loader
FARAJA KOTTA: Mlimbwende aliyegeukia sekta ya elimu

FARAJA KOTTA: Mlimbwende aliyegeukia sekta ya elimu

TANZANIA ni nchi iliyojaliwa watu waliobarikiwa ubunifu, hata wakati wa changamoto mbalimbali zinapojitokeza.

Ugonjwa wa Covid-19 ulipoivamia dunia kwa mara kwanzam, Tanzania ilikuwa kati ya nchi zilizoguswa hadi kusababisha shule kufungwa na wanafunzi kubakia majumbani, jambo lililolazimisha wanafunzi kuendelea kujisomea kupitia huduma mtandao na kati ya huduma hizo ni Shule Direct.

Kupitia huduma ya Shule Direct wanafunzi walisoma na kuelewa masuala mbalimbali yahusuyo elimu na hivyo likizo hiyo ya dharura haikuisha kwa wao kukaa ama kucheza tu majumbani, ila walitumia muda mwingi kujisomea kwa njia ya mtandao.

Shule Direct ni wazo la Faraja Kotta na vijana wenzake, baada ya kuamua kuanzisha shirika hilo mwaka 2013 ikiwa miaka saba kabla ya ugonjwa huo kuingia hapa nchini mwezi Machi mwaka jana baada ya kulipuka kwa mara ya kwanza nchini China Desemba, 2019.

Faraja anasema kuwa tangu kuanzishwa kwa shirika hilo mwaka 2013 mpaka sasa watumiaji zaidi ya milioni tatu wameshatumia majukwaa ya kidijiti ya Shule Direct ambayo yanapatikana katika mifumo mbalimbali ukiwemo mtandao wa Intaneti (Wavuti).

Anafafanua kuwa licha ya kutumia mtandao wa intaneti pia wanaweza kutumia huduma ya elimu bila kutumia mfumo huo, badala yake wanaweza kutumia programu tumizi ya simu ya mkononi inayopatikana kwa kutumia simu janja au vishkwambi (tablets) na vile vile kwa njia ya huduma ya ujumbe mfupi wa maandishi (sms).

Kuhusiana na ubunifu huo na kwa nini ameamua kuanzisha mradi huo na siyo biashara nyingine, Faraja ambaye alikuwa Miss Tanzania 2004, anasema kuwa yeye ni mtu anayeamini kuwa maendeleo siyo mtu kuwa na mafanikio binafsi, isipokuwa ni kubadilisha maisha ya watu wengine hasa kwa kuwawezesha kupata maarifa ya maisha.

Anasema kuwawezesha kupata maarifa ni urithi ambao unaweza kudumu kwa mtu kwa miaka mingi zaidi na ndiyo maana ameamua kuwajengea uwezo wa kupata elimu bora zaidi kwa njia ya mtandao huku akifafanua kuwa kuna utofauti wa elimu kwa njia hiyo ya mtandao kutoka shirika lake na huduma nyingine.

Kwa mujibu wa Faraja, kupitia huduma ya elimu ya Shule Direct inayofanya kazi kwa ukaribu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa maana ya mitaala ya kufundishia, ila inamtumia mwalimu anayefundisha mtandaoni anayejulikana kwa jina la Ticha Kidevu.

Anasema kuwa mwalimu huyo amekuwa muhimu ambaye kwa kupitia jukwaa maalum kwa wanafunzi wa sekondari, Ticha Kidevu anafundisha masomo 13 ya kidato cha kwanza hadi cha nne kufuatana na mtaala wa taifa wa elimu ya sekondari. Faraja anasema kuendesha Shule Direct kwa muda mrefu alikaa na kuona kuwa bado kuna pengo katika elimu hasa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake hapa nchini.

Anasema kuwa amekulia katika mazingira yanayomfanya aone umuhimu wa mama katika kujiendeleza hasa kujishughulisha na masuala ya ujasiriamali.

Ndoto Hub

Anasema baada ya kupata matokeo chanya kutoka kwa wadau wa elimu na wengine ndani na nje ya nchi wakipongeza huduma yake ya elimu kupitia Shule Direct, alikaa na kuona kuwa kuna kitu kingine kimepungua katika elimu ya ujasiriamali kwa wanawake.

Faraja anasema kuwa pamoja na kutoa mafunzo kwa wanawake wajasiriamali pia hutumia mafunzo hayo kama sehemu ya kutengenezea maudhui ya mtandaoni kwa ajili ya kuwasaidia wanawake wengine wengi wasioweza kufika Ndoto Hub nao kujifunza.

Anasema, Ndoto Hub pia ni jukwaa linalowawezesha wanawake kupata fursa za masoko na mitaji, ambapo tangu mwaka 2018 hadi sasa imeshatoa mafunzo kwa wanawake zaidi ya 200 na kati ya hao waliohitimu ni karibu wa asilimia 60 yao wamesharasimisha biashara zao na kuzisajili.

Kwa kuwa lengo lake ni kuwafikia wanawake wengi, kwa sasa Ndoto Hub imefungua tawi lingine Arusha na pia wameanzisha Chuo cha Ubunifu, Ndoto Innovation College ambacho pia kiko mjini Arusha.

Faraja anasema, “ kwa kuwa lengo ni kuwafikishia wanawake wote nchini elimu ya ujasiriamali na kuwawezesha, ikaja hoja ya kuhakikisha kuwa wanawake hawa wanajengewa chuo ili wapate mafunzo ambayo yanatambulika zaidi hivyo kimefunguliwa Chuo cha Ndoto Innovation College jijini Arusha.”

Kwa kuwa wanawake wanaohitimu hupata uzoefu unaowawezesha kujiajiri lakini kuna haja ya kuwepo kwa One Stop Center itakayowezesha kupatikana kwa taarifa na kuwezesha usajili na kulipia ada na leseni mbalimbali za biashara kwa mifumo ya kidijiti.

Ndoto Hub imeshewanufaisha kielimu wanawake 61 huku 48 kati yao wakifanikiwa kuanzisha miradi yao ambayo inaendelea kufanya vema na wengine wakiwa wameajili watendaji wengine.

Faraja licha ya kuwaendeleza kupitia mradi wa Ndoto Hub na kwa sasa akiwa na Ndoto Hub College pia ameanzisha mpango wa kutembelea sehemu mbalimbali za kazi na kutoa mafunzo ya kiutaalamu kuhusiana na fani ya masoko, mawasiliano, biashara na huduma nyingine.

Waziri azungumzia jitihada hizo

Kwa kuwa jitihada za Faraja za kuchagiza maendeleo ya elimu kwa njia ya mtandao zinaonekana katika jamii, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile anasema Wizara yake imekiwekea kipaumbele kikubwa kuhakikisha kuwa wanawake nao wanapata fursa ya kushiriki katika shughuli za kidijiti hususan uchumi wa kidijiti.

Alifurahishwa na kazi ya Ndoto Hub na kutaka wanawake waendelee kushiriki katika uchumi wa kidijiti huku akigusia mpango wa Wizara yake kutengeneza namba maalum za simu zitakazotambulisha wafanyabiashara wa mitandaoni.

Anasema, “ kwa mfanyabiashara anayefanya biashara mtandaoni atatakiwa kuhakikiwa kabla ya kupewa namba hiyo ikiwa ni sehemu mojawapo ya kukabiliana na wimbi la wizi na uhalifu wa mtandaoni na kuwalinda wale ambao kweli ni wafanyabiashara na hivyo pia kumlinda mlaji”.

Kuhusiana na Shule Direct, Ndugulile anasema “ni lazima wadau kuendelea kutengeneza maudhui ya kimtandao yetu wenyewe huku akielezea suala la gharama ambapo alieleza kuwa mtandao wa Internet umefikia takribani asilimia 60 ya nchi kwa kiwango cha 3G lakini takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia 28 tu ya watanzania ndio wanatumia Internet kila siku.

Anasema kwa kutambua nafasi ya teknolojia kama hiyo ya Shule Direct katika kusaidia maendeleo ya elimu, Wizara yake inaratibu mpango wa kuhakikisha Shule za Sekondari zinapatiwa kompyuta na zinakuwa na mtandao wa intaneti kuwezesha matumizi ya TEHAMA kama nyenzo ya kujifunzia na kufundishia mashuleni.

Faraja ni nani Faraja ambaye ni mama wa watoto wawili ameolewa na mwanasiasa, Lazaro Nyalandu na mbali masuala ya kijamii amekuwa akishiriki kikamilifu katika kuwafungua mawazo vijana kwa kushiriki mijadala mbalimbali ikiwa ni pamoja na umuhimu wa vijana wa Kitanzania kuwa wabunifu ili waweze kushindana katika nyanja za kimataifa pamoja na kunufaika na ubunifu wa kisayansi katika kuendeleza jamii ya Watanzania.

Anasema, “ yaani mimi hata uniambie sasa hivi kuwa kuna masuala haya na haya kuhusu maendeleo ya vijana, wanawake hata watoto nipo tayari kuzungumzia muda wowote tena hata bila ya kulipwa, kwa sababu bado ninaona kuna mengi kuhusiana na Watanzania ambayo yanapaswa kubadilishwa… mmi siyo kwamba ninajua kila kitu ila ninachoona kuwa bado Watanzania wanapaswa kuhamasishwa, katika masuala mbalimbali hasa kwenye kubainisha na kutumia fursa katika nyanja mbalimbali iwe utalii, sanaa, kilimo na mengine mengi.”

Kuhusiana na maisha yake binafsi Faraja anasema katika muda wake wa ziada hupenda kusoma mambo mbalimbali yanahusuyo uchumi, biashara, masuala ya elimu na hasa kusoma vitabu vilivyoandikwa na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, vinavyohusiana na masuala hayo.

Faraja pamoja na mambo mengine, anapendelea zaidi kujadiliana masuala ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kupokea changamoto mpya za maisha na kitaaluma. Mbali na hivyo anapenda kupika na pia Faraja ni mpenzi wa muziki hasa wa Bongo Fleva wenye maudhui ya kubadilisha maisha ya jamii huku akijinasibu kuwapenda wasanii wote wa muziki huo.

Faraja anasema kuwa mtu ambaye amekuwa akimvutia katika maisha ya siasa na jamii kwa ujumla ni Rais Samia Suluhu Hassan hasa kwa namna alivyoweza kuimudu siasa tangu akianza hadi kufikia hatua ya kuwa Rais wa Tanzania.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/50c27c15ba0a2f2785b014226ee45f7f.jpg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi