loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mambo bambam viwanja vya Mwalimu Nyerere

Mambo bambam viwanja vya Mwalimu Nyerere

PILIKAPILIKA za mafundi katika viwanja vya Mwalimu Nyerere kunakofanyika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara Wilayani Temeke Jijini Dar es Salaam, zimetawala huku sauti za nyundo zikigongagonga misumari zikiashiria kuwa asilimia kubwa ya wadau wapo katika maandalizi kabambe ya kushiriki katika maonesho hayo.

Gazeti la HabariLEO limepita na kuzungumza na wasimamizi wa mafundi ambao walisema wamewahi kuanza maandalizi kwa sababu wamejifunza kutokana na usumbufu mkubwa walioupata katika maonesho yaliyopita.

Wamesema changamoto ya kuchelewa kufanya maandalizi ilikuwa ikileta usumbufu mkubwa kwa wateja kwa sababu wakati mafundi wa nje wakipaka rangi wafagizi wa ndani wanaendelea kufagia huku wateja wakitaka kuhudumiwa hali iliyoleta usumbufu kwao na kwa wateja wao.

Mtaalamu wa wa kupaka rangi kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Malcomx Omari ameliambia Gazeti la HabariLEO kuwa maandalizi ya maonesho ya mwaka huu yameanza mapema ili kutoa nafasi kwa wateja wao kutembelea banda lao bila usumbufu.

Alisema mwaka huu wamejipanga kuja tofauti na mwaka jana kutokana na uwekezaji mkubwa waliowekeza katika ubunifu hivyo wananchi wote watakaotembelea banda la Veta wana uhakika wa kupata vitu adimu kuliko vya mwaka jana.

“Tumejipanga kuvunja rekodi yetu wenyewe, mwaka jana tulishika nafasi ya kwanza kwa kuwa na bidhaa bora na ubunifu mkubwa lakini mwaka huu tumedhamiria kuvunja rekodi yetu wenyewe kwa kuwaacha mbali kabisa wapinzani wetu lakini kubwa zaidi kukata kiu ya wananchi kwa kuleta bidhaa adimu ambazo wengi hawakudhani kuwa zitatengenezwa na Veta,” alisema Omari.

Kwa upande wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kimeridhishwa na mazingira yaliyowekwa na Tantrade ya kuwezesha maandalizi ya mapema kwa wadau kujenga miundombinu ya mabanda yao mapema kwani itawasaidia wananchi kufikia malengo yao yaliyowaleta.

Msimamizi wa Usafi na Mafundi wa chuo hicho Juma Ulochi alisema chuo kimejipanga kukamilisha maandalizi mapema ingawa fedha za maandalizi zinatoka katika bajeti ya mwaka huu wa fedha.

“Pamoja na kwamba fedha za bajeti bado hazijafika lakini tunajitahidi kuhakikisha kuwa hazileti athari katika maandalizi kuelekea Jumatatu siku ya ufunguzi,” alisema Ulochi.

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), limesema maandalizi ya mapema linayofanya ni ishara kuwa limejipanga kuleta vitu vya tofauti kwa Watanzania.

Msimamizi wa maandalizi katika banda la (JKT), alisema ingawa sio msemaji wa banda hilo lakini kutakuwa na vitu vya kuvutia vitakavyoleta changamoto kwa washiriki wa maonesho hayo.

Wasimamizi wa ukarabati katika banda la mahakama walisema maandalizi yanaendelea vizuri na hadi kufika Jumapili watakuwa wamekamilisha tayari kwa ajili ya ufunguzi siku inayofuata.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/3200c374d5400a2f6c94caa46b2b546a.jpg

MKURUGENZI wa Idara ya Diplomasia ya ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi