilala, jijini Dar es Salaam,” anasema.

Utafiti uliofanywa kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto nchini na matokeo yake kutoka mwaka 2011, ulionesha kiwango kikubwa cha ukatili dhidi ya watoto.

Utafiti huo ulionesha kuwa watoto watatu wa kike na wanne wa kiume katika watoto 10 wametendewa ukatili wa kingono mara tatu au zaidi kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Kulingana na taarifa ya utafiti wa mwaka 2011, asilimia 50 ya ukatili dhidi ya watoto hutokea nyumbani na asilimia 40 hutokea shuleni ambapo kwenye matokeo hayo imebainishwa kuwa mimba kwa wanafunzi ni sehemu ya ukatili huo kwa watoto na kukatiza masomo yao.

Kutokana na hali hiyo serikali imeandaa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto kwa lengo la kupunguza kiwango cha ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.

Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000); Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Jinsia (2005); Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008); na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (1998).

Wakati mpango huo ukitekelezwa katika ngazi mbalimbali hadi za mitaa bado jamii haijachukua hatua madhubuti kukabiliana na ukatili na unyanyasaji kijinsia.

Katika kutekeleza wajibu huo inabainishwa kuwa mzazi kwa maana ya baba na mama anao wajibu wa kwanza katika kuhakikisha watoto wanakua na kuishi katika mazingira yaliyo bora na salama.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania ya mwaka 2017, matukio ya ukatili kwa watoto hususani vitendo vya ubakaji na ulawiti, mimba za utotoni, ndoa za utotoni na ukatili wa kimwili, vimezidi kuongezeka.

Mkuu wa Dawati la Polisi la Jinsia mkoani Kigoma, Doris Sweke, anasema kuwa pamoja na serikali kutekeleza wajibu wake kwa kuweka adhabu kali kwa watuhumiwa wanaowapa wanafunzi mimba bado tatizo hilo ni kubwa.

Sweke anasema tatizo kubwa ni kwamba kesi nyingi zinafutwa na watuhumiwa kuachiwa kutokana na kukosekana ushahidi kwa wazazi kukaa pamoja na watuhumiwa na kukubaliana kuharibu Ushahidi.

“Baada ya kesi kwenda mahakamani pande tatu hukutana na kuzungumza na mwisho hukubaliana kuharibu ushahidi kwa muathirika (mwanafunzi) kukana mtuhumiwa kwamba hausiki na ujauzito huo bali muhusika amekimbia na kesi inafutwa kwa kukosa ushahidi,” anasema Doris.

Akizungumzia tatizo hilo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kigoma, Keneth Mutembei anasema kuwa ushahidi usiotia shaka ndiyo pekee unaompa nafasi hakimu kutoa hukumu dhidi ya mtuhumiwa.

“Kuna adhabu kuhusiana na kesi za ujauzito kwa wanafunzi na ubakaji zimetolewa hukumu ya kifungo cha miaka thelathini (30) na watuhumiwa kutupwa jela lakini baadaye wanakata rufaa na kuonekana ushahidi haujitoshelezi, kulingana na adhabu aliyopewa mshitakiwa, hivyo kwa hali hiyo ni lazima tujiridhishe kwamba ushahidi usio na shaka unapaswa kuwasilishwa na polisi ili adhabu itolewe,” anasema hakimu Mutembei.

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) inaonesha kuwa asilimia 20 ya watoto wenye umri kati ya miaka 10 hadi 14 hawaishi na wazazi wao au wanaishi na mzazi mmoja huku sehemu kubwa wakilelewa na bibi au shangazi zao.

UNICEF katika ripoti zake inaeleza kuwa unyanyasaji na mateso ya vipigo (mateso ya kimwili) bado ni tatizo kubwa ambapo asilimia 22 ya watoto wenye umri wa miaka 15 hadi 19 wamekumbana na mateso hayo huku asilimia 11 wakikumbana na mateso ya kingono.

Aidha taarifa mbalimbali zinabainisha kuwa kuvunjika kwa ndoa au kuvunjika kwa mahusiano ya wazazi wawili kuna mahusiano makubwa na kuacha mateso kwa watoto na idadi kubwa ya wanafunzi kukatiza masomo.

Utafiti wa pamoja wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) na ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wa mwaka 2016 unaohusu watoto wa Tanzania walio nje ya shule unaonesha kuwa watoto milioni 4.3 wenye umri wa miaka mitano hadi 17 waliacha shule na kati yao watoto milioni 2.5 hawakuwa wamesoma kabisa.

Wakati hali ikiwa hivyo, ILO katika ripoti yake ya mwaka 2014 inaonesha kuwa asilimia 41 ya watoto milioni 3.6 wenye umri wa miaka 14 hadi 17 nchini Tanzania wanafanya kazi za kutumikishwa kukiwa na mahusiano makubwa ya kukimbia nyumbani na kuanza maisha yao.

Takwimu hizo ni sehemu ya watoto milioni 152 ambao wanatumikishwa sehemu mbalimbali duniani huku Bara la Afrika likiwa na watoto milioni 72.1 walio na umri kati ya miaka mitano hadi 17 na sehemu kubwa wakifanyishwa vibarua kwenye mashamba, migodi ya madini, kazi za ndani na uchuuzi wa biashara.

Serikali ya Tanzania katika awamu zake zote, imekuwa na maendeleo makubwa kwa wanafunzi kuhudhuria shule ambapo Serikali ya Awamu ya Tano ilitekeleza sera ya elimu bila malipo na inaendelea kutekelezwa katika awamu hii ya sita.

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu yalio na kauli mbiu isemayo: Tutekeleze ajenda 2040 kwa afrika inayolinda haki za watoto, inapaswa kutekelezwa kuanzia ngazi ya familia (wazazi na walezi) katika kutoa malezi bora kwa watoto.

Ulinzi, matunzo na malezi ya mtoto bado wazazi wengi leo wanakwepa kwa kisingizio za kazi nyingi. Jukumu hili linapaswa kusimamiwa kisheria na kisera.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/4fd5c00a8ff83eaf92aa5a5aff90efa9.JPG

*Ni salama asilimia 99.99

foto
Mwandishi: Fadhili Abdallah

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi