loader
Dstv Habarileo  Mobile
Tunapozungumzia uharibifu  wa misitu tusisahau kilimo

Tunapozungumzia uharibifu wa misitu tusisahau kilimo

MISITU ni mkusanyiko wa uoto unaojumuisha miti mingi ambamo pia hupatikana mimea mbalimbali zikiwemo nyasi fupi au ndefu. Ndani ya misitu pia kuna viumbe hai kadha wa kadha.

Misitu inaweza kuwa ya asili ikiwa na miti mbalimbali kama vile mipingo, mikoko, miyombo, migunga na mingine mingi au yaweza kutokana na miti ya kupandwa na binadamu kama misaji, mikaratusi na kadhalika.

Misitu ya asili ni kama vile msitu wa Udzungwa ulioko Morogoro na ya kupadwa ni kama vile Tongwe na Nilo iliyoko Muheza na Korogowe mtawalia, mkoani Tanga.

FAIDA ZA MISITU

Misitu ina faida nyingi kwa mwanadamu na viumbe wengine, baadhi ya hizo ni kunyonya hewa chafu na kutoa hewa nzuri kwa mwanadamu, kusababisha vyanzo vingi vya maji, kuwa makazi ya viumbe mbalimbali na ndani ya misitu hupatikana aina mbalimbali za miti ikiwemo miti dawa au inayotoa mbao.

Misitu pia hutupatia nishati ya kupikia (kuni na mkaa, husaidia kuzuia mmomonyoko wa udongo, huwezesha ufugaji wa nyuki huwa chanzo cha kuvuta mvua na pia misitu ni kivutio cha utalii.

Kwa mantiki hiyo, mwanadamu hutegemea sana uwepo wa misitu kwa mustakabali wa maisha yake kutokana na faida lukuki anazopata. Kwa lugha nyingine misitu ni uhai.

MADHARA YA KUMALIZA MISITU

Pamoja na umuhimu huo wa rasilimali misitu, dunia imeendelea kushuhudia uharibifu mkubwa wa misitu ambao unatokea kila kukicha, hali ambayo inatoa ujumbe wa hatari kwa siku zijazo kuhusu mazingira.

Mbali na kukosa faida luluki za misitu pale inapoharibiwa kama ilivyoelezwa tayari, kuna tatizo kubwa ambalo dunia inakabiliana nalo sasa la mabadiliko ya tabianchi, linalochangiwa kwa kiwango kikubwa na uharibifu wa mazingira ikiwemo uharibifu wa misitu, hali ambayo inasababisha ongezeko la joto duniani.

Nchini Tanzania, kwa takwimu zilizopo kiasi cha hekta 469 za misitu, ukubwa ambao ni mara tatu ya ukubwa wa jiji la Dar es Salaam, hupotea kila mwaka nchini Tanzania kutokana ukataji wa miti usio endelevu.

NINI KINACHOMALIZA MISITU?

Watu wengi ukiwauliza swali ni kitu gani hasa kinachoongoza kwa kusababisha uharibifu mkubwa wa misitu, watatupa lawama kwenye ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa, mbao au kuni.

Lakini ukweli si hivyo. Kinachoongoza katika uharibifu wa misitu kwa mujibu wa tafiti zilizopo ni kilimo, hususani kilimo cha kuhamahama. Kwamba wakati ukataji mkaa unaweza kuruhusu msitu kuota upya, kilimo huondoa kabisa msitu!

Pamoja na watu kutegemea rasilimali za misitu kuendesha maisha yao, asilimia kubwa ya Watanzania hutegemea kilimo ili kujipatia mahitaji yao ya kila siku. Kilimo hutoa chakula, kilimo ni biashara na kilimo hutoa mali ghafi kwa ajili ya viwanda vyetu.

Kilimo katika nchi za Afrika ambazo ziko nyuma katika utumiaji wa teknolojia za kisasa unaowezesha eneo dogo kuzalisha mazao mengi, kimekuwa kila wakati ni chenye kuhitaji eneo kubwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Charles Meshack anasema mahitaji ya ardhi kwa ajili ya mashamba ya kilimo yanachangia upotevu wa misitu kwa asilimia 80 wakati mkaa ambao unanyooshewa sana kidole ni chini ya asilimia 10.

Meshack amebainisha hayo hivi karibuni alipozungumza na wabunge wa Jamhuri ya Muungano ambao ni wajumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii jijini Dodoma.

Anasema kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanywa na TFCG na taasisi nyingine zimeonesha upotevu mkubwa wa misitu nchini unasababishwa na kilimo hasa cha zao la mahindi.

Anasema asilimia kubwa ya upotevu huo unatokea hasa katika maeneo ambayo misitu yake haina mfumo wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ).

Meshack anasema utafiti unaonesha kuwa Tanzania ina jumla ya hekta milioni 48 za misitu ambapo asilimia 47 ya misitu hiyo ipo katika ardhi za vijiji na kwamba ni hekta milioni mbili pekee ndizo zipo kwenye usimamizi shirikishi (USMJ).

Meshack anasema iwapo hakutakuwa na jitihada za kuilinda, kuitunza na kuindeleza, baada ya miaka 40 ijayo misitu itatoweka kabisa nchini.

Mkurugenzi huyo anasema mfumo wa USMJ umeweza kuchochea uhifadhi, ulinzi na utunzaji huku maendeleo yakipatikana.

“Ushahidi upo kuwa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii umeweza kuongeza thamani mazao ya misitu nchini, lakini pia miradi ya elimu, afya, maji, uhifadhi ikifanikishwa kwa uendelevu," anasema.

USIMAMIZI SHIRIKISHI UNAFANYIKAJE?

Usimazizi shirikishi ni pale wananchi, wanapowezeshwa kupitia elimu kuona manufaa ya msitu unaowazunguka na kugeuka kuwa walinzi thabiti wa msitu huku wakuvuna raslimali za misitu kwa njia endelevu.

Mfano wake unapatikana katika vijiji zaidi ya 30 katika wilaya za Kilosa, Mvomero na Morogoro vijijini mkoani Morogoro ambako vijiji vingine nchini vinaweza kwenda kujifunza.

Vijiji hivyo, kwanza vina mpango wa matumizi bora ya ardhi. Baada ya kupimwa kijiji hutenga eneo kwa ajili ya msitu, eneo mashamba, malisho, makazi na huduma za jamii.

Kupitia mradi wa Kuleta Mabadiliko Katika Sekta ya mkaa nchini (TTCS), vijiji hivyo viliwezeshwa na TFCG kwa kushirikiana na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) kuzalisha mkaa kwa njia endelevu.

Baada ya kumalizika kwa TTCS katika vijiji hivyo darasa, sasa TFCG na Mjumita wananaendesha mradi wa kuhifadhi misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya mazao ya misitu (CoForEST).

Kinachofanyika msituni eneo la asilimia 10 la msitu wa kijiji ndilo hutengwa kwa ajili ya uzalishaji mkaa miaka yote. Mkaa huzalishwa kitalaamu kwa kuruhusu miti kukua na kuzaliana upya na hivyo uzalishaji kuwa endelevu. Pia uchomaji wa mkaa hutumia tanuri kichuguu ambalo hutoa mkaa mwingi mzuri.

Katika eneo hilo la asilimia 10, kunatengwa vitalu vya mita 50 kwa 50 vinavyovunwa kwa kuruka. Kama kitalu A kinavunwa leo, B kinarukwa hadi C na Bi kitarejewa baada ya miaka 12 katika mzunguko wa miaka 24 ambapo kitalu kilichokatwa leo huwa kimerejea kuwa msitu mkubwa.

Miti yenye sifa tu ndio inayovunwa kwa ajili ya mkaa. Miti inayofaa kwa mbao inaachwa au iliyo katika vyanzo vya maji au makazi ya viumbe wengine kama nyuki pia haiguswi.

JE, WANANCHI WAAACHE KILIMO?

Wanachi katika vijiji hivyo pia wamejifunza kilimo hifadhi kinachowawezesha kulima eneo dogo kisasa ili kupata mazao mengi. Wamejifunza pia ufugaji wa kisasa wa nyuki na kufungua vikundi hisa vya kuweka na kukopa. Hatua hizo zinasaidia kuwapa kipato mbadala badala ya kutegemea misitu kiwa kiwango kikuwa.

Asilimia 60 ya mapato ya kijiji hutumika kulinda misitu kupitia kamati mbalimbali na asilimia 40 hupelekwa kwenye miradi ya maendeleo ambayo Meshack anaitaja kwamba ni pamoja na ujenzi wa shule, madarasa, kulipia bima wananchi na mingineyo.

Ukitembelea vijiji hivyo utagundua kwamba misitu inalindwa vyema kulinganisha na vijiji visivyo na USMJ na hii inaonesha kwamba wananchi wanaposhirikishwa na kuona faida ya kufanya uzalishaji endelevu, huwa ndio walinzi namba moja wa misitu yao.

TAASISI YA MPINGO NA USMJ

Mkurugenzi wa Shirika la Mpingo na Maendeleo (MCDI), Jasper Makala anasema kupitia USMJ wameweza kulinda misitu na kukuza kipato kwa wananchi wanaozungukwa na misitu.

Anasema MCDI maarufu Mpingo, imekuwa ikijijita kutoa elimu namna ya kukabiliana na moto, kuunganisha wanakijiji na masoko ya mazoa ya misitu na uhifadhi wa mazingira.

Anasema wamewezesha mapato ya vijiji kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 60 baada ya kuwawezesha kuachana kuuza magogo.

Makala anasema MCDI kwa kushirikiana wadau mbalimbali kama Program ya Kuongeza Mnyororo wa Thamani (FORVAC) na WWF wameweza kutoa mashine nne za Norwood ambazo zinaongeza thamani ya mazao ya misitu kwa asilimia 60.

Mkurugenzi Mkuu Mjumita, Rahima Njaidi anasema USMJ umegawanyika katika maeneo mawili muhimu ambayo ni vijiji na halmashauri za miji kusimamia misitu na USMJ.

Anasema Mjumita na wadau wengine walikuja na USMJ ili kuhakikisha rasilimali misitu inakuwa salama.

“Tumekuwa tukisimamia uhifadhi, utunzaji na uendelevu wa misitu kwa kuafuata Sheria ya Misitu ya mwaka 2002, Sera ya misitu ya mwaka 1998 pamoja na kanuni zake kuhakikisha rasilimali hiyo inanufaisha watu wote na nchi,” anasema.

Anasema serikali haina uwezo wa kulinda misitu yote na hivyo USMJ kubaki kuwa nyenzo muhimu na madhubuti kwa ulinzi wa misitu.

Mbunge wa Lulindi, Issa Mchungahela anasema USMJ inapaswa kusambaa nchini kote kwa kuwa inagusa maisha ya wananchi.

Mchungahela anasema miradi hiyo ni moja ya maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo juhudi zinahitajika utekelezaji unafanyika.

Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima anasema misitu ni muhimu kwa maisha ya binadamu hivyo inapaswa kutunzwa kwa nguvu zote.

Hivyo katika kutimiza upatikanaji wa chakula kwa wingi ni lazima misitu ilindwe kwa nguvu zote katika ukuaji na ustawi wa jamii, la sivyo maisha ya viumbe vyote yatakuwa hatarini.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/415fece399df8acc8c930c8311da9f03.jpg

*Ni salama asilimia 99.99

foto
Mwandishi: Suleiman Msuya

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi