loader
Dstv Habarileo  Mobile
Metacha afungiwa, aomba radhi

Metacha afungiwa, aomba radhi

UONGOZI wa klabu ya soka ya Yanga umemsimamisha kipa wake namba moja, Metacha Mnata, kufuatia kitendo alichokifanya cha kuwaonesha mashabiki wa timu hiyo kidole cha kati baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting, ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Kipa huyo ambaye pia anaichezea timu ya taifa alifanya tukio hilo baada ya mashabiki wa timu yake kutoridhishwa na kiwango alichokionesha, ikiwemo kuruhusu mabao mepesi, ambayo yaliiweka timu yao kwenye presha ya kupata pointi tatu.

Taarifa iliyotolewa na klabu ya Yanga, muda mfupi baada ya tukio hilo imeeleza kusikitishwa na kitendo kilichofanywa na mchezaji huyo na wamechukua jukumu la kumsimamisha kutoa huduma mpaka pale suala lake watakapolifikisha mbele ya Kamati ya Nidhamu na kujadiliwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu za klabu hiyo.

Katika taarifa hiyo uongozi umewaomba radhi wanachama, wapenzi na mashabiki, wadau na wanamichezo kwa ujumla kwa kitendo ambacho siyo cha kiungwana na hakikutakiwa kufanywa na mchezaji kama yeye.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa timu hiyo Nasreddine Nabi, alikiri kipa wake kufanya makosa, lakini akawatupia lawama mashabiki wa timu hiyo kwa kumzomea mchezaji huyo badala ya kumpa sapoti ili azidi kujituma.

“Ni kweli Metacha alifanya makosa, lakini kwenye mpira vitu kama vile hutokea kwa mchezaji yeyote, walichokosea mashabiki wetu ni kumzomea badala ya kumpa sapoti ili alichokifanya kisijirudie tena, naweza kusema wao ndio wamempanikisha na kufanya kitendo kile,” alisema.

 “Nitoe mfano hivi chukulia wewe nyumbani kwako unapoishi inapotokea unafanya kosa alafu majirani zao wanakuzomea badala badala ya kukupa sapoti utajisikiaje? Ndicho walicho kosea mashabiki wa Yanga wanapaswa kutambua kwamba Metacha ni binadamu anakosea pia,” alisema Nabi.

Hiyo ni mara ya tatu kwa Metacha kuingia kwenye mgogoro na uongozi wa Yanga, mara ya kwanza ilikuwa ni katika sare ya 1-1 na Polisi Tanzania na baada ya kulaumiwa kufungwa bao jepesi, aliandika ujumbe kwenye mtandao wake wa kijamii wa Instagram, akiwaaga mashabiki wa timu hiyo.

 Tukio la pili alipoondolewa kambini mkoani Shinyanga, ambapo Yanga ilikwenda kucheza mechi  ya robo fainali ya Kombe la FA na Mwadui FC, ambapo siku moja kabla ya mchezo alikutwa amelewa na kocha kuamuru aondolewe kambini  arudishwe Dar es Salaami yeye na Michael Sarpong.

Aidha, kocha huyo aliuzungumzia mchezo huo dhidi ya Ruvu  Shooting, na kusema timu yake pamoja na ushindi lakini ilicheza kwa asilimia 40 tu kati ya 100, kutokana na namna ambavyo aliwaelekeza lakini hiyo ilitokana na uchovu wa baadhi ya wachezaji ambao walikuwa kwenye timu zao za taifa ingawa hilo haliwakatishi tamaa sababu lengo lao ni kushinda mechi zote zilizo salia kwenye ligi.

Aidha, kipa wa Yanga Metacha Mnata jana aliomba radhi kwa kitendo kisicho cha kiungwana cha kuwatukana mashabiki wa timu hiyo na kusisitiza kuwa alikosea kufanya hivyo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/ac07a1d084a446b222c1ff1d45161fd6.jpeg

AISHI Salum Manula sio jina geni ...

foto
Mwandishi: Mohamed Akida 

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi