loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wataalam wachambua kodi, vyanzo vya mapato na udhibiti matumizi Bajeti 2021/22

Wataalam wachambua kodi, vyanzo vya mapato na udhibiti matumizi Bajeti 2021/22

WATAALAMU wa masuala ya uchumi na fedha nchini wamebainisha hoja tatu muhimu za kodi na mapato kwenye Bajeti ya Serikali ya 2021/22 na kutoa mapendekezo kwa serikali juu ya uboreshaji mifumo ya usimamizi na ukusanyaji kodi ili kupanua wigo wa kodi nchini.  

Katika uchambuzi huo uliofanywa na Taasisi ya Wajibu umetoa mapendekezo kwenye vyanzo vipya vya mapato, kodi za biashara mitandaoni na udhibiti wa matimizi ya mapato.

Katika jukwaa hilo la uwasilishwaji wa uchambuzi wa Bajeti ulifanyika jana mkoani Dar es Salaam chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wajibu, Ludovick Utouh akishirikiana na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Tawi la Dar es Salaam, Profesa wa Uchumi, Honest Ngowi ulipendekeza yafuatayo.
Utouh ambaye aliwahi kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alisema uchambuzi wao umebaini bajeti hiyo imeweka malengo ya jumla yanayojumuisha kuboresha mifumo ya usimamizi na ukusanyaji kodi ili kupanua wigo wa kodi.

BIASHARA MTANDAONI
Utouh ambaye ni mtaalamu wa masuala ya fedha alisema Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA), ifanye uwekezaji mkubwa katika kujenga uwezo wa kutambua na kutoza kodi biashara zinazofanyika kupitia mtandao ambazo zinakua kwa kasi kubwa nchini.

Utouh pia alilishauri Bunge kupitia Kamati yake ya Bajeti kufanya usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa bajeti itakayoidhinishwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa kuhakikisha linapitia ripoti za utekelezaji wa bajeti za robo mwaka zinazotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango.

UDHIBITI MATUMIZI

Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Ngowi alielekeza uchambuzi wake kwenye mikakati ya kudhibiti matumizi ambapo alisema bajeti hiyo inalenga kuelekeza fedha kwenye maeneo ya kipaumbele yatakayochochea ukuaji wa uchumi na kuhakikisha miradi inayoendelea inapewa kipaumbele kabla ya kuanzisha miradi mipya.
Profesa Ngowi alisema mkakati mwingine uliowekwa kwenye bajeti hiyo ni kudhibiti uzalishaji na ulimbikizaji wa madeni, kuendeleza nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na kuongeza matumizi ya Tehama katika usimamizi wa fedha za umma akiona kama kiashiria kitakachosaidia katika kukuza uchumi kwa kuwa na mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji.

VYANZO VINGINE VYA MAPATO
Utouh alishauri Serikali kuanza mazungumzo ya kuuziana bidhaa na huduma za ziada zinazotokana na miradi ya kimkakati, mfano umeme na usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya kisasa (SGR).
Utouh alisema hatua hiyo itasaidia kuihakikishia serikali kuwa na fedha za kigeni za kuhudumia madeni yanayotokana na miradi hiyo pindi yatakapoanza kulipwa.
"Serikali ihakikishe inaziongeza uwezo wa kifedha, watumishi na miundombinu mahakama za usuluhishi wa kodi ili ziweze kusikiliza na kuamua mashauri ya kodi ambapo hivi sasa kuna shilingi trilioni 360.08 na Dola za Marekani milioni 181.43 viporo vya kufanyiwa uamuzi ili serikali ipate mapato stahiki kutoka katika mashauri hayo," alisema.

Utouh pia alisema serikali inapaswa kupunguza idadi ya miradi inayopangwa kutekelezwa kwa mwaka ili kuipa nafasi kutenga kiasi kikubwa zaidi katika kutekeleza miradi michache ambayo itakamilika kwa wakati.

MAENEO YA KUBORESHA
Aidha Utoah alishauri Serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara, kuimarisha uendeshaji wa mashirika ya umma ili yafanye kazi kibiashara, kuongeza uzalishaji wa mazao ya sekta za mifugo, kilimo na uvuvi, na kuchochea uwekezaji hasa katika viwanda vinavyotumia malighafi za ndani.

Pia aliyataja maeneo mengine kuwa ni kupambana na utoroshaji wa madini na kujenga mitambo ya uchenjuaji wa madini nchini, kuboresha miundombinu ya sekta za usafirishaji na nishati, kuboresha utoaji wa huduma za kijamii katika sekta za afya, elimu na maji pamoja na kuimarisha uhusiano wa kimataifa.

"Kwa ujumla, tunaipongeza serikali kwa kukamilisha uandaaji wa bajeti ya mwaka 2021/22 pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato, mfano kodi ya laini za simu, hati fungani za manispaa pamoja na tozo ya pango kupitia Luku za umeme," Utouh alihitimisha.
Katika bajeti hiyo, Serikali imependekeza kutumia Sh trilioni 36.329, ambapo kati yake, asilimia 63 ilielekezwa kwa matumizi ya kawaida na asilimia 37 kwa ajili ya maendeleo.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/e313d726099ece3c825b4f976910e065.jpeg

MKUU wa Chuo cha Uhasibu Arusha ...

foto
Mwandishi: Alfred Lasteck

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi