loader
Dstv Habarileo  Mobile
Waha “Wa hapa hapa” na ugali wa rowe usioharibika

Waha “Wa hapa hapa” na ugali wa rowe usioharibika

LEO katika mwendelezo wa makala za utamaduni, mila na desturi za makabila mbalimbali ya Tanzania, tunaangazia jamii ya Waha wanaopatikana katika Mkoa wa Kigoma.

Waha huzungumza lugha ya Kiha, hapo zamani himaya yao kiutawala iliitwa Buha ambayo ilijumuisha mipaka yote ya eneo la Mkoa wa Kigoma.

Nyumba halisi ya Waha iitwayo Ngondano kwa kawaida ni ndogo na wakati mwingine hubebeka. Kabla ya kuezekwa nyuma ya Waha hufanana na bakuli kubwa lililofunikizwa. Uezekaji wa Ngondano huanzia chini kwenda juu na hufanywa kwa uangalifu sana.

Waha kama jamii nyingi za ukanda wa joto wa Afrika, hutumia muda mdogo ndani ya nyumba. Hii hutokana na namna ya maisha yao ya kila siku na hali ya hewa ambayo huwafanya kuwa nje muda mwingi.

Asili ya kabila la Waha

Waha ni miongoni mwa makabila ambayo yana historia kubwa sana tangu walipofika katika ardhi hiyo.

Waha (Abhaha katika wingi na katika umoja Umuha) na Warundi ni moja ya makabila makubwa yaliyoathiriwa na mipaka ya kikoloni. Kiasi cha asilimia 7.5 ya jamii hii huishi Tanzania katika Mkoa wa Kigoma na hujulikana kama Waha na sehemu iliyobaki wanaishi Burundi na huko wanaitwa Warundi.

Kwa mujibu wa masimulizi kutoka kwa baadhi ya wakazi wa Kigoma na baadhi wanahistoria wanakubaliana kuwa, kipindi Waha wanafika maeneo ya Afrika Mashariki hawakujulikana kama Waha kama tuwajuavyo leo.

Kwa Tanzania, historia ya Waha ilianzia katika kijiji kiitwacho Buha kilichopo Heru, hapo ndipo Waha walipofikia baada ya kutoka maeneo ya Burundi, Rwanda na Congo.

Asili ya Waha ni watu kutoka Burundi, Rwanda na Congo, kama ilivyo kwa Wamanyema ambao asili yao ni Sudan na Congo.

Waha ni moja ya makabila kutoka Wabantu wa Mashariki. Walifika maeneo hayo hata kabla ya miaka ya 600 yaani kabla ya Wamanyema.

Na kipindi Wabantu hawa wanakuja maeneo ya Afrika Mashariki, hawakuja wakiwa na kundi moja. Bali walikuja kwa mtindo wa Koo zilizokuwa na majina yake kadri walivyopenda.

Na kila ukoo ulikuwa na jina lake. Ukoo au koo zilipokuwa hapo zilipata kumiliki ardhi na kuanzisha shughuli mbalimbali za uzalishaji mali. Na cha msingi ni kwamba watu hao walifanikiwa kutaja majina ya maeneo waliyokaa kutoka na mazingira yake.

Kwa mfano kuna ule ukoo uliokaa sehemu zenye udongo (Bayungu) walijiita Wayungu na wale waliokaa sehemu za mwinuko (Heru) walijiita Wanyaheru au Waheru.

Lakini baadaye koo hizo ziliungana na kuishi sehemu moja na kutawaliwa na chifu (Mwami) mmoja. Na hapo ndipo watu hao walipoanza kupata jina moja lililowatambulisha kwa wageni.

Asili ya jina la Waha

Ilikuwaje wakaitwa Waha? Hii ndiyo mitazamo inayosimulia asili ya neno Waha au ‘Ha’.

Ifahamike kuwa asilimia kubwa ya makabila mengi yaliyopo hapa Afrika yalipata majina kulingana na wageni walivyoelewa au walivyoona. 

Na kuna makabila yalipata majina kutokana na namna wanavyopigana, yapo makabila yaliyopata majina namna wanavyopiga kelele na wengine walipewa majina kulingana na lugha yao au matamshi yao.

Kwa upande wa kabila la Waha ambao wengi tunafahamu kuwa wanapatikana katika Mkoa wa Kigoma, kwanza, wapo wanaodai kuwa asili ya neno Waha ni pale wageni walipofika katika ardhi ya Kigoma na kuwauliza watu hao kuwa “ninyi ni wakina nani?” na ndipo watu hao walipojibu “turi abhaha” wakimaanisha “sisi ni wa hapa hapa”.

Pili, kuna wanaodai kuwa wageni walipokuja na kukuta ufalme wa Buha umekuwa na ulikuwa na watu wengi, walimuuliza mfalme wao kuwa “hawa ni wakina nani?” na ndipo mfalme wa Buha alipojibu kuwa “N’abhaha” akimaanisha kuwa “hawa ni wenyeji wa hapa hapa”.

Kwa upande mwingine, historia inafafanua kuwa, Watusi walikuwa watawala wa kabila la Waha. Na kuna uhusiano mkubwa sana kati ya Watusi na Waha. Na hivyo hata neno Waha bado lilionekana kuhusiana na Watusi.

Kwa Watusi neno Abaha lina maana ya mtu yeyote “anaowapa ardhi” na kwa Watusi aliyekuwa akitoa ardhi alifahamika kwa jina la Mteko.

Na Mteko alikuwa akitoa ardhi kwa Watusi, walifahamika kwa jina moja la Uwaha. Na waliolima shamba moja na Mteko walijiita “Abhaha” na hata kuna baadhi ya Watusi hujiita “Waha” na ndiyo maana hata walivyotawala walijiita hivyo na wageni walijua habari hizo. 

Waha na mfumo wao wa utawala

Mfumo maarufu uliotumika kutawala katika jamii ya Waha ilikuwa wa Ukoo. Koo zilizoishi katika eneo moja zilipaswa kuchagua ukoo mmoja na kuusimika kuwa ukoo wa utawala wao, hivyo mtawala alitokea katika ukoo huo.

Koo tawala ziliitwa kwa jina moja la Wateko katika wingi na katika umoja Umteko. Mfano mmojawapo wa koo hizi za utawala ulikuwa ukoo wa Wajiji uliotawala katika eneo la Nkalinzi au Kalinzi ya leo ikianzia sehemu za Mukigo.

Ili Mteko/Wateko aweze kutawala alipaswa kuwa na sifa mbalimbali kama; uwezo wa kutoa tiba, kuleta mvua, uwezo wa kuongoza watu kwa hekima, uwezo katika shughuli za ulinzi na usalama, uwezo wa kuleta neema miongoni mwa jamii yao na kulinda ardhi n.k.

Mfano wa pili wa ukoo wa Wateko ulikuwa ukoo wa Wakimbil wa Manyovu-Ibhugalama (Kibila), ukoo huu ndio ulikuwa ukiongoza katika sehemu hizo kwani tunaona kwamba hata wakati mfumo wa utawala wa Wami ukoo huu na maeneo yake ndiyo yaliyochukuliwa kuwa makao makuu ya viongozi (umtwale Munini/ watwale) na katika kipindi cha matambiko inasemekana shughuli zilikuwa hazifanyiki hadi ukoo wao umehudhuria.

Hivyo, koo za Waha zimedumu na kuishi kwa miaka mingi huku baadhi ya koo zikiwa ndio watawala (Wateko) wa koo zingine hadi mfumo wao ulipobadilika kutokana na ujio wa jamii ya Wahima/Watutsi ambao walifika na kuanzisha mfumo mwngine wa utawala.

Katika miaka hiyo eneo lote la Buha lilikuwa na kabila moja tu la Waha lililoishi hapo. Hivyo ujio wa Watutsi ndiyo uliosababisha mwingiliano wa kwanza wa jamii ya watu wasio Wabantu katika eneo hilo la Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.

Kuanzia hapo Waha walianza kupoteza umaarufu wao wa mfumo wa utawala wa ukoo/ Wateko.

Mfumo wa Watutsi ulichukua nafasi na Buha ikaangukia katika mikono ya watawala wa Mwami. Katika nyakati tofauti tofauti tawala ziliundwa katika eneo lote la Buha.

Tawala zilizoanzishwa katika eneneo lote la Buha zilikuwa 6; Utawala wa Heru (Ikulu yake Heru Juu pamoja na sehemu ya mipaka yote ya Manyovu, Kasulu Vijijini na Kasulu Mjini); Muhambwe (Ikulu yake Kibondo na sehemu za Wilaya ya Kibondo); Buyungu (Ikulu yake Kakonko na sehemu za mipaka yote ya Wilaya ya Kakonko) na Ujiji (Ikuu yake Nkalinzi na sehemu zote za mipaka ya Kigoma Vijijini, Manispaa ya Kigoma/ Ujiji na Wilaya ya Uvinza).

Nyingine zilizomeguka kutoka kwenye utawala wa Heru ni Nkanda-Luguru (Ikulu yake Nkanda na maeneo yote ya mipaka yake) na Heru-Ushingo (Ikulu yake Heru Ushingo).

Shughuli za kiuchumi

Shughuli kuu za kiuchumi za Waha ni kilimo cha mahindi, maharage, ndizi, kahawa, mhogo, karanga, mbaazi, njegere, viazi mviringo, viazi vitamu, mtama, ulezi, mahore, miwa, mpunga, korosho n.k.

Pia Waha ni wavuvi wa samaki katika Ziwa Tanganyika, Mto Malagarasi, Mto Rwiche, Mto Mkoza, na mito mingine midogomidogo kama vile, Nyajijima, Mresi, Kazingu na mingineyo.

Mbali na ukulima na uvuvi Waha ni wafugaji wa ng'ombe, mbuzi, kuku, bata, nguruwe, sungura, mbwa, paka na Wanyama wengineo.

Biashara zao ni mazao wanayoyalima, samaki, na bidhaa nyingine za kawaida.

Usafiri wao wa asili ulikuwa wa miguu yao wenyewe, ambapo kuna imani ilikuwepo pia ya kusadikika kuwa walitumia ungo kusafiria kama ndege yao ya asili.

Utamaduni wao, yaani mavazi yao ilikuwa ni magome ya miti yaliyojulikana kama mpuzu, na nyumba zao ni za msonge, udongo na miti, kulingana na sehemu mbalimbali, maana kuna sehemu zenye joto kama vile bondeni, na sehemu zenye baridi kama vile nyanda za juu.

Chakula cha asili cha Waha

Chakula cha asili cha kabila la Waha (na nchi za Rwanda, Burundi na Congo) ni samaki aina ya migebuka wanaopatikana Ziwa Tanganyika na ‘ugali wa rowe’ (unatokana na muhogo).

Baada ya kupikwa unahifadhiwa kwenye majani maalumu ya mgomba na unaliwa kwa mboga ama bila mboga, pia unaweza kusafiri nao popote kwenye begi

Ugali huu hauwezi kuharibika hata ukikaa mwezi mzima, ni ugali unaotengenezwa kutokana na muhogo na masharti yake ni kwamba usihifadhiwe kwenye jokofu ama sahani. Ugali huu huandaliwa kwa siku nne mpaka saba.

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari.

0685 666964 au bhiluka@gmail.com

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/7b888f914cd7b84bce32ed75ba34c4e7.jpg

*Ni salama asilimia 99.99

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi